Naibu Waziri Mabula awashukia wakurugenzi halmashauri

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendelea ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amewajia juu baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri kwa kushindwa kuzihudumia idara za ardhi katika halmashauri zao na kuzifanya idara hizo kufanya kazi katika mazingira magumu, anaripoti na Munir Shemweta (WANMM) Pwani.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akizungumza na Watendaji wa Sekta ya Ardhi, uongozi wa mkoa wa Pwani wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri wakati wa ziara yake katika mkoa huo kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) tarehe 31 Desemba 2020. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhandisi Martini Ntemo na katikati ni Katibu Tawala Msaidizi Uchumi, Shangwa Twamala.(Picha na Munir Shemweta-WANMM/Diramakini).

Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi, uongozi wa mkoa wa Pwani na Wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo tarehe 31 Desemba 2020 akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kukagua miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika mkoa wa Pwani, Dkt. Mabula amesema kuna baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri wamekuwa wakorofi na kuziona idara za ardhi kama siyo sehemu ya idara zao na kuziacha bila kuzihudumia. 

Amesema, baada ya kutoka waraka uliohamisha Maafisa Ardhi kurudi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuna baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri waliamua kujivua kuzihudumia idara hizo kwa kisingizio kuwa idara hizo sasa haziko chini yao na zimerejeshwa wizarani.
Sehemu ya Watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Pwani wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na miradi ya ujenzi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika Mkoa wa Pwani tarehe 31 Desemba 2020.(Picha na Munir Shemweta-WANMM/Diramakini).

Dkt. Mabula amesema, waraka uliotolewa na kusambazwa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ulieleza wazi kuwa wajibu wa Wizara ya Ardhi kwa watumishi wa sekta hiyo utakuwa kwenye masuala ya sera, ajira na nidhamu lakini usimamizi utaendelea kubaki kwa wakurugenzi wa halmashauri. 

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, majukumu ya kupanga miji ni ya halmashauri za miji, manispaa na majiji hivyo wakurugenzi wa halmashauri bado wana wajibu wa kuzihudumia idara hizo ili ziweze kupanga miji vizuri pamoja na kutoa huduma zinazohusiana na masuala ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki iliyopo Kibaha mkoa wa Pwani wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).(Picha na Munir Shemweta-WANMM/Diramakini).

‘’Hawa ni watumishi wenu kama walivyo wale wa idara nyingine za afya, elimu nk hivyo mnapaswa kuwahudumia vizuri ikiwemo kuwapatia vitendea kazi ili waweze kufanya kazi vizuri,’’amesema Dkt. Mabula. 

Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kubadilika na kuanza kuzihudumia idara za ardhi vizuri kwa kuzipangia idara hizo bajeti ya kutosha pamoja vitendea kazi kama magari na vifaa vya kupimia ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. 

Akigeukia suala la ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi, Naibu Waziri Mabula aliwataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuziwezesha idara za ardhi ili ziweze kufuatilia madeni ya wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi katika maeneo mbalimbali. 

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, mkoa wa Pwani pekee unadai bilioni 32, 762,665,972 za kodi ya pango la ardhi kutoka kwa wadaiwa mbalimbali na kusisitiza kuwa kama idara za ardhi zitawezeshwa vizuri zinaweza kukusanya mapato mengi yatakayosaidia utekelezaji miradi mbalimbali kama vile ya afya, elimu na miundombinu ukilinganisha na idara nyingine.
Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami akisisitiza jambo mbele ya Watendaji wa Sekta ya Ardhi mkoa wa Pwani wakati wa kikao kazi baina ya watendaji hao na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula tarehe 31 Desemba 2020.(Picha na Munir Shemweta-WANMM/Diramakini).

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masamia amesema, pamoja na mikakati iliyowekwa na Wizara yake katika kukusanya kodi bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika suala hilo kutokana na hadi kufikia Desemba 31, 2020 ni Bilioni 61 ndizo zilizokusanywa na kutaka juhudi za makusanywa kuongezwa katika kila halmashauri. Malengo ya Wizara katika mwaka wa fedha 2020/2021 ni bilioni 200. 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki uliopo wilayani Kibaha mkoani Pwani mradi unaojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki iliyopo Kibaha mkoa wa Pwani wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Kulia ni Meneja wa Huduma za Jamii na Mahusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa, Muungano Saguya. (Picha na Munir Shemweta-WANMM/Diramakini).

Akiwa katika mradi wa ujenzi wa Ofisi hiyo, Dkt. Mabula alilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kazi nzuri ya ujenzi wa miradi mbalimbali iliyokabidhiwa na kulitaka kuhakikisha ujenzi wa miradi hiyo unakamilika kwa wakati na kwa ubora ili kujenga imani kwa wateja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news