Prof.Manya atoa maelekezo utoaji leseni mgodi wa Mwime 2

 Amesema Leseni hutolewa kwa kutoa Matangazo na Kamati kukaa pamoja, ahaidi kuboresha mahusiano ya Ofisi ya Madini na wachimbaji ili kupunguza migogoro, asema Rush hazitaendelea, baadaye tutatoa leseni



Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya amesema migogoro yote inayohusu leseni za uchimbaji madini lazima zitatuliwe kupitia Tume ya Madini ambayo ndio taasisi yenye dhamana ya utoaji leseni hapa nchini wakati alipokutana na Viongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Mwime 2 katika Ukumbi wa Mikutano wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Jijini Dodoma, anaripoti Steven Nyamiti (WM) Dodoma
Prof. Shukrani Manya amewataka Viongozi wa Mgodi wa Mwime 2 kufuata Sheria na Taratibu zilizowekwa na Wizara ya Madini wakati wanapohitaji leseni kwenye maeneo ya uchimbaji ili kuondoa migogoro inayojitokeza mara mara.

Ametoa maelekezo hayo leo, Januari 25. 2021 wakati alipokutana na Viongozi wa Mgodi wa Mwime 2 wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa mgodi huo kutoka Kahama Mkoani Shinyanga ambapo wamefika ofisini kwake kupata maelekezo ya sababu ya ucheleweshwaji wa maombi ya leseni ya Mgodi wa Mwime 2.
Naibu Waziri ametoa maelekezo hayo baada ya kuelezwa migogoro waliyonayo na Ofisi ya Madini wilaya ya Kahama kuhusu ucheleweshwaji wa kupatiwa namba ya malipo “control number” kwa ajili ya kupatiwa leseni halali ya eneo la machimbo yaliyopo Mwime 2.
“Historia ya mgogoro wa Mwime 2 ni wa muda mrefu toka nikiwa kwenye nafasi ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini. Mimi ndiye niliyepitia leseni zenu tatu mnzazozitumia sasa. Kwa hiyo historia yenu yote ninaitambua. Ni vema mkafuata Sheria na Taratibu zilizowekwa na Wizara kupitia watoa leseni Tume ya Madini,"amesema.

Aidha, Naibu Waziri amewataka Viongozi hao wa mgodi wa Mwime 2 kusubiri kikao cha kamati ya wilaya ya Ulinzi na Usalama kitakachoongozwa na Mkuu wa wilaya mapema Mwezi Februari, 2021 kwa ajili ya kutoa maamuzi ya mgogoro huo. 
Pia amewaeleza ili kuondoa migogoro hii mara kwa mara ni vyema kupokea maelekezo kutoka kwa afisa madini mkazi na kuyafanyia kazi kabla ya kuamua kuonana na Waziri mwenye dhamana kwanza.
Mhandisi Yahaya Samamba akipokea maelekezo toka kwa Naibu Waziri amesema suala hilo analifahamu. “Ni vyema tukasubiri maelekezo ya kamati ya Ulinzi ya wilaya na kwa sababu nyinyi ndio watu wa mwanzo wa eneo hilo kuanza kufanya kazi nina imani mtapewa kipaumbele kuliko kugawa eneo kwa watu wageni kutoka nje ya Shinyanga,"amesisitiza Sambamba.

Naye, Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi wa Mgodi wa Mwime 2, Emmanuel Mlimandago amesema wanaiomba Tume ya Madini iwasaidie kutatua mgogoro huo ili wapate leseni ya kuendelea kuchimba katika eneo hilo.

“Tumeboresha miundombinu ya barabara katika maeneo yanayozunguka mgodi wa Mwime 2. Awali kulikuwa na changamoto ya mgodi kuingiliwa na maji lakini tuliweka juhudi ya ujenzi wa tuta kubwa ambalo limekuwa msaada mkubwa katika kazi zetu,"amesema Mlimandago.

Pia, Afisa Mahusiano wa mgodi wa Mwime 2 Christopher Bundala amemuomba Prof. Manya kumuelekeza Kaimu Mtendaji wa Tume ya Madini Yahaya Samamba kutembelea mgodi wa Mwime 2 wilayani Kahama ili mgogoro huo uweze kutatuliwa vizuri. Amesema ni vyema Tume ya Madini ikatutembelea ili isikilize pande zote za mgogoro huu kabla ya kutoa maamuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news