Mfanyabiashara alivyokamatwa na magunia 15 ya bangi akiwa amevalia nguo za JWTZ

Mfanyabiashara Hussein Sadick (29) mkazi wa Kimara Temboni jijini Dar es Salaam ambaye alikuwa dereva wa gari aina ya Toyoya Land Cruiser- Prado rangi ya silver namba T 168 BWB na Teresphory Hamisi (40) mkazi wa Mgeta wilaya ya Mvomero aliyekuwa msindikizaji wamekamatwa na magunia ya viroba 15 yakiwa yamejazwa bangi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Watu hao wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro huku Sadick akiwa amevalia kofia na fulana ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakati akijua kuwa, yeye si mwanajeshi.

Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Wilbroad Mtafungwa amesema leo Novemba 11, 2020 kuwa, watu hao walikamatwa Novemba 5,mwaka huu majira ya saa 11 afajiri katika Kijiji cha Bonye barabara ya Duthumi Kata ya Bwakila chini iliyopo Wilaya ya Morogoro mkoani hapa.

Amesema,Novemba 5,mwaka huu majira ya saa 11 katika eneo hilo askari polisi wakiwa doria walipokea taarifa za watu waliokuwa wakisafirisha bangi na kufanikiwa kuwakamata Hussein Sadick (29) ambaye alikuwa dereva akiwa amevalia kofia na fulana ya JWTZ na Teresphory Hamisi (40) mkazi wa Mgeta wilaya ya Mvomero aliyekuwa msindikizaji.

“Watuhumiwa hao walikuwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser-Prado rangi ya `silver`yenye namba T 168 BWB. Baada ya kukaguliwa walikutwa wakiwa na viroba 15 vya bangi vyenye uzito wa kilo 237walivyoviweka ndani ya gari na mtuhumiwa Hussein Sadick alikutwa amevalia kofia na fulana ya JWTZ kinyume cha sheria huku kofia nyingine ikiwa imewekwa mbele ya gari,"amesema Kamanda huyo.

Sadick alipohojiwa na Jeshi la Polisi, Kamanda amesema alikiri kuwa si askari bali fulana na kofia zinamsaidia asikaguliwe na askari wa usalama barabarani.Amesema, watuhumiwa wote walihojiwa na kukiri kufanya matukio kama hayo ya kusafirisha bangi mara kadhaa na kwamba hatua za kuwafikisha mahakamani zitafuata mara upelelezi utakapokamilika huku Kamanda huyo akisema kuwa, jeshi hilo lipo macho saa 24 na hakuna mwalifu ambaye atafanikisha njama zake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news