Rais Magufuli apokea hati za utambulisho za mabalozi watatu kutoka Uingereza, Pakistan na Uswisi

Leo Oktoba 5,2020 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Pombe Magufuli amepokea hati za utambulisho za mabalozi watatu walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho, Ikulu jijini Dar es Salaam ni David William Cancar (aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Uingereza hapa nchini),Muhammad Saleem (aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Pakistan hapa nchini) na Didier Chassot (aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Uswisi hapa nchini).

Mabalozi hao wameahidi kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi zao ikiwemo kuwashawishi wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza hapa nchini, kuvitangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika nchi zao, kununua bidhaa za Tanzania kama mazao ya kilimo na madini na kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wafanyabiashara wa nchi zao ili kukuza biashara kati ya Tanzania na nchi hizo.

Balozi wa Uingereza hapa nchini, David William Cancar amempongeza, Rais Magufuli kwa uongozi wake mzuri ambapo Tanzania kwa kufanikiwa kuingia katika uchumi wa nchi za kipato cha kati, kusambaza umeme kwa kasi kubwa, kutoa elimu bure, kujenga miundombinu hasa barabara, kupambana na rushwa na amekiri kuwa inauona utekelezaji wa kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”.

“Tumekuwa na mazungumzo mazuri na Mheshimiwa Rais Magufuli, tunatazamia kukuza zaidi uhusiano wa Uingereza na Tanzania hasa katika biashara, kwa sasa biashara yetu ni takribani shilingi Bilioni 390 kwa mwaka na pia tunachangia takribani shilingi Bilioni 800 kwa mwaka katika miradi mbalimbali ya maendeleo hapa Tanzania. Matarajio yangu ni kuwa tutaongeza zaidi,"amesema Balozi David William Cancar alipozungumza baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho.

Balozi wa Pakistan hapa nchini,Muhammad Saleem ameelezea kufurahishwa kwake na maendeleo ya Tanzania na ameahidi kuwaunganisha wafanyabiashara wa Pakistan na Tanzania ili kupanua zaidi uwigo wa biashara na kuongeza ununuzi wa bidhaa za Tanzania hasa kahawa, pamba, korosho na chai.

Balozi wa Uswisi hapa nchini,Didier Chassot amesema, Uswisi inao mkakati wa miaka minne ambapo atahakikisha utekelezaji wa mkakati huo unaleta manufaa yaliyotarajiwa hasa kwa kuzingatia vipaumbele vyake vya kuzalisha ajira, kuongeza kipato, kuboresha huduma za afya, na utawala bora.

Kwa upande wake Rais Magufuli amewapongeza mabalozi hao kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewaahidi kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wowote utakaohitajika katika utelekezaji wa majukumu yao.

Rais Magufuli amewataka kutoa kipaumbele katika uchumi kwa kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza hapa nchini ambapo watanufaika na uwepo wa malighafi, soko la uhakika na mazingira bora ya uwekezaji.

Pia Rais Magufuli amewaalika viongozi wakuu wa nchi hizo kutembelea Tanzania.Hafla ya kupokea hati za utambulisho za mabalozi hao zimehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Prof. Palamagamba Kabudi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news