Mpango wa JIFUNZE wajengea uwezo wanafunzi kujua kuhesabu, kusoma shule za msingi Kisarawe

Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani kwa kushirikiana na Shirika la Uwezo Tanzania na Champion Chanzige chini ya Mpango wa JIFUNZE imefanikiwa kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuhesabu katika shule tano zilizopo wilayani humo katika kipindi cha kuanzia Septemba 2019 hadi Septemba 2020,anaripoti Ahmad Nandonde (Diramakini) Kisarawe.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwengelo (katikati) amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora kuanzia shule za msingi hadi sekondari.

Akitoa taarifa ya mafanikio ya mradi wa huo unaotekelezwa katika halmashauri hiyo afisa elimu taaluma, John Malibiche amesema halmashauri kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kupunguza idadi ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuhesabu.

Amesema, halmashauri imefanikiwa kupima maendeleo ya watoto hao waliokuwa katika mpango huo kwani kati ya wanafunzi 456 walioshiriki katika mpango huo katika shule hizo tano wanafunzi 409 wameweza kusoma na kuhesabu.

Malibiche ameongeza kuwa, katika mitihani ya darasa la nne kitaifa kati ya shule hizo tano shule tatu zimefanya vyema katika mwaka 2020, kwani wanafunzi wameweza kusoma na kujibu vyema majibu kupitia mitihani hiyo ya kujipima.
"Hakika mpango wa jifunze kwa siku 30 kama tulivyoona umeanza kuzaa matunda, kwani ukiangalia hata majaribio ya kawaida tumeona jinsi mtoto anavyoweza kusoma na kujibu maswali ipasavyo na si tu majaribio ya darasani bali hata mtihani wa taifa kwa darasa la nne tumeona idadi ya ufaulu imeongeza,’’amesema Malibiche.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi mmoja wa wazazi mwenye mtoto aliyenufaika na mpango huo, Bi. Fatma Juma ameeleza kufurahishwa na mpango huo ambao tangu kuanzishwa kwake umeendelea kuwa chachu kwa watoto wao na hivyo kuleta muamko wa kielemu.

‘’Kwa kweli mwanzoni mtoto alipokuwa akitoka shule ilikua ni nadra kumuona akishika daftari kujikumbushia aliyoyasoma shuleni, lakini kwa sasa tangu mpango huo umeanza naona kuna mabadiliko makubwa sana, hivyo nawashukuru wadau na pengine ikiwezekana mpango huo usambae maana leo imetokea kwa mwanangu kesho natamani umfikie mtoto wa mwenzangu,’’amesema Fatma.

Katika wilaya ya Kisarawe mpango wa jifunze umeweza kuzikifikia shule tano zenye watoto wasiojua kusoma na kuhesabu kuanzaia darasa la tatu mpaka la sita na miongoni mwa shule zilizopitiwa na mpango huo ni Manerumango, Madugike, Kidugalo, Mtakayo na Mitengwe.

Post a Comment

0 Comments