Mkoa waridhishwa kasi ya upandaji miti Jiji la Dodoma

Uongozi wa Mkoa wa Dodoma umeridhishwa na mwendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya kijanisha Dodoma inayofanywa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo kwa lengo la kulinda na kutunza mazingira, anaripoti Dennis Gondwe (Dodoma).
Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Jiji la Dodoma, mwalimu Joseph Mabeyo akipanda mti wake wa 17 katika zoezi la upandaji miti lililofanyika katika shule ya msingi Ipala jijini Dodoma likiwa ni utekelezaji wa kampeni ya kijanisha Dodoma. (Picha na Dennis Gondwe).

Kauli hiyo imetolewa na mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Natalius Linuma alipokuwa akitoa shukrani kwa washiriki wa zoezi la upandaji miti kwa timu “B” lililofanyika katika Shule ya Msingi Ipala jijini hapa.

Linuma ambaye pia ni Katibu Tawala msaidizi, anayesimamia menejimenti ya Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amesema kuwa, mheshimiwa mkuu wa mkoa aliagiza kila mtumishi apande miti angalau 10 kila siku ya Jumamosi. 

Aidha, ameipongeza halmashauri ya jiji hilo kwa muitikio huo ambao ni utekelezaji wa agizo la mheshimiwa Mkuu wa Mkoa. 

“Sasa wito wangu kwenu ni kuitunza miti hii na kuhakikisha inakuwa. Ili kampeni hii itoe mafanikio makubwa haraka lazima tuongeze kasi ya upandaji miti na kuitunza,"amesema Linuma.

Mwakilishi huyo, ameupongeza uongozi wa kata ya Ipala kwa kuwa mstari wa mbele katika upandaji miti. 
Mthibiti Ubora wa Elimu Wilaya ya Dodoma Mjini, Mwalimu Lucy Mbolu akishiriki kupanda mti wake wa 11 wa mpapai katika Shule ya Msingi Ipala iliyopo jijini Dodoma katika utekelezaji wa kampeni ya Kijanisha Dodoma. (Picha na Dennis Gondwe).

“Hapa Kata ya Ipala mmejitahidi sana kupanda miti, naona idadi ya miti iliyopandwa ni kubwa na inaendelea vizuri. Natamani kata zote ziige mfano wa kata hii,"amesema Linuma.

Awali, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Joseph Mabeyo amesema kuwa jumla ya miti 1,500 ilipandwa katika zoezi la upandaji miti katika Kata ya Ipala. 

Mwalimu Mabeyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma amesema kuwa, katika zoezi hilo, limehusisha upandaji wa miti ya matunda. 

“Wote tumeshuhudia katika zoezi hili tumepanda pamoja na miti mingine, miti ya matunda. Lengo ni kuboresha lishe ya wanafunzi. Wanafunzi wanapokuwa na afya njema inawawezesha kupata maarifa na ujuzi kwa uhakika. Hivyo, lishe bora itawafanya wanafunzi kuwa huru dhidi ya magonjwa na kutumia muda wao vizuri katika masomo,”amesema Mwalimu Mabeyo.

"Matunda pia ni sehemu ya chakula, hivyo yatakapokuwa na kukomaa yatawavutia wanafunzi kuyatumia kama matunda na chakula. Matumaini ya halmashauri ni kwamba, matunda haya yatasaidia kuondoa utoro kwa wanafunzi,"ameongeza.

Nae mratibu wa kampeni ya kijanisha Dodoma katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro amesema kuwa halmashauri ilizigawanya timu mbili za watumishi wa halmashauri ili kuharakisha zoezi la upandaji miti. 

Amesema kuwa, timu “A” iliongozwa na Mkurugenzi wa Jiji na timu “B” iliongozwa na Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi.

Zoezi la upandaji miti katika shule ya msingi Ipala iliyopo Kata ya Ipala lilishirikisha watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Jiji, Mthibiti ubora wa wilaya, Tume ya Utumishi wa Walimu, Wakala wa Misitu Tanzania, Kata ya Ipala na wananchi kwa ujumla. 

Post a Comment

0 Comments