WAZIRI MKUU AKAGUA VYANZO VYA MAJI DODOMA, AAGIZA MRADI WA FARKWA UANZE HARAKA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Maji, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini Dodoma (DUWASA) na Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma wahakikishe mradi wa bwawa la maji Farkwa uliopo kijiji cha Mombose, wilayani Chemba, mkoani Dodoma unaanza mapema.
Akizungumza wakati alipotembelea eneo la mradi huo leo Novemba 21, 2020, Waziri Mkuu amesema idadi ya watu katika mkoa wa Dodoma imekuwa ikiongezeka kwa kasi hivyo ni lazima kuwepo na chanzo cha maji cha uhakika.

“Mhe. Rais Dkt John Magufuli ameutamka sana mradi huu wa maji. Hata Ilani ya Uchaguzi imeutaja mradi huu ambao umetengewa zaidi ya sh. bilioni 900 na utakuwa na uwezo wa kutoa mita za ujazo 128,000 kwa siku. Rais wetu ana nia njema ya kupeleka huduma hii ya maji kote nchini, tuanze mradi huu mapema,” amesisitiza.

Akizungumzia kuhusu fidia kwa wakazi watakaoguswa na mradi huo, Waziri Mkuu amesema kuwa waliolipwa fidia ni asilimia 91 na kwamba kila anayedai atalipwa kwa sababu fedha zipo na hakuna hata mtu mmoja atakayedhulumiwa.

“Fedha kwa ajili ya fidia ipo, hivyo wananchi wote walioathiriwa na mradi huu watalipwa, mpaka sasa jumla ya shilingi bilioni 7.6 zimeshalipwa na wale waliobaki watalipwa,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amewahakikishia wakazi wa eneo hilo kuwa Serikali itasimamia ipasavyo ujenzi wa miundombinu ya huduma za kijamii ikiwemo shule na huduma za afya katika eneo lililotengwa kabla ya kuwahamisha na takribani sh. milioni 600 zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ahakikishe wananchi wa eneo hilo wanapewa kipaumbele katika ajira pindi mradi huo utakapoanza kutekelezwa.

“Ajira za ujenzi wa ukuta na kazi nyingine zifanywe na watu wa hapa, kwani shughuli kama kubeba zege inahitaji mtu awe na digrii? alihoji na kuongeza: “Mkandarasi aambiwe kuwa ajira hizo ni kwa wakazi wa eneo hili kwanza.”

Akitoa maelezo mbele ya Waziri Mkuu kuhusu faida nyingine za mradi huo pindi utakapokamilika, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Sanga amesema bwawa hilo litawezesha wananchi kupata maji ya kutosha kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.

Naye, Mbunge wa Chemba, Bw. Mohamed Moni ameishukuru Serikali kwa kuamua kuutekeleza mradi huo ambao utakuwa ni moja ya miradi mikubwa ya maji nchini kwani kwa kiasi kikubwa utasaidia kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Dodoma.

Mapema, Waziri Mkuu alitembelea chanzo cha maji cha Mzakwe kilichopo nje kidogo ya mji wa Dodoma na kuagiza mkandarasi ambaye anapaswa kuchimba kisima cha kuzalisha maji lita 430,000 kwa saa, aanze haraka kazi hiyo ili kuongeza kiwango cha maji yanayoenda mjini.

Post a Comment

0 Comments