Barabara, bandari zarejesha tumaini jipya la uchumi Ukanda wa Magharibi

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kutatua kero na malalamiko ya wananchi kwa wakati katika miradi na huduma wanazozitoa, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Akizungumza mkoani Rukwa mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu wa kilomita 112 na upanuzi wa bandari ya Kasanga, Naibu Waziri Kasekenya ameridhishwa na utekelezaji wa barabara hiyo na kumtaka mkandarasi China Railway 15 Group kukamilisha sehemu iliyobaki yenye urefu wa mita 150 katika kipindi cha siku 45. 

Aidha, amemtaka Mkandarasi Shanxi Construction Engineering anayetekeleza mradi wa upanuzi wa bandari ya Kasanga kutathmini kazi anayoifanya kama iko katika viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa mkataba kabla ya kuchukuliwa hatua.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (aliyevaa miwani) akikagua gati katika bandari ya Kabwe ambalo ujenzi wake umekamilika Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.

“Hakikisheni kazi za ujenzi wa barabara na upanuzi wa bandari zinakamilika katika kipindi kifupi kuanzia sasa, kwa kuwa muda uliopangwa kimkataba umemalizika,”amesema Naibu Waziri Kasekenya. 

Naibu Waziri huyo amemuagiza Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Meneja wa Bandari ya Kigoma kufika eneo la mradi ndani ya wiki moja kwa ajili ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kutoa ripoti.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga Port yenye urefu wa kilomita 112 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami mkoani Rukwa. 

Kukamilika kwa barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port na upanuzi wa bandari ya Kasanga ni mkakati wa Serikali wa kuhuisha uchumi katika ukanda wa Magharibi wenye mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi na hivyo kuchochea biashara kati ya Tanzania na nchi za Zambia, Burundi na Congo DRC.
Muonekano wa gati katika bandari ya Kabwe ambayo ujenzi wake umekamilika iliyopo wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga Port yenye urefu wa kilometa 112 na upanuzi wa bandari ya Kasanga, mkoani Rukwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Rukwa mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga Port yenye urefu wa kilometa 112, mkoani Rukwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Karolius Misungwi, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kuchochea shughuli za kibiashara za Wilaya na kuiomba Serikali kuendelea kuibua fursa za kiuchumi kwenye ukanda huo wenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara. 

Naibu Waziri Kasekenya yupo katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa miundombinu katika Ukanda wa mikoa ya Magharibi ambapo pamoja na mambo mengine anakutana na watumishi wa Wizara ili kubadilishana uzoefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news