Mtanzania anayetuhumiwa kuuza madawa ya kulevya asimulia yaliyomkuta mbele ya Mahakama ya Mafisadi

Ayubu Kiboko ambaye ni mfanyabiashara ameiomba Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (Mahakama ya Mafisadi) imuachie huru kwa sababu upekuzi uliofanywa nyumbani kwake hakukupatikana na dawa za kulevya, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mfanyabiashara huyo na mke wake, Pilly Mohammed Kiboko wanakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kuĺevya aina ya heroine zenye uzito wa gram 251.25.

Amedai hayo mbele ya Jaji Lilian Mashaka wa Mahakama hiyo wakati akitoa utetezi wake dhidi ya shtaka la uhujumu uchumi kwa kusafirisha dawa za kulevya linalomkabili yeye na mkewe.

Akiongonzwa na Wakili wake, Majura Magafu, Kiboko amedai kuwa, hakubaliani na tuhuma zinazomkabili kwani upekuzi ulipofanyika hakukupatikana kitu nyumbani kwake.

Amesema,anaiomba Mahakama hiyo tukufu imuachie huru ili aweze kuendelea na shughuli zake.

Aidha, wakati Kiboko, anaieleza Mahakama namna upekuzi ulivyofanyika nyumbani kwake Mei 23, 2018,  amedai siku hiyo majira ya saa nane au tisa usiku akiwa amelala nyumbani kwake alisikia mlango ukigongwa kwa nguvu, akamwamsha mke wake.

Amedai kuwa, baada ya kumwamsha alichukua silaha yake na kushuka chini kuwasikiliza, alipofika akawauliza wao ni akina nani, wakadai kuwa ni askari ambapo alirudi chumbani kuchukua ufunguo wa mlango.

Amesema, alipofungua mlango askari saba walimvamia na kunirudisha jikoni huku wakimpiga kabla ya kumfuata mkewe wake na kurudi naye chini yeye akiwa amefungwa pingu.

Amedai kuwa, askari hao walidai kuwa wanataka kupekua nyumba yake, lakini hakujua walikuwa wanatafuta nini, nilipowauliza wakadai wanatafuta dawa za kulevya na chohote chenye kutia shaka.

"Nikawauliza mnataka kunipekua bila mjumbe? Ndipo wakaniomba funguo ya geti wakatoka na kurudi na mjumbe anayefahamika kwa jina la Christina Macha," amedai Kiboko.

Amedai, baada ya mjumbe kufika upekuzi ulianza ambapo walianzia chumbani kwake wakiwa na askari wanne pamoja na shahidi mwingine aliyefahamika kwa jina la Raymond Kimambo ambaye ni jirani wa Kiboko.

Amedai katika upekuzi wote askari hao walikamata bastola moja, kadi nne za benki simu mbili aina ya Nokia na mafaili yenye nyaraka, pia walikamata kifuko cha nailoni angavu chenye chenga za mkaa kilichopatikana chumbani kwa msaidizi wa kazi.

Amedai baada ya upekuzi askari walijaza fomu ya ukamataji na kuorodhesha vitu vilivyokamatwa kisha wakampatia asaini na  wakampeleka Ofisi za Mamlaka ya Dawa za Kulevya (DCEA).

Akiendelea kuongozwa na Wakili Magafu, amekataa kuwa nyumbani kwake askari hawakukuta chenga chenga za unga mweupe uliokuwa katika mfuko wa nailoni angavu, vikopo viwili vyenye unga mweupe, mfuko mweusi wenye unga mweupe ndani na mfuko unaodaiwa kukutwa kwenye eneo la kutunzia viatu.

"Vitu vyote hivyo ambavyo vilitolewa mahakamani hapa kama vielelezo sikuwahi kuviona zaidi ya kuviona mahakamani na siku hiyo hakukufanyika upekuzi katika eneo la kutunzia viatu,"amedai.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka umewakilishwa na mawakili wa Serikali Salim Msemo, Constantine Kakula na Candid Nasua.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Mei 23, 2018 eneo la Tegeta Nyuki Masaiti wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam walisafirisha dawa za kuĺevya aina ya heroine gramu 251.25.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news