Wanafunzi wapya 5,168 mwaka wa kwanza wapangiwa mikopo Bilioni 19.9/-

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya wanafunzi 5168 wa awamu ya pili wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 19.9, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 17, 2020 na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma. Amesema kuwa, hadi leo jumla ya wanafunzi 52,473 wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mkopo yenye thamani ya shilingi bilioni 170.02.

Badru amesema Novemba 11, mwaka huu HESLB ilitangaza orodha ya Awamu ya Kwanza waliopangwa mikopo iliyokuwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 47,305 ambao walipangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi 150.03 bilioni.

“Wanachotakiwa kufanya kwa sasa ni kutembelea katika akaunti zao za SIPA walizotumia kuomba mkopo na watapata taarifa za kina kuhusu mkopo,”amesema Abdul-Razaq Badru leo jijini Dar es Salaam.

Waliokosea sasa ruksa kurekebisha

Kuhusu wanafunzi waombaji ambao maombi yao yalikua na upungufu, Badru amesema HESLB imetoa muda wa siku tano kuanzia kesho (Jumatano, Novemba 18, 2020) kurekebisha taarifa zao na kuzituma kwa njia ya mtandao.

“Tuna wanafunzi wachache ambao maombi yao yana upungufu ambao kuanzia kesho wataweza kuingia katika akaunti zao za SIPA walizotumia kuomba mkopo na kurekebisha kwa kuweka nyaraka sahihi na tutazifanyia uchambuzi na wenye sifa watapangiwa mikopo mapema iwezekanavyo,” amesema Badru.

Katika mwaka 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi 464 Bilioni kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu 145,000 wakiwemo wanafunzi 54,000 wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 91,000 wanaoendelea na masomo.

Post a Comment

0 Comments