Rais Dkt.Mwinyi aeleza Zanzibar mpya itakavyokuwa miaka mitano ijayo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameahidi kuijenga Zanzibar mpya kwa kupitia uchumi wa kisasa wa Buluu (Blue Economy), anaripoti Mwandishi Diramakini.
Ahadi hiyo ameitoa leo Novemba 11,2020 katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la 10 la Wawakilishi lililofanyika huko katika ukumbi wa baraza hilo Chukwani, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.

Hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzzibar, Amani Abeid Karume, Dkt.Ali Mohammed Shein, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mama Maryam Mwinyi, wake wa Marais wastaafu, mabalozi na viongozi wengineo.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dkt. Hussein amesema kuwa, moja ya ahadi yake kubwa aliyoitoa kwa wananchi na ambayo imeelezwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kujenga uchumi wa kisasa wa Buluu.

Amesema kuwa Uchumi wa Buluu ama uchumi wa bahari unafungamanisha kwa pamoja sekta za uvuvi, ufugaji samaki, ujenzi wa viwanda vya samaki, ukulima wa mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi, matumizi bora ya rasilimali mbali mbali za bahari pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini.

Ameongeza kuwa, uchumi wa Buluu haukamiliki bila ya kuwepo kwa Bandari za kisasa zenye ufanisi wa hali ya juu.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dkt.Hussein Mwinyi ameeleza kuwa, miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni vitendo vya rushwa, uzembe, kukosa uwajibikaji, kutofuata sheria na kukiukwa kwa maadili hivyo, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itakabiliana ipasavyo na vitendo vyote vinavyoathiri utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Rais Dkt.Hussein amerejea ahadi yake kwa wananchi mbele ya baraza hilo kwamba atapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi wala kuoneana muhali na kuwaomba Wawakilishi na wananchi wote wamuunge mkono wakati wa mapambano hayo.
“Tutashinda vita hii endapo wananchi pia watatuunga mkono. Sina shaka kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao, wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika mapambano haya. Ni matumaini yangu pia vyombo husika katika jambo hili vitatekeleza wajibu wao,”amesema Rais Mwinyi.

Katika hotuba hiyo pia, Rais Dkt.Hussein ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa Chama cha ACT Wazalendo, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Marehemu Abubakar Khamis Bakari ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Katiba na Sheria katika Serikali ya Awamu ya Saba kipindi cha kwanza.

Rais Dkt.Mwinyi ameweka wazi kuwa kiongozi yoyote atakayemteua kwa mamlaka aliyonayo kikatiba, atamuwajibisha mara moja pindi tu akibaini na kujiridhisha kuwa anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Ameongeza kuwa, uteuzi wa viongozi na watendaji katika serikali yake utazingatia uwezo wa mtu kitaaluma, uwajibikaji na uaminifu.

Ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane itasimamia kwa umakini nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma na haitakuwa na muhali kwa mtendaji yoyote ambae hatowajibika katika utekelezaji wa majukumu yake.

Ameongeza kuwa, atakayeshindwa kuwajibika aelewe kuwa atawajibishwa kwani uzembe na ukosefu wa nidhamu kazini huzorotesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwa hivyo, tabia hiyo hatoivumilia.

Amewataka viongozi wote atakaowateua katika nafasi mbalimbali wawe wabunifu na waweze kuishauri Serikali juu ya masuala yanayohusu fani na utaalamu wao huku akisisiza kwamba Serikali haitowavumilia viongozi wenye kusubiri kuambiwa kutoka kwake au Serikalini nini wafanye katika kutekeleza majukumu yao.

Akieleza kuhusu sekta ya mafuta na gesi, Rais Dkt.Mwinyi amesema kwamba, Serikali ya Awamu ya Nane itaziimarisha na kuzijengea uwezo wa kitaaluma na nguvu kazi Kampuni ya Mafuta Zanzibar (ZPDC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mafuta na Gesi (ZPRA) ili ziweze kuiongoza sekta hiyo muhimu.

Vile vile, Rais Dkt.Hussein amesema kwamba, Serikali itaendelea kushirikiana na kampuni mbalimbali zenye dhamira njema ya kuwekeza hapa nchini katika sekta hiyo.

Aidha, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane ina malengo ya kujenga bandari kubwa ya kisasa katika maeneo ya Mangapwani itakayokuwa na sehemu kadhaa za kutolea huduma zikiwemo sehemu za kuhudumia meli zitakazobeba mafuta na gesi, chelezo kwa ajili ya matengenezo ya meli, eneo la kuhudumia meli zinazobeba mizigo na makontena, bandari ya uvuvi pamoja na bandari ya meli za kitalii.

Amegusia kuwepo kwa malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kucheleweshwa mizigo yao bandarini na msongamano wa makontena katika Bandari ya Malindi, vitendo vya rushwa na kukosa uwajibikaji kwa baadhi ya watumishi wa bandarini.

Ameeleza dhamira ya Serikali ya kuimarisha bandari za Wete na Shumba Mjini na kuendelea na matayarisho ya ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi huko Mangapwani na kuiimarisha bandari ya Mkoani ili iweze kuhudumia meli kubwa kutoka nje moja kwa moja kwa lengo la kunyanyua uchumi na biashara kwa kisiwa cha Pemba.

Amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki.

“Tutahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi,”amesema Rais Mwinyi.

Aidha, amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane, itaweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ili sekta hizo ziwe na mchango mkubwa zaidi katika kukuza ajira na katika Pato la Taifa.

“Ushirikiano na umoja wetu ndio utakaotuwezesha kutekeleza miradi yenye tija ikiwemo uendelezaji wa viwanda, utaliii na uchumi wa buluu; ili kufanikisha azma hii, serikali itaweka mifumo rafiki kwa sekta binafsi kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi,”amesisitiza Dkt.Hussein.

Ameongeza kuwa, Serikali itaweka mazingira rafiki kwa Wanadiaspora kuja kuwekeza nyumbani kwa lengo la kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi yanayokusudiwa kufanywa.

Kutokana na kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii, Rais Dkt.Hussein alisema kuwa, kunampa matumaini kwamba malengo yaliyowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya kuongeza idadi ya wageni wanaoitembelea Zanzibar kutoka 538,264 mwaka 2019 hadi kufikia wageni 850,000 mwaka 2025 yatafikiwa.

Amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane itaendeleza dhamira njema ya kukuza sekta za Biashara na Viwanda hapa Zanzibar, ili kuwaletea wananchi wake maendeleo zaidi ya kiuchumi.

Ameeleza kuwa, hatokubaliana na visingizio vya aina yoyote na uzembe wa watendaji utakaozorotesha mipango ya kukuza sekta hizo na ndio maana, siku ya pili baada ya kuapishwa na kuanza kazi rasmi alitembelea Bandari ya Malindi ili kufahamu kwa kina malalamiko ya wafanyabiashara na wananchi kuhusiana na utendaji kazi na utoaji wa huduma usioridhisha unaofanywa na wafanyakazi bandari hapo.

Rais Dkt.Hussein amewaeleza viongozi na wafanyakazi wote katika bandari kuu za Unguja na Pemba pamoja na Viwanja vya ndege kwamba atakuwa akifuatilia kwa karibu utendaji wa taasisi hizo.

Ameeleza bayana kwamba hajaridhishwa na uendeshaji wa shughuli za bandari na viwanja vya ndege, katika maeneo yote, hasa utoaji wa huduma, uendeshaji, ukusanyaji na udhibiti wa mapato, kiwango cha faida kinachopelekwa Serikalini kila mwaka pamoja na mipango ya matumizi ya fedha za maendeleo

Ameeleza kuwa, atahakikisha wafanyakazi wa bandarini na viwanja vya ndege ni wale wanaopenda kazi kwa kuwatumikia umma, na sio wale wenye malengo binafsi ya kujinufaisha.

Rais Mwinyi amezitaja miongoni mwa barabara zitakazojengwa kwa Unguja ni Tunguu-Jumbi (km9.3), Jozani-Charawe-Ukongoroni-Bwejuu (km23.3), Fumba-Kisauni (km 12), Kizimbani-Kiboje (km 7.2) na Kichwele-Pangeni (km 4.8).

Nyingine amesema kuwa, ni barabara ya Umbuji-Uroa (km 6.9), Mkwajuni-Kijini (km 9.4) na Tunguu-Makunduchi (km48). Vile vile, kwa kuzingatia usumbufu wanaoupata wananchi wanaoishi vijiji vya Uzi na Ng’ambwa, Serikali itashughulikia ujenzi wa barabara na daraja kutoka Unguja ukuu hadi kisiwa cha Uzi.

Kwa upande wa Pemba, amezitaja barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni barabara ya Chake chake – Wete (km 22.1), Mkoani-Chake chake kupitia Chanjaani (km 29) na barabara ya Finya – Kicha (km 8.8) pamoja na kuzitengeneza barabara za ndani za Unguja na Pemba ili zipitike kwa urahisi wakati wote.

Sambamba na miongozo ya Ilani ya Uchaguzi, ameeleza kwamba Serikali ya Awamu ya Nane, itaweka mkazo katika kuimarisha Sekta ya Huduma za Fedha kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa shughuli za benki, mashirika ya bima na taasisi nyengine za fedha.

Amesema kuwa, Serikali itasimamia utendaji wa mashirika yake kwa lengo la kuhakikisha taasisi hizo zinatoa huduma bora zenye kuaminika kwa wateja wote.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kwamba, serikali itaimarisha mitaala ya masomo ya sayansi katika skuli, vituo na taasisi za ufundi pamoja na vyuo vikuu ili kuwaandaa vizuri vijana wetu na hatimae kuweza kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia katika sekta zote.

Ameeleza kwamba, Serikali ya Awamu ya Nane itaendeleza juhudi zilizopo za kuliimarisha zao la karafuu kwa kutoa mikopo na kuwatafutia masoko wakulima.

Kadhalika, kutokana na tatizo kubwa la uhaba wa nazi unaopelekea kupanda bei ya zao hilo kila uchao, alisema kuwa Serikali itaimarisha upandaji wa miche ya minazi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo pamoja na kuendeleza program ya kukuza zao la minazi iliyoanzishwa mwaka 2019.

Amesema kuwa, Serikali yake itaweka mkazo katika kuendeleza shughuli za ufugaji wa njia za kisasa, ili sekta hiyo iwe na tija zaidi kwa wakulima na kuongeza mchango wake katika upatikanaji wa chakula na kuimarisha pato la Taifa.

Serikali itabuni na kutekeleza mikakati madhubuti ya kukomesha wizi wa mifugo na mazao.Aliweka wazi kwamba kiwango cha usafi katika miji yetu hakiridhishi hivyo Serikali itahakikisha miji inakuwa safi wakati wote kwa ajili ya kulinda afya za wananchi na kuvutia wageni wanaokuja kututembelea.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya 8, itaweka kipaumbele katika kuziimarisha huduma za elimu, afya na maji safi na salama kwa kuzigatia umuhimu wake kwa ustawi wa maendeleo ya jamii.

Katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, amesema kuwa Serikali itaimarisha miundombinu ya elimu, ikiwemo, ujenzi wa skuli za kisasa na kuzikarabati skuli za zamani, kuzipatia skuli vifaa vya kufundishia na kusomea pamoja na madawati, kupitia upya mitaala ya elimu na kupunguza tatizo la walimu hasa wa masomo ya Sayansi.

Amesema kuwa, Serikali itaongeza bajeti ya sekta ya elimu ili iweze kugharamia vyema huduma za elimu katika ngazi zote kwa kuendeleza sera ya elimu pamoja na kuongeza fursa za mikopo ya wanafunzi wanaojiunga na masomo ya elimu ya juu.

Pamoja na hatua hizo, tutayaimarisha maslahi ya walimu ili kuwapa motisha ya kufundisha na tutaendeleza sera ya elimu bure kwa lengo la kuwaondolea wazazi mzigo wa kuchangia elimu ya watoto wao

Akiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ameeleza kuwa atahakikisha chuo hicho kinaanzisha programu mpya kutegemea mahitaji halisi ya nchi sambamba na kujenga majengo mapya, vifaa vya kisasa vya kufundishia ili kuweza kutoa elimu bora kwa wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho pamoja na kuweka mkazo katika kufanya tafiti kwenye maeneo muhimu kwa kuzingatia ajenda za maendeleo ya kiuchumi na kijamii za nchi.

Kwa upande wa Sekta ya Afya, Rais Dkt. Mwinyi amesema kwamba Serikali itandelea na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa huko Binguni Wilaya ya Kati ambayo itakuwa na huduma zote za kibingwa.
“Sambamba na juhudi hizo, tutaendelea kuimarisha miundombinu ya afya, ununuzi wa dawa na vifaa tiba, kuongeza idadi ya madaktari bingwa wa fani mbali mbali na wataalamu wengine wa afya. Tutaongeza bajeti ya kununulia dawa na vifaa vingine vya huduma za afya.

“Kwa kuzingatia kuwa maji ni uhai, Serikali ya Awamu ya 8 itamalizia kazi iliyobaki ya kuiboresha miundo mbinu ya maji na kuongeza upatikanaji wake,”amesema Rais Dkt.Mwinyi.

Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ni miongoni mwa malengo ya Serikali ya Awamu ya 8 katika kukabiliana na tatizo la umaskini wa kipato unaosababishwa na ukosefu wa ajira na kuahidi kuwa Serikali itauimarisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kuuongezea uwezo wa kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi wengi zaidi.

Kadhalika, tutawasajili wajasiriamali wote na kuwapatia vitambulisho. Pia, tutatoa mafunzo ya namna bora ya kuitumia mitaji na mikopo hiyo katika kupata vifaa na zana za kisasa na kuendesha shughuli za ujasiriamali kitaalamu zaidi, kulingana na mahitaji ya masoko ya wakati tulio nao.

Vile vile, tutawajengea wajasiriamali sehemu maalum za kufanyia biashara zao zilizojengwa vizuri, ili waondokane na usumbufu wa kuhamahama huku na kule. Pamoja na jitihada hizi, Serikali itawawekea mfumo na utaratibu bora wa kulipa kodi mara moja tu kwa mwaka na kuondosha ile kero ya utitiri wa kodi.

Amesema kwamba maendeleo, amani na utulivu ni dhana zenye maana zinazotegemeana ili uwiano mzuri upatikane baina ya amani, utulivu na maendeleo ni lazima tuhakikishe kwamba Serikali inaongozwa katika misingi ya utawala bora.

Amesema Serikali itasimamia utekelezaji wa sera na sheria ya hifadhi ya jamii kwa manufaa ya wanachama wote, wafanyakazi na wastaafu na kufungua Ofisi za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii katika mikoa ya Zanzibar ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wanachama wake.

Amesema Serikali itaziendeleza Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili ziendelee kutoa huduma bora za ulinzi na usalama kwa wananchi na kuendelea kuwajengea uwezo maofisa na wapiganaji kwa kuwapatia vifaa na mafunzo ya kisasa katika vyuo vya ndani na nje ya nchi pamoja na kuimarisha maslahi yao kwa kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu.

Alieleza kuwa Mapinduzi makubwa ya Uchumi yanayokusudiwa yatapelekea kuwa na uchumi mpya wa kisasa, ambao utaongeza fursa nyingi za ajira kwa vijana hivyo, vijana watawezeshwa kwa kupatiwa mitaji ili waweze kujiajiri wenyewe na kuondokana na tatizo la kutegemea ajira chache kutoka Serikalini.

Alisisitiza kwamba Serikali itaandaa sera nzuri za ajira kwa kuwashajiisha wawekezaji kuweka kipaumbele katika kuajiri vijana wa Zanzibar.

Vile vile, alisema kuwa huduma ya pensheni jamii kwa wazee waliofikia umri wa miaka 70 na zaidi zitatolewa na hapo baadae, Serikali itaangalia uwezekano wa kushusha umri na kuongeza kiwango cha pensheni inayotolewa sasa kwa mwezi.

Kwa upande wa wanawake na watoto, Serikali imeazimia kuwasaidia wanawake wajane ambao tayari wameshaunda rasmi jumuia yao. Wanawake hao watasaidiwa kwa kuwezeshwa kiuchumi na kusimamia haki zao ikiwemo mirathi.
Ameeleza kuwa, Serikali itaendeleza juhudi za kuwapatia wanawake na watoto haki zao zote za msingi ili waishi vizuri katika jamii na katika kulinda haki zao, itaendeleza mapambano ya vitendo vya udhalilishaji wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia.

Amesema kuwa, kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Serikali itaweka kipaumbele maalum katika kuwashirikisha watu wenye ulemavu kwenye shughuli mbali mbali za kiuchumi pamoja na kuzilinda na kuziimarisha haki zao.

Rais Dk. Mwinyi amesema kuwa, jukumu la kulinda na kudumisha amani iliyopo sio la vyombo vya ulinzi na usalama peke yake bali ni wajibu wa kila mtu kwani kuiharibu amani ni jambo jepesi na la mara moja, ila kuirudisha ni vigumu hivyo, kila mmoja awe mlinzi wa amani kwa kutambua kuwa bila ya amani hakuna maendeleo.

Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya 8 itashirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha amani na usalama wa Watanzania na mali zao pamoja na wageni wote wanaotembelea nchini vinadumishwa na kulindwa.

Amewaahidi wananchi kwamba Serikali atakayoiunda itasimamia kwa weledi na umahiri mkubwa utekelezaji wa ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni kwa ufanisi huku ikizingatia kuwa ahadi ni deni na wananchi wanamatumaini.

Dk. Hussein Mwinyi alimpongeza Spika wa Baraza hilo Zubeir Ali Maulid, Naibu Spika wa Baraza hilo Mgeni Hassan Juma pamoja na Wawakilishi wote huku akikipongeza chama chake cha CCM kwa ushindi wa asilmia 76.2 kwa nafasi ya Urais wa Zanzibatr, asilimia 92 ya Majimbo na asilimia 93.6 kwa nafasi ya Madiwani.

Mapema mara baada ya kufika katika viunga vya Baraza la Wawakilishi, Dk. Mwinyi alikagua Gwaride la Heshima lililoandaliwa kwa ajili ya hafla hiyo huko katika viwanja vya Baraza hilo la Wawakilishi, Chukwani Jijini Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news