Wanajwangwani, Yanga SC wametoka nyuma na kushinda mabao 2-1 dhidi ya wenyeji waliowapeleka jijini Mwanza, KMC FC, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Ni katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza uliochezwa leo Oktoba 25,2020.Kwa ushindi huo,Yanga wanafikisha alama 19 katika mchezo wa saba, ingawa wanabaki nafasi ya pili, nyuma ya vinara, Azam FC waliokusanya alama zote 21 katika mechi saba wakati mabingwa watetezi,Simba SC wakiwa na alama 13 za mechi sita.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ramadhan Kayoko aliyekuwa anasaidiwa na Hamisi Chang’walu na Abdul Malimba wote wa Dar es Salaam KMC FC walitangulia kwa bao la Hassan Salum Kabunda 27'. Pengine kutangulia si kufika, ilikuwa hivi;
Kabunda ambaye ni mtoto wa beki wa Yanga SC miaka ya 1990, Salum Kabunda sasa marehemu alimtungua kipa Metacha Boniphace Mnata kwa shuti kali la umbali wa mita 22 baada ya kuwahadaa walinzi wa Yanga kufuatia kupokea pasi ya kiungo mwenzake, Kenny Ally Mwambungu.
Aidha, kipindi cha pili, Yanga
SC wakafanikiwa kupata bao la ushindi kupitia kwa mshambuliaji wake
mpya, Waziri Junior aliyemalizia kwa kichwa kona ya mtokea benchi Farid
Mussa Malik dakika ya 61.
Baada ya
kufunga bao hilo, Waziri, alivua jezi kuonyesha fulana iliyoandikwa “The
King of CCM Kirumba Stadium’, akimaanisha yeye ni Mfalme wa Uwanja huo
kutokana na rekodi yake ya mabao tangu akiwa anachezea Toto Africans na
Mbao FC zote za Mwanza ambazo zimeshuka daraja kwa sasa.
Wakati
huo huo, mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Timu ya Biashara United
imeshinda 1-0 dhidi ya wenyeji, Polisi Tanzania bao pekee la Deogratius
Judika Mafie 53' katika Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.
JKT Tanzania ikaichapa 6-1 Mwadui FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga mabao ya timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa yalifungwa na Adam Adam matatu dakika ya 24, 48 na 82, Danny Lyanga dakika ya 40 na 52 na Said Luyaya dakika ya 90 wakati la wenyeji limefungwa na Pastory Athanas dakika ya 62.
Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tatu, ikiwemo mabingwa watetezi, Simba SC kumenyana na Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Dodoma Jiji na Tanzania Prisons Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na Mtibwa Sugar na Azam FC Uwanja wa CCM Gairo.

