Serikali ya Tanzania imesaini makubaliano ya awali na Kampuni ya Total East Afrika kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda kuja Chongoleani ,Tanga utakaogharimu kiasi cha dola za kimarekani Bilioni 3.5 sawa na sh. Trilioni 8 fedha za kitanzania,anaripoti Pamela Mollel (Diramakini),Arusha.
Akiongea na waandishi wa habari wakati wa kusaini mkataba huo jijini Arusha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Prof. Adelardus Kilangi amesema, majadiliano ya mradi huo yamefanywa na timu ya Serikali yakiongozwa na Mwanasheria Mkuu (AG) ambayo yamechukua wiki tatu huku nchi ya Uganda yakichukua miezi mitatu.
Prof.Kilangi amesema, awali Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni alikutana na Rais John Magufuli nyumbani kwake Chato Septemba 13, mwaka huu na kukubaliana kila nchi ifanye makubaliano ya haraka kwa upande wa mradi wa EACOP ili mchakato wake uanze mara moja.
Amesema, katika makubaliano hayo yamezingatia, haki ya ardhi,matumizi ya rasilimali za ndani,masuala ya afya, usalama na mazingira pamoja na viwango vya ajira.
"Bomba hilo lina urefu wa kilomita 1,445 ambapo mchakato wake unapaswa kukamilika ndani ya miezi minne au mitano ijayo na mradi unatarajiwa kuanza rasmi Februari mwakani 2021,"amesema Prof. Kilangi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi akiwa na Mwakilishi wa Total East Africa, Nicolas Terraz baada ya kukamilisha majadiliano na kutia saini mkataba wa nchi hodhi baina ya Total na Serikali ya Tanzania juu ya utekelezaji wa mradi wa EACOP.
Prof. Kilangi amezitaja faida za uwekezaji wa mradi huo ni pamoja na ajira 10,000 kwa watanzania,mapato ya kodi,ujenzi wa barabara na miundombinu mbalimbali, ujenzi wa bandari mpya, upatikanaji wa fursa mbalimbali za kibiashara, usafirishaji ,ulinzi, chakula na vinjwaji na mahoteli kwa ajili ya malazi.
Amesema, mradi huo ni kielelezo muhimu cha kupokea uwekezaji mkubwa na kuwakaribisha wawekezaji wengine kuja kuwekeza nchini kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Angelina Ngalula amempongeza Rais Magufuli na Rais Museveni kwa hatua ya kuingia mkataba wa makubaliano hayo kwani kwa wafanyabiashara ni fursa tosha ya kuzalisha mabilionea.
Amewataka wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa hiyo itakayopelekea kuzalisha mabilionea wengi nchini kupitia mradi huo wa bomba la mafuta.