Mo Dewji bilionea wa 13 Afrika, atangaza ajira 100,000 miaka mitano ijayo

Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya METL, Mohamed Dewji (Mo Dewji) ametajwa kuwa Bilionea pekee Afrika Mashariki na Bilionea aliyeshika nafasi ya 13 barani Afrika kati ya mabilionea 18 wenye ukwasi mkubwa kwa mwaka 2021, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mo mwenye umri wa miaka 45 amepanda nafasi ya tatu zaidi kutoka ya 16 ya mabilionea 20 wa Afrika kwa ripoti ya mwaka 2020.

Akizungumza juu ya hatua hiyo ya kupanda nafasi tatu zaidi Afrika, Mo Dewji ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli kwa kuendelea kuweka mazingira bora kwa wawekezaji ambayo yamemuwezesha kufikia hatua hiyo. 

Mo Dewji amesema, kwa hatua hiyo anaamini shauku yake ya kwenda kutoa ajira 100,000 kupitia kampuni yake ifikapo 2025 itatimia. 

Kwa sasa, METL inatoa ajira 33,000 kwa makundi mbalimbali ya Watanzania. Aidha, ameendelea kuwa bilionea kijana barani Afrika kwa miaka sita mfululizo sasa.

Kwa mujibu wa jarida maarufu la masuala ya fedha la Forbes, Mo Dewji ana utajiri wa dola bilioni 1.6 kwa mwaka huu, hii ikiwa ni sawa na mwaka jana.Pia ameendelea kuwa miongoni ma matajiri wa umri mdogo zaidi Afrika.

Mohammed Dewji ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa METL iliyoanzishwa na baba yake miaka ya 1970 anaelezwa kuisimamia kwa ufanisi mkubwa, hatua ambayo imewezesha kuleta ushindani mkubwa ndani na nje ya Tanzania.

METL ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwemo vyakula, sabuni na vinywaji, usagaji nafaka na nyingine nyingi. Kampuni hiyo inatoa huduma Ukanda wa Mashariki, Kusini na Katikati mwa Afrika.

Aidha, METL ina shughuli zake katika nchi sita barani Afrika na ina malengo ya kujipanua zaidi katika maeneo mengine.

Mo Dewji ndiye bilionea Mtanzania pekee aliyesaini mkataba mwaka 2016 wa kutoa kwa wahitaji nusu ya mali yake.

Kwa mujibu wa taarifa, Mo Dewji Foundation ndio asasi ambayo aliianzisha ili kutekeleza nia yake hiyo na kazi yake kubwa ni kusaidia watanzania wasiojiweza kwa upande wa afya,elimu na maendeleo ya jamii.

Mbali na biashara na shughuli za jamii Mo Dewji amewahi kuwahi kuwa mwanasiasa mwaka 2005 mpaka 2015 kwani alikuwa mbunge wa Singida Mjini.

Dewji pia ni mpenzi wa michezo na amewekeza katika klabu ya mpira ya Simba ya Tanzania, uwekezaji ambao unatajwa kuwa na matokeo mazuri katika soka la Tanzania.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wameieleza Diramakini (www.diramakini.co.tz) kuwa, kutokana na moyo wa Mo Dewji wa kujitoa katika kusaidia jamii kupitia sehemu ya faida za biashara zake na maarifa ya kuwekeza zaidi huenda akazifikia ndoto za kutoa ajira zaidi ya hizo ndani ya muda mfupi.

"Ukiwa na moyo wa kujitoa kwa wenye mahitaji, ni rahisi zaidi kuchanua kiuchumi, tunalitambua hilo kwa huyu Mtanzania mwenzetu ambaye amekuwa na moyo huo na kila wakati anawazo jipya la kibiashara,"Mchambuzi huyo ameieleza Diramakini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news