Katibu wa Bunge ataja maumivu ya Sera isiyozingatia uhalisia wa changamoto zinazowakabili wananchi

Imeelezwa kuwa sera isiyozingatia uhalisia wa changamoto zinazowakabili wananchi hupelekea utungwaji wa sheria isiyofaa na isiyojibu changamoto halisi za wananchi,anaripoti Victoria Kazinja (Diramakini) Morogoro.

Hayo yamebainishwa leo na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Stephen Kagaigai, wakati akifungua mafunzo ya uchambuzi wa sera na matumizi ya tafiti kwa watumishi wa Ofisi ya Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu mkoani Morogoro, ambayo yameandaliwa na Taasisi inayojishughulisha na Utafiti katika Masuala ya Uchumi na Maendeleo (REPOA).

Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai akizungumza wakati akifungua mafunzo ya uchambuzi wa sera kwa watumishi wa Ofisi ya Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu mkoani morogoro leo Oktoba 5,2020. (Diramakini).

Kagaigai amesema, watumishi hao wa Ofisi ya Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu wamepatiwa mafunzo hayo ili kuwapa nyenzo na kuwawezesha kutoa ushauri wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao bungeni, na kwa watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wanapokuwa wanatoa ushauri kwa mamlaka husika ipasavyo.

“Muunganiko wa hawa washiriki ni muhimu kwa vile maarifa yatakayopatikana yataleta uelewa wa pamoja na hivyo kuleta tija wakati wa utekelezaji wa majukumu yao katika ofisi zote mbili, REPOA toka imeanza imesaidia kuwajengea uwezo watumishi wa bunge pamoja na wabunge wenyewe kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya utungaji wa sera, sheria na mambo mengine yanayohusiana na maendeleo ya nchi,"ameeleza Kagaigai.

Aidha, amesema sera isiyozingatia uhalisia wa changamoto zinazowakabili wananchi itapelekea utungwaji wa sheria isiyofaa, na kwamba kutokana na hali hiyo ni muhimu sana washiriki wa mafunzo hayo wakawa na uelewa mpana kuhusu nafasi yao, ili hatimaye sera na sheria zinazotungwa ziakisi na kujibu changamoto halisi zinazowakabili wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dkt.Dolnad Mmari anasema kuwa, sera na mikakati mizuri ni lazima izingatie mahitaji ya watu na jamii kwa ujumla, huku ikizingatia mabadiliko katika mazingira ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ndani ya Afrika na Dunia kwa ujumla, pamoja na mabadiliko ya haraka ya teknolojia ili mipango hiyo ikidhi malengo yaliyokusudiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dokta Dolnad Mmari akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya uchambuzi wa sera kwa watumishi wa Ofisi ya Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu mkoani Morogoro leo Oktoba 5,2020. (Diramakini).

“Kwa kuwa Bunge la 12 limekaribia kuchaguliwa baada ya uchaguzi, na kwa vyovyote kutakuwa na mipango na sera mbalimbali zinapita kule bungeni, kwa hiyo ni vizuri sasa tukajaribu kukumbushana,”amesema Dkt.Mmari.

Pia anasema, REPOA katika kutekeleza mpango wake w anne wa kimkakati wa miaka mitano (2020-2024), imedhamiria kuimarisha uhusiano kati ya tafiti na sera za nchi, huku akisema lengo kuu ni kuchangia katika juhudi za kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi ili kuwa na maendeleo jumuishi, kama Dira ya Maendeleo 2025 inavyoelekeza.

Watumishi Ofisi ya Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mafunzo yaliyotolewa na REPOA juu ya uchambuzi wa sera yaliyofanyika mkoani Morogoro leo Oktoba 5, 2020. (Diramakini).

Hata hivyo, majukumu makubwa ya REPOA ni kujenga uwezo wa watafiti katika masuala ya kisera, na kufikisha matokeo ya tafiti hizo kwa watumiaji, ikiwa ni pamoja na watunga sera na wafanya maamuzi juu ya mipango na mikakati ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news