Watumishi Sekta ya Maji watakiwa kuacha kuzoea matatizo ya wananchi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amezitaka Bodi za Wakurugenzi za Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Nchini kuhakikisha watumishi wanaacha tabia ya kuzoea matatizo ya wananchi na badala yake wayatatue kwa wakati, anaripoti Mohamed Saif, Mwanza.

Ametoa maelekezo hayo Oktoba 5,2020 mkoani Mwanza wakati wa kufungua mafunzo ya Bodi za Wakurugenzi na Menejimenti za Mamlaka 14 za Majisafi na Usafi wa Mazingira kutoka Kanda ya Ziwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akizungumza na washiriki wa mafunzo ya Bodi za Wakurugenzi na Menejimenti za Mamlaka 14 za Majisafi na Usafi wa Mazingira kutoka Kanda ya Ziwa.
“Wananchi wakati mwingine wamekuwa na malalamiko mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa huduma ya maji ama kero zingine na wakati huohuo unakuta watumishi wanaopaswa kutatua wamejenga tabia ya kuzoea malalamiko hayo, sasa Bodi mnapaswa kusimamia ili watendaji wasizoee shida za wananchi,”ameelekeza Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga amesisitiza kwamba, wajibu wa Bodi za Mamlaka za Maji ni kusimamia shughuli zote za uendeshaji wa mamlaka kwenye utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

“Natambua Bodi sio watendaji ila wasimamizi, mnapokea taarifa za utendaji sasa nawasihi msiwe Bodi za kupokea tu taarifa za kila baada ya miezi mitatu muende hatua zaidi hasa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma yenye kiwango,”amesisitiza Katibu Mkuu Sanga.

Amesema, lengo la Wizara ya Maji kupitia Mamlaka za Maji kote nchini ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na toshelevu ya majisafi na salama na kwamba ili kufikia lengo hilo bodi zinapaswa kuwawajibisha watumishi watakaofanya kazi kinyume na utaratibu.

Washiriki wa mafunzo ya Bodi za Wakurugenzi na Menejimenti za Mamlaka 14 za Majisafi na Usafi wa Mazingira kutoka Kanda ya Ziwa wakifuatilia mafunzo.
“Muda mwingine mtumishi anamjibu mwananchi jibu lisiloeleweka na mwananchi hana sehemu nyingine ya kwenda kupeleka malalamiko yake. Mwananchi kama analalamika hapati huduma wakati bodi ipo, menejimenti ipo inamaana bodi haitusaidii. Ninazielekeza bodi zichukue hatua, mtumishi ambaye hatimizi wajibu wake awajibishwe hata ikibidi kusimamishwa kazi,”amesisitiza Mhandisi Sanga.

Vilevile amezielekeza bodi kuhakikisha zinajikita kwenye ukaguzi wa mara kwa mara wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili kujiridhisha na ujenzi wake badala ya kusubiri taarifa kutoka kwa watendaji hasa ikizingatiwa Serikali inapeleka fedha nyingi kwenye ujenzi wa miradi.

Washiriki wa mafunzo kutoka Mamlaka ya Maji Musoma katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (aliyekaa katikati) na viongozi wengine.
“Zaidi ya asilimia 70 ya matumizi ya mamlaka za maji ni ya manunuzi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini je ni mara ngapi Bodi zinatembelea hii miradi? Ni muhimu Bodi kufika kujionea ujenzi na kukagua thamani halisi ya fedha inayotumika badala ya kuishia kusoma kwenye taarifa za watendaji,”amesisitiza Katibu Mkuu Sanga.

Mhandisi Sanga hakuishia hapo badala yake amezielekeza Mamlaka za Maji zihakikishe zinawasilisha taarifa sahihi kwenye Bodi na lakini pia Bodi nazo kuhakikisha zinakagua vitendea kazi vya kila siku ikiwemo mitambo ya kusukuma maji ili kujiridhisha ufanisi wake kulingana na taarifa zinazotolewa na watendaji.

Washiriki wa mafunzo kutoka Mamlaka ya Maji Mwanza katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (aliyekaa katikati) na viongozi wengine.
Aidha, maelekezo mengine ya kiutendaji yaliyotolewa na Katibu Mkuu Sanga ni pamoja na kuhakikisha Mamlaka zinakuwa na mpango wa kupanua utoaji wa huduma katika maeneo yao ya huduma, michango ya fedha kwenye mifuko ya kijamii inawasilishwa kwa wakati, mikakati madhubuti ya kupunguza upotevu wa maji inawekwa.

Vilevile kuhakikisha huduma ya maji na usafi wa mazingira inapatikana kwenye taasisi nyeti kama vituo vya afya, vyuo, magereza pamoja na shule za msingi na sekondari zisizo na huduma hizo.

Amezitaka Bodi kufanyia kazi malakamiko ya watumishi pia, “Bodi inauwezo wa kuajiri na kufukuza sasa ikitokea kuna mtumishi hafanyi vizuri achukuliwe hatua akae pembeni apishe wenye kutaka kufanya kazi,” alielekeza Katibu Mkuu Sanga.

Washiriki wa mafunzo kutoka Mamlaka ya Maji Shinyanga katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga na viongozi wengine.
Amesema Bodi zikitimiza wajibu wake inavyopasa, ni dhahiri huduma za maji kote nchini zitaimarika na hivyo kupunguza malalamiko miongoni mwa wananchi na hivyo alizikumbusha katika kutekeleza majukumu yake zihakikishe zinatanguliza maslahi ya wananchi.

Akizungumzia juu ya mafunzo aliyoyafungua, Katibu Mkuu Sanga amewakumbusha washiriki wote wa mafunzo kuzingatia mada zitakazowasilishwa na wataalam mbalimbali ili kuhakikisha huduma ya maji ina imarika.

Washiriki wa mafunzo kutoka Mamlaka ya Maji Bukoba katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga na viongozi wengine.
“Ni matarajio yangu mtakuwa wasikivu na mtazingatia mafunzo ili hatimaye kwa pamoja mpate dira sahihi ya utekelezaji wa majukumu yenu. Tunasisitiza ushirikiano baina ya Bodi, Menejimenti na watumishi na fanyeni maamuzi yenye maslahi mapana kwa wananchi na sio maslahi binafsi,”amesisitiza Mhandisi Sanga.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanatolewa kwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za Maswa, Shinyanga, Bukoba, Mwanza, Kahama, KASHWASA, Musoma, Bunda, Bariadi, Sengerema, Geita, Muleba, Biharamulo na Mugango-Kyabakari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news