Namungo FC yawapiga Al Rabita 3-0, Mlandege yapigwa 5-0

Namungo FC imejisafishia njia katika raundi inayofuata ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF) baada ya kurekodi ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Al-Rabita kutoka Sudan Kusini, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Matokeo hayo ya aina yake yamepatikana leo Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Chamanzi Complex uliopo Chamanzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.

Timu hiyo ambayo ni miongoni mwa wawakilishi wa Tanzania, ambao wanashiriki mashindano ya CAF kwa sababu ya kufanya vizuri michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, baada ya matokeo ya leo wanatabiriwa huenda wakafanya maajabu makubwa mbeleni.

Mchambuzi wa masuala ya michezo katika chumba cha habari cha Diramakini amemueleza Mwandishi Diramakini kuwa, Namungo walikwenda kwenye mechi wakijua lazima watumie faida yao ya uwanja wa nyumbani na kuepuka kufungwa na walifanya hivyo, hatua ambayo imewapa matokeo mazuri.

Namungo FC katika mchezo huo wa kwanza wa Raundi ya Awali, mabao yake yamefungwa na Steven Sey dakika ya 20 na 39 na Shiza Kichuya dakika ya 64.

Hata hivyo, timu hizo zinatarajiwa kurudiana wiki ijayo nchini Sudan Kusini ambapo hii ni mara ya kwanza kwa Namungo FC kushiriki mashindano ya Kimataifa.

Wakati huo huo, wawakilishi wa Tanzania upande wa Tanzania visiwani (Zanzibar) timu ya Mlandege wameanza vibaya baada ya kupigwa mabao 5-0 na CS Cfaxien ya Tunisia

Matokeo hayo yanaiweka katika mazingira magumu timu hiyo ambayo ilikuwa wenyeji wa Watunisia ambapo mabao yake yaliwekwa kimiani na Kingsley Eduwo dakika ya 30, Hani Amamou dakika ya 41 na hat trick kutoka kwa Firas Chaouat aliyefunga dakika 56, 79 na 84 yaliyoimaliza kabisa Mlandege.

Post a Comment

0 Comments