Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi awataka wananchi kujitokeza kupiga kura

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mheshimiwa Jaji (Mst) Semistocles Kaijage amewataka Watanzania milioni 29,188,348 waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kupiga kura tarehe 28 Oktoba 2020 katika vituo 80,155 nchini, vitakavyofunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni, anaripoti Lilian Shembilu (MAELEZO).

Akizungumza na waandishi wa habari,Jaji (Mst) Kaijage, amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi tayari imekamilisha maandalizi yote muhimu ya mchakato huo vikiwemo vifaa vya uchaguzi.

“Vifaa vyote vimefikishwa kwenye halmashauri na kata mbalimbali na hivi sasa zoezi la kusambazwa vifaa hivyo kwenye vituo vya kupigia kura linaendele,” amesema Jaji (Mst) Kaijage.

Aidha, Jaji (Mst) Kaijage katika mkutano huo amesema kuwa kwa mujibu wa ratiba ya Uchaguzi Mkuu iliyotangazwa na tume, mwisho wa kampeni ilikuwa leo Tanzania Bara.

“Katika uchaguzi huu, vyama vya siasa 15 vimesimamisha wagombea katika nafasi ya Kiti cha Urais na Makamu wa Rais, aidha, vyama vyote 19 vyenye usajili wa kudumu vinashiriki uchaguzi huu kwa kusimamisha wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi na kuna jumla ya wagombea 1,257 katika nafasi ya Ubunge na kuna jumla ya wagombea 9,237 katika nafasi ya udiwani,” ameongeza Jaji (Mst) Kaijage.

Jaji (Mst), alibainisha kuwa tume imechambua takwimu kwa kuangalia pia uwiano wa kijinsia katika nafasi zote za uongozi zinazogombewa. 

Wagombea wanawake katika Kiti cha Rais ni 2 kati ya 15, sawa na asilimia 13, kwa nafasi ya Kiti cha Makamu wa Rais wanawake ni 5 kati ya 15, sawa na asilimia 33. 

Kwenye nafasi ya ubunge wanawake walioteuliwa ni 294, sawa na asilimia 23, kwa madiwani wanawake walioteuliwa ni 669, sawa na asilimia 7.2 ya wagombea wote.

Jaji (Mst) Kaijage amevipongeza Vyama vya Siasa na Wagombea waliojitokeza kuchukua fomu na hatimae kuteuliwa kuwa wagombea katika nafasi mbalimbali, lakini pia amewapongeza wananchi wote, kwa utulivu wakati wote wa kipindi cha kampeni.

“Kwa mara nyingine natoa rai kwa wapiga kura wote nchini kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura ili kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka. Kumbuka kura yako sauti yako, nenda kapige kura,"amesema Jaji (Mst) Kaijage.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here