NA FRESHA KINASA
Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) linalojihusisha na kutoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni lililopo Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly kwa kushirikiana na Ofisi ya Dawati la Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii wilayani humo, limeanza kampeni ya kutoa elimu ya madhara ya ukatili hususani ukeketaji katika shule za msingi na sekondari zipatazo 60 wilayani humo.
Askari kutoka Dawati la Jinsia Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara, Sijali Nyambuche akitoa elimu ya madhara ya ukatili katika Shule ya Msingi Remung'orori. Kampeni hiyo inaendeshwa na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania kwa kushirikiana Ofisi ya Dawati la Jinsia, Ustawi na Maendeleo ya Jamii. (Picha na Amos Lufungulo/Diramakini).
Lengo la kampeni hiyo ni kuwajengea uelewa wanafunzi juu ya madhara yatokanayo na ukeketaji wawe mabalozi wema wa kuwaelimisha wengine katika maeneno yao, ili kukabiliana na ukatili pamoja na kuwatambua wasichana walio katika hatari ya kukeketwa kusudi kuweka mazingira bora ya kuwaokoa na mila hiyo yenye madhara kabla ya kufanyiwa ukeketaji.
Miongoni mwa madhara ya ukeketaji ni pamoja na kutatisha masomo kwa watoto wa kike kwa kukeketwa ili kuwaandaa kuwaozesha kabla ya umri unaokubalika kisheria, kutokwa damu nyingi wakati wa kukeketwa, kusababisha kovu la kudumu sehemu za siri, kuathirika kisaikolojia, hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza kwa kuchangia vifaa mfano nyembe, hivyo kupitia kampeni hiyo watajengewa uwezo wa kuwa tayari kuepukana na vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha haki za binadamu na sheria za nchi.
Kampeni hiyo ilizinduliwa Novemba 3, 2020 wilayani humo ikitajwa kuwa na umuhimu mkubwa katika kuwanusuru watoto wa kike katika kuelekea mwezi Desemba ambao hutumiwa na baadhi ya wazazi na walezi wa koo za Kikurya zikiwemo koo za Wailegi, Wakenye, Walinchoka, Wakila na Wanyabasi kuwakeketa mabinti zao wakiwa likizo kwa ajili ya maandalizi ya kuwaozesha ili kupata mahari, licha ya Serikali na asasi za kiraia kuendelea kukemea vikali mila hiyo yenye athari kwao na kandamizi.
Akizungumzia juu ya kampeni hiyo ambayo itazifikia shule 60 wilayani Serengeti, Mratibu wa Elimu ya Ukatili wa Kijinsia katika Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Emmanuel Good Luck Maingu amesema kuwa, itawezesha kuwapa elimu na ufahamu mpana wa kutambua madhara ya ukeketaji sanjari na kuwatambua wasichana ambao wapo katika hatari kubwa ya kukeketwa kuwawekea mikakati thabiti ya kuwanusuru na ukeketaji kabla hawajafanyiwa vitendo hivyo.
Mratibu wa Elimu ya Ukatili kutoka Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Emmanuely Good luck akitoa ufafanuzi kwa mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Msingi walizozifikia kutoa elimu ya madhara ya ukatili. Shirika hilo litazifikia shule 60 za msingi na sekondari kutoa elimu hiyo. (Diramakini).
"Sisi kama Shirika la HGWT tumekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii juu ya suala zima la ukatili hususani ukeketaji wakati wote, na inapofikia mwezi Desemba nguvu kubwa hutumiwa kuelimisha jamii ikiwemo kutoa elimu shuleni, barabarani, kuonesha sinema, kutumia vyombo vya habari, na kuwafikia wazee wa kimila na kuwabaini Ngariba walioko kwenye mipango ya kukeketa ili kuwapa elimu waachane na vitendo hivyo vya kikatili, kwa mwaka huu tumejipanga vyema kuwaokoa wasichana wote watakaokuwa kwenye hatari ya kukeketwa,"amesema Emmanuely.
Aidha, Emmanuely amewaasa wazazi na walezi wote wawalinde watoto wao kama abavyo Sheria ya Mtoto inaelekeza na kutowafanyia ukeketaji na aina yoyote ile ya ukeketaji kwa tamaa zao ili wajipatie mali katika kipindi hiki cha kuelekeza Desemba, ambapo amesisitiza kuwa Serikali kwa kushirikiana na shirika hilo watahakikisha kwamba yeyote atakayebainika anachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mpaka sasa shule zilizofikiwa ni pamoja na Shule ya Sekondari Ling'wani, Shule ya Sekondari Nyansurura, Shule ya Sekondari Melenga 'A' na 'B' Shule ya Msingi Nyansurura, Shule ya Msingi Moningori, Shule ya Msingi Magange, Shule Msingi Remng'orori na zoezi la kuzifikia shule zingine linaendelea.
Mwalimu Rose Mgina kutoka Shule ya Sekondari Ring'wani ambaye ni Mwalimu wa Malezi shuleni hapo, amelipongeza Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania kwa kupeleka kampeni hiyo shuleni amesema elimu hiyo itakuwa chachu ya kupunguza ndoa za utotoni, vitendo vya ukeketaji, na kuwafanya watoto wa kike kujitambua na kusoma kwa bidii na kutoshawishika ili wafikie ndoto zao kwa siku za usoni.
Naye Jamila Jackson Mwita mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Nyansurura wilayani Serengeti amesema elimu hiyo imekuja kwa muda mwafaka kwani imewajengea uwezo wanafunzi wa kike namna bora ya kuchukua hatua za kuripoti vitendo hivyo ikiwemo Ofisi za Serikali za mitaa, Polisi, Dawati la Jinsia, wadau mbalimbali na akaomba elimu hiyo ifikishwe kwenye kila kundi ili kutokomeza vitendo hivyo.

