Rais Magufuli aongeza shangwe kwa wafanyakazi nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameahidi kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wote ili yaendane na hali halisi ya maisha ya Watanzania, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Novemba 13, 2020 bungeni jijini Dodoma wakati akizindua Bunge la 12 ambalo ameahidi kushirikiana nalo kwa karibu.
“Tutaendelea kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wetu wote ili yaendane na hali halisi ya maisha ya Watanzania, kwa hiyo, watumishi wasiwe na wasiwasi,”amesema Rais Magufuli.

Kuhusu utawala bora katika miaka mitano ijayo, Rais Magufuli ameahidi kuendelea kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma pamoja na kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa, wizi, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.

Ameongeza kuwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali iliwachukulia hatua za kinidhamu watumishi 32,555 na kuiwezesha Tanzania kushika nafasi ya kwanza kati ya nchi 35 za Afrika kwa kupambana na rushwa, kwa mujibu wa Transparency International; na pia kushika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 duniani kwa matumizi mazuri ya fedha za umma kwa mujibu wa Utafiti Jukwaa la Dunia (World Economic Forum) wa mwaka 2019.

Bunge la 12 lililozinduliwa leo Novemba 13, 2020 na Rais Magufuli, limeahirishwa hadi Februari 2, 2021 saa tatu asubuhi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news