TAKUKURU yarejesha TANESCO vifaa vya umeme vya Bilioni 1.2/-

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imelirejeshea Shirika la Umeme (TANESCO) vifaa ghafi vya umeme vya zaidi ya shilingi Bilioni 1.2, anaripoti Mwandishi Diramakini. 
Hayo yabebainishwa leo Desemba 29, 2020 na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, John Julius Mbungo.

“Awali ya yote, ningependa nianze na nukuu mbalimbali za Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo amekuwa akiiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Agosti 28, 2017 alipotembelea ofisi za TAKUKURU Makao Makuu, Mhe. Rais alisema maneno yafuatayo. Ninanukuu

“…Ndugu zangu mna wajibu mkubwa sana. Kazi yenu ni kusacrifice kwa ajili ya watu wengine. Hakuna mtu mwingine au taasisi yoyote ambayo inaweza kupambana na rushwa ambao wako front kama ninyi. Ninyi mkicheza na huu mchezo, tutaleteleza taifa letu kuangamia.

Kila mahali kutakuwa na rushwa. Sasa kazi hii mmeshaianza, ninawaomba mkaiendeleze.”

1. Septemba 12, 2018 akimwapisha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU - C.P Diwani Athumani, Mhe. Rais alisema: Ninanukuu

“ Wananchi hasa vijijini wanateseka sana. Ukitembea huko unasikia vilio vya dhuluma vinavyofanyika. Chombo hiki kinaweza kikawa mkombozi mkubwa wa dhuluma hizo zinazofanyika miongoni mwa watu.”

2. Lakini pia naomba kunukuu maagizo mengine aliyoyatoa Julai 22, 2020 akiongea na wananchi kwenye hafla ya uzinduzi wa majengo mapya saba ya TAKUKURU ngazi ya Wilaya – pale Chamwino jijini Dodoma. Alisema:

Rushwa ni mbaya mno… mimi nikizunguka kwenye wilaya, mikoa …kila mahali ninapozunguka unaiona hapa kuna rushwa.  Unakuta Mwanamama analia amedhulumiwa labda hajapata urithi wake…na unakuta chombo cha TAKUKURU KIPO pale wilayani!

· Unakuta wananchi wamedhulumiwa mazao yao…Chombo cha TAKUKURU KIPO!

· Unakuta kwenye Ardhi watu wanalia wamedhulumiwa mashamba yao…Chombo cha TAKUKURU KIPO!

· Unakuta tajiri mmoja tu anawanyanyasa masikini …TAKUKURU MPO!

Na kero hizi ndogondogo kwa wananchi masikini zinauma mno… zinauma mno!

Kutokana na maagizo haya, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa - TAKUKURU, pamoja na kuendelea na majukumu yetu ya kuongoza mapambano dhidi ya rushwa kwa mamlaka tuliyopewa na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11 ya Mwaka 2007, tumejikita katika OPERESHENI MAALUM nchi nzima, za utatuzi wa kero hizi na kwa kiwango kikubwa tumefanikiwa kurejesha fedha na mali za wananchi wanyonge ambazo zilikuwa zimedhulumiwa na wajanja wachache wasio na uzalendo na nia njema kwa taifa lao.

Mali za Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania – TANESCO ambazo mnaziona hapa mbele yenu, zilikuwa zimepotea kwa mbinu mbalimbali ambazo zimefanywa na baadhi ya wananchi wajanja.

Leo tunashuhudia mali hizo zikiwa zimerejeshwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU ambayo imefanya kazi kubwa tatu zifuatazo:

· Kwanza ni kutambua na kuhakiki vifaa ghafi vya umeme vilivyotakiwa kurejeshwa kwa mujibu wa mkataba.

·Pili ni kuwatambua wakandarasi wa Miradi ya REA II ambao Mikataba waliyotekeleza iliwataka kuwasilisha Vifaa ghafi TANESCO baada ya kuwa wamepewa NOTISI ya kufanya hivyo tangu mwaka 2017. Na

· Tatu ni kwa kushirikiana na TANESCO, REA pamoja na Wakandarasi, kuhakikisha kwamba vifaa ghafi vya umeme vinawasilishwa TANESCO vikiwa kwenye ubora na utimilifu.

Tukio hili ni moja ya kielelezo ambacho kinathibitisha utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli – Mkuu wa Nchi na Jemedari wa mapambano dhidi ya Rushwa nchini ambaye amekuwa akiyatoa SI kwa TAKUKURU peke yake bali kwa wananchi wote wanaopenda maendeleo ya Taifa lao.

Hivyo nachukua fursa hii kuwashukuru sana TANESCO, REA, Wakandarasi pamoja na wananchi waliojitokeza kutoa taarifa na ushirikiano kwa TAKUKURU hadi kufanikiwa kurejesha mali hizi kama mnavyoziona hapa mbele yenu ambazo tutazikabidhi katika mikono salama.

“Leo tunarejesha TANESCO vifaa ghafi vyenye jumla ya thamani ya shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia Mbili Kumi na Sita, Laki Nane na Arobaini, Mia Tatu na Sitini - 1,216,840,360 na tutamkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme TANESCO Dkt Tito Mwinuka pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa WAKALA wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Bw. Amos William Maganga.

Makabidhiano haya ni mwendelezo wa OPERESHENI ya kufuatilia uokoaji wa mali za Serikali na kuhakikisha kwamba Miradi ya Maendeleo ya Nishati Umeme iliyopangwa na Serikali inawafikia walengwa wote na kwa wakati bila kugubikwa na vitendo vya rushwa au ubadhirifu.

Kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007, TAKUKURU kupitia Kurugenzi yetu ya UZUIAJI RUSHWA tunalo jukumu la kufuatilia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo nchini ili kujiridhisha iwapo miradi hiyo ilitekelezwa kwa mujibu wa mikataba iliyoingiwa kati ya Wakala wa Nishati vijijini na Wakandarasi waliopata zabuni za kutekeleza miradi hiyo na iwapo THAMANI YA FEDHA ILIYOTUMIKA INAENDANA NA UBORA WA UTEKELEZAJI WA MIRADI HIYO.

Kutokana na sababu hiyo, Miezi mitano iliyopita - Julai 2020, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilianzisha OPERESHENI kwenye Miradi ya Usambazaji wa Umeme vijijini - Awamu ya pili (REA II) mradi ambao uko chini ya Wakala wa Usambazaji wa Nishati Vijijini (REA). Mpaka sasa operesheni hii imeshafanyika katika mikoa mitano ya Geita, Iringa, Pwani, Morogoro na Kagera.

Kwa mujibu wa mikataba kila mkandarasi, ana wajibu wa kurejesha TANESCO vifaa ghafi vya umeme vinavyobaki baada ya mkataba kukamilika. Vifaa hivi ni vile ambavyo ni Mandatory Spare Parts and Materials remained for uncovered scopes.

YALIYOBAINIKA:

· Katika mikoa mitano iliyofanyiwa kazi - wakandarasi hawakukabidhi TANESCO vifaa ghafi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 4.3 (4,355,790,604.95/=) licha ya kukumbushwa mara kwa mara kufanya urejeshaji huo na kupewa NOTISI ya kufanya hivyo mwaka 2017.

Vifaa ghafi tutakavyokabidhi ni kutokana na Operesheni ya uchunguzi wa Miradi ya REA II iliyofanyika katika mkoa wa Iringa. Vifaa ghafi hivyo ni pamoja na:

(i) Transfoma 34 zenye ukubwa tofauti,

(ii) Mita za LUKU 1,458 na vifaa vyake,

(iii) Nyaya zenye urefu wa km 70.8 pamoja na

(iv) Vifaa 30 vya umeme (Ready boards) vya aina tofauti tofauti kama mnavyoviona mbele yenu

Vyote vikiwa na thamani ya shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia Mbili Kumi na Sita, Laki Nane na Arobaini, Mia Tatu na Sitini - 1,216,840,360.

Natumia hadhira hii kutoa RAI kwa Wakandarasi 16 nitakaowataja, ambao walipelekewa NOTISI na REA tangu mwaka 2017 lakini bado hawajawasilisha vifaa ghafi hivyo katika ofisi za TANESCO kama NOTISI walizopokea zinavyowataka kufanya. Ninawaagiza kwamba wahakikishe WAMEREJESHA VIFAA GHAFI hivyo ndani ya siku 14 kuanzia leo. Wakandarasi hao ni wafuatao:

S/N

MKANDARASI

ENEO LA MRADI 

01.

Shandong Taikai Power Engineering Co. Ltd

Kasulu, Kibondo, Kigoma, Mbinga, Ngara, Tunduru

02.

Angelique International Limited

Arusha

03.

Derm Electrics (T) Ltd

Mara, Dodoma

04.

Lucky Exports (Energy Division)

Katavi

05.

Spencon Services Limited

Singida, Kilimanjaro

06.

LTL Projects (PVT) Limited

Shinyanga, Ruvuma

07.

Namis Corporate Ltd

Mtwara

08.

O K Electrical & Electronics Services Ltd

Lindi-Kilwa &Lindi Rural

09.

China Henan International Co corporation Group Co. LTD na China National Electrical Wire & Cable Imp/Expo Corporation

 

Tabora, Mwanza

10.

States Grid Electrical & Technical Works Ltd; M.F  Electrical Engineering Ltd, Power General &TD Limited, DIEYNEM Co Limited na GESAP Electrical Supplies Co. Ltd

Mbeya-Ileje, Kyela & Mbeya Rural

11.

CCC International Engineering Nigeria

Manyara

12.

Sinotec Co. Ltd

Rukwa-Nkasi Sumbawanga Rural, Mbeya-Mbozi, Mbeya-Chunya & Mbeya Rural

13.

STEG International Services

Tanga-Handeni, Korogwe &Lushoto

14.

Nakuroi Investments & DERM Electric (T) Limited

Rukwa-Kalambo

15.

Urban and Rural Engineering Services Limited

Kagera

16.

MBH Power Limited

Pwani, Morogoro na Lindi

Wakandarasi hawa kwa pamoja wanatakiwa kurejesha vifaa ghafi vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 10.

TAKUKURU inaahidi kuendelea kutekeleza majukumu yake ya uokoaji wa Mali za Umma na Binafsi mbali na usimamiaji wa mapambano dhidi ya Rushwa nchini ili kuokoa mali zinazopotelea mikononi mwa wananchi wachache wasio wazalendo.

“Mwisho, naomba nimsimamishe Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ugavi wa Umeme TANESCO ili nifanye naye ishara ya ya kupokea vifaa ghafi vilivyookolewa na TAKUKURU ikishirikiana na wananchi wazalendo,”ameongeza Mkurugenzi huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news