Naibu Waziri Waitara aagiza uchunguzi matumizi ya Bilioni 1.9/- Geita

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwita Waitara ameagiza uongozi wa Mkoa wa Geita kuchunguza mkandarasi aliyejenga Dampo la taka ngumu mjini Geita pamoja na msimamizi wake ili kujiridhisha na matumizi ya fedha sh.Bilioni 1.9,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwita Waitara akikagua Dampo la kisasa eneo la Usindakwe mjini Geita lilojengwa kwa sh.Bilioni 1.9 bila kukamilika. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

Ametoa agizo hilo baada ya kukagua ujenzi wa dampo hilo ambalo lilianza kujengwa mwaka 2015 kutelekezwa bila kukamilika hadi sasa, lakini likionekana kuwa mapungufu mengi.

Naibu Waziri Waitara amesema, fedha zilizotumika katika mradi huo ni kubwa lakini thamani ya fedha haipo hivyo kuna dalili za upotovu wa mamilioni ya fedha.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwita Waitara akizungumza na mmiliki na wafanyakazi wa kiwanda cha kuyeyusha Dhahabu cha Mass Elution Geita. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Ameagiza uchunguzi hufanyike ili kila aliyehusika katika mradi huo ambao haujakabidhiwa ,ajulikane na hatua zichukulie kwa kila mtu kulingana na uhusika wake.

Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji, Aloyce Mutayuga amemueleza Naibu Waziri Waitara kuwa mradi huo ulijengwa kwa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na msimamizi mkuu wa mradi huo alikuwa ni Mamlaka vya Maji Safi na Mazingira ya Jiji la Mwanza (MWAUWASA).

Mkandarasi wa ujenzi alikuwa ni kampuni ya Jasco ambaye aliishia njiani na kutelekeza mtambo wake eneo la mradi na baadae akaingia mkandarasi mwingine ambaye hajakabidhi pia mradi huo.

Mutayuga amesema kuwa, katika mradi huo kulikuwa na visima vitatu lakini mkandarasi alijenga kisima kimoja tu na visima vingine havionekani.
Moja ya gari linalotumika kubeba taka maji katika mji wa Geita. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

Afisa mazingira ameongeza kuwa, dampo hilo kwa sasa lina mapungufu mengi hivyo inahitajika zaidi ya sh. milioni 400 kwa ajili ya kulifanyia matengenezo ili liweze kutumika.

Amesema,kwa sasa Halmashauri ya Mji wa Geita imelazimika kutoendelea kutumia dampo hilo badala yake inatumia mashimo ya muda ambayo yalichimbwa na wakandarasi waliokuwa wanachukua changarawe kujenga barabara.

Post a Comment

0 Comments