Miaka mitano ijayo wakulima Tanzania kutajirika

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema kuwa, anatarajia ndani ya miaka mitano ijayo Sekta ya Kilimo nchini iwe yenye tija kubwa na watahakikisha wanakifanya kilimo kinakuwa kibiashara zaidi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

"Mbali na hatua hizo, kwa lengo la kukuza uchumi, kupambana na umasikini, na pia kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira, tunakusudia, kwenye miaka mitano ijayo, kuweka mkazo mkubwa katika kukuza sekta zetu kuu za uchumi na uzalishaji, hususan kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, madini, biashara na utalii.

"Sekta hizi ndizo zenye kuajiri Watanzania wengi. Kwa hiyo, ni wazi, tukifanikiwa kuzikuza, uchumi wetu utakua kwa kasi na hivyo kupunguza matatizo ya umasikini na ukosefu wa ajira nchini.

"Kwa msingi huo, kwenye kilimo, tunakusudia kuongeza tija na kukifanya kilimo chetu kuwa cha kibiashara. Lengo ni kujihakikishia usalama wa chakula, upatikanaji wa malighafi za viwandani na pia kupata ziada ya kuuza nje.

"Ili kufanikisha hayo, tutahakikisha pembejeo na zana bora za kilimo, ikiwemo mbegu, mbolea, viatilifu/dawa na matrekta, vinapatikana kwa uhakika na kwa gharama nafuu. Tutaongeza pia eneo la umwagiliaji kutoka hekta 561,383 hadi hekta milioni 1.2 mwaka 2025 ili kupunguza utegemezi kwenye mvua;

Rais Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo Novemba 13, 2020 wakati akifungua Bunge la 12 na kulihutubia Taifa bungeni jijini Dodoma.

"Tutaimarisha mifumo ya upatikanaji wa mitaji kwa wakulima wadogo na wawekezaji kwa kushirikisha taasisi za fedha, ikiwemo Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo pamoja na benki nyingine.

"Tutashughulikia pia tatizo la upotevu wa mazao (yaani post harvest loss), ikiwemo kwa kukamilisha ujenzi wa vihenge na maghala maeneo mbalimabli nchini ambayo yataongeza uwezo wetu wa kuhifadhi mazao kutoka tani 190,000 za sasa hadi tani 501,000.

Takwimu zinaonesha kuwa, kila mwaka, nchi yetu inapoteza wastani wa kati ya asilimia 30 - 40 ya mavuno yake kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kukosekana kwa miundombinu ya kuhifadhi.

Zaidi ya hapo, tunakusudia kuanzisha bidhaa mbalimbali za huduma ya Bima ya Kilimo na pia kuingia makubaliano ya kibiashara na nchi walaji na wanunuzi wa mazao ili kupata soko la uhakika.

Mazao ya kimkakati tunayolenga kuyapa kipaumbele kikubwa ni pamba, korosho, chai, kahawa, tumbaku, mkonge, michikichi, cocoa, alizeti na miwa; lakini pia mazao ya chakula.

Nchi yetu kila mwaka inaagiza tani 800,000 za ngano na kwa ujumla, tunatumia wastani wa shilingi trilioni 1.3 kuagiza chakula kutoka nje.

Hii ni aibu kwa nchi kama Tanzania. Hivyo basi, ni lazima tutafute majawabu ya suala hili. Na hii ndiyo ikawe kazi ya kwanza ya Waziri wa Kilimo nitakayemteua.

Lakini, zaidi ya hapo, tutaweka mkazo mkubwa kwenye kilimo cha mazao ya bustani (matunda, mbogamboga, maua na viungo), ambacho kinakua kwa kasi kubwa nchini.

Hivi sasa nchi yetu inashika nafasi ya 20 kwa kuzalisha kwa wingi mazao hayo duniani na mauzo yetu ya nje yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 412 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 779 mwaka 2018/2019.

Hii ndiyo sababu, hatuna budi kukiendeleza kilimo cha mazao hayo. Na katika hilo, napenda kuriafu Bunge hili Tukufu kuwa, kwenye miaka mitano ijayo, tunakusudia kununua ndege moja ya mizigo ili kurahisisha uzafirishaji wa mazao ya bustani, lakini pia minofu ya samaki pamoja na nyama.

Wakulima wetu ni lazima watajirike na shughuli wanazozifanya; hivyo basi, Mawaziri wa Kilimo, Biashara, Mambo ya Nje na Mabalozi wajipange vizuri kwa hili,"amefafanua kwa kina Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news