Bodi ya Kitaaluma ya Ununuzi na Ugavi (PSPTB), inayofanya kazi chini ya Wizara ya Fedha, imetoa onyo kali kwa watahiniwa wote wa fani ya Ununuzi na Ugavi kujiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa kanuni na taratibu za mitihani, ikisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watakaobainika kufanya udanganyifu.
Onyo hilo limetolewa Januari 30, 2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Bw. Godfred Mbanyi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu udahili na matokeo ya mitihani ya 32 ya bodi hiyo.
Bw. Mbanyi amesema adhabu kwa mujibu wa kanuni ni pamoja na kufutiwa matokeo ya mitihani yote, kusimamishwa kushiriki mitihani kwa mikao mitatu mfululizo, kutozwa faini au hata kifungo cha jela kulingana na uzito wa kosa.
Katika mitihani hiyo, jumla ya watahiniwa 1,291 walidahiliwa, ambapo watahiniwa 1,223 walifanya mitihani huku watahiniwa 68 wakikosa kushiriki kwa sababu mbalimbali.
Kati ya waliofanya mitihani, watahiniwa 595 sawa na asilimia 48.7 walifaulu, watahiniwa 589 (asilimia 48.2) wanarudia masomo yao, huku watahiniwa 39 sawa na asilimia 3.2 wakifeli na kuanza upya masomo yao katika ngazi husika.
Tags
Kurasa za Magazeti
Kurasa za Mbele na Nyuma za Magazeti
Magazeti
Magazeti ya Leo
Magazetini
Magazetini leo
Yaliyojiri Magazetini Leo























