NECTA yatangaza rasmi ratiba ya mitihani ya Kidato cha Sita 2026

NA DIRAMAKINI

BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia limetangaza rasmi ratiba ya Mitihani ya Kidato cha Sita (ACSEE) kwa mwaka 2026, itakayofanyika mwezi Mei,2026 kote nchini.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa,mitihani itaanza Mei 4,2026 na kuhitimishwa Mei 25,2026 ikihusisha masomo ya nadharia na vitendo kwa watahiniwa wa michepuo mbalimbali.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, mtihani utaendeshwa kwa vipindi viwili kwa siku, kipindi cha asubuhi (saa 2:00 hadi saa 5:00) na kipindi cha mchana (saa 8:00 hadi saa 11:00).

Mtihani utaanza rasmi Jumatatu, Mei 4, 2026 kwa somo la General Studies katika kipindi cha asubuhi, huku masomo mengine kama Historia, Baiolojia, Uhasibu na Lugha ya Kichina yakifanyika katika kipindi cha mchana siku hiyo.

Siku zinazofuata zitahusisha masomo mbalimbali ya lazima na ya mchepuo, yakiwemo Kiswahili, Fizikia, Kemia, Jiografia, Uchumi, Biashara, Kilimo, Lishe na Sayansi ya Kompyuta.

Aidha, masomo ya lugha kama Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu na Kichina pia yamepangiwa tarehe maalum katika ratiba hiyo.

Kwa upande wa mitihani ya vitendo (practical), ratiba inaonesha kuwa itaanza tarehe 11 Mei 2026 kwa baadhi ya masomo kama Kilimo, Baiolojia na Hisabati.

Mitihani hiyo itaendelea hadi tarehe 25 Mei 2026, ikihusisha masomo ya sayansi kama Fizikia, Kemia na Baiolojia katika makundi mbalimbali (3A, 3B na 3C), pamoja na Sayansi ya Kompyuta.

Watahiniwa wanapaswa kuzingatia kwa makini maelekezo yote yaliyotolewa, hususan kuhusu muda na siku za mitihani kama zilivyoainishwa kwenye ratiba.

Aidha, imesisitizwa kuwa iwapo kutatokea mkanganyiko wowote, muda na taarifa zilizo kwenye karatasi ya mtihani ndizo zitakazochukuliwa kuwa sahihi.

Pia, imetolewa tahadhari kuwa mitihani itaendelea kama ilivyopangwa hata kama itagongana na siku za mapumziko ya kitaifa.

Kutangazwa kwa ratiba hii kunatoa mwongozo muhimu kwa wanafunzi, walimu na wadau wa elimu nchini katika kujiandaa ipasavyo kwa mitihani hiyo muhimu inayohitimisha elimu ya sekondari ya juu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here