Ujenzi Chuo cha VETA Ludewa kuanza mwezi ujao

Kufuatia kusimama kwa ujenzi wa Chuo cha Ufundi (VETA) kilichopo katika kata ya Lugarawa kijiji cha Shaurimoyo wilayani Ludewa kwa takribani miaka mitatu hatimae ujenzi huo kuanza tena Januari 2021 baada ya upatikanaji wa fedha za kuendeleza ujenzi huo kufikia hatua za mwisho,anaripoti Damian Kunambi (Diramakini) Njombe.
Akitoa ufafanuzi juu ya ujenzi huo meneja mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA, Mhandisi Benitho Mgava kutoka VETA Kanda ya Iringa mbele ya mkuu wa mkoa wa Njombe, Marwa Rubirya pamoja na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema kuwa awali ujenzi ulipangwa kukamilika kwa miezi nane na kugharimu sh.Bilioni 9 mpaka kuisha ujenzi huo.

Amesema, zoezi hilo lilishindwa kukamilika kwa kuwa mkandarasi aliyekabidhiwa kazi hiyo alitumia fedha hizo kusawazisha eneo la ujenzi badala ya kujenga.

Ameongeza kuwa, kwa juhudi za uongozi wa VETA walijaribu kuona namna ya kupata pesa ya kuendeleza ujenzi huo ambapo ilifanikiwa kutenga bilioni 2 ili kusogeza ujenzi, lakini kabla fedha hizo hazijatumika Wizara ya Elimu ikamteua Arusha Technical College kuwa mshauri na kusimamia miradi yote iliyokuwa chini ya ADB.
"Mpaka sasa eneo hili tayari limeshafanyiwa michoro na kukabidhiwa kwa Katibu wa Wizara ya Elimu ambapo wameridhia na kukubali kutoa fedha kwa njia ya force account badala ya kupitia kwa mkandarasi na mpaka kuisha kwake utagharimu shilingi bilioni 6,"amesema Mgava.

Aidha, kwa upande wa mkuu wa mkoa wa Njombe, Marwa Rubirya amemtaka kutoa ahadi hiyo ya muda wa kuanza ujenzi kwa maandishi kwani kumekuwa na maelezo mengi ambayo hakuna utekelezaji wake.

Amesema , wananchi walitoa maeneo hayo wakiamini chuo kitajengwa kama ilivyopangwa, lakini wanavyoona utekelezaji hakuna imefikia hatua wanadai maeneo yao ambayo waliyatoa kwa ujenzi wa chuo hicho ili waendelee na shughuli zao.
"Wananchi waliyatoa maeneo Haya kwa moyo wote wakitumaini watoto wao watapata elimu ya ufundi hapa sasa mnapochelewesha mnapelekea kupoteza imani kutoka kwa wananchi hawa,"amesema. Rubirya.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo , Joseph Kamonga amesema chuo hicho kikikamilika kitakuwa msaada mkubwa kwa vijana kwani watapata ajira katika ujenzi na kwa wale watakaosoma ufundi watakuwa watendaji wazuri pindi utakapoanza mradi wa Liganga na Mchuchuma.

"Wazawa wanatakiwa kuwa vipaumbele katika kupata ajira katika miradi iliyo ndani ya wilaya sasa watapataje ajira hizi wasipokuwa na ujuzi? Kwa hiyo chuo hiki kikiwajengea vijana wetu ujuzi itasaidia vijana kupata ajira katika rassilimali zilizo katika wilaya yao,"amesema Kamonga.

Amesema, atakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa kuwa ana historia kubwa na eneo hilo kwani yeye ndiye aliyetoa hati ya eneo hilo wakati alipokuwa afisa ardhi wa wilaya hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news