Rais Dkt. Mwinyi autaka uongozi wa ZSSF kusimamia ipasavyo amana za wanachama

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kufanya kazi kwa karibu na uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) katika kuhakikisha amana zote za wananchama zinasimamiwa ipasavyo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikata utepe kulifungua jengo jipya la Ofisi za ZSSF Tibirizi “Hifadhi Building” Chakechake Pemba na (kulia kwa Rais) Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Maalim Seif Sharif Hamad, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.(Picha na Ikulu/ Diramakini).

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Januari 5, 2021 katika hotuba yake ya ufunguzi wa jengo jipya la “Hifadhi Building” la (ZSSF) lililopo Tibirinzi, Wilaya ya Chake Chake , Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo pia, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad alihudhuria.

Katika hotuba hiyo Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, ni jukumu la Serikali kuhakikisha inachukua hatua zionazofaa na kwa wakati katika kuhakikisha mfuko huo unaendelea kuimarika, unaongozwa na kusimamiwa na viongozi walio makini na wanaojiepusha na vitendo vya ubadhirifu, rushwa na wizi.

Amesisitiza kwamba, Serikali itahakikisha wanachama wa mfuko huo wanaishi bila kuwa na wasiwasi wa hatma ya amana wanayowekeza ambayo mara nyingi huwa nitegemeo kubwa katika maisha ya wafanyakazi baada ya kustaafu.

Amesema kuwa, ni lazima viongozi wa ZSSF wahakikishe kwamba utekelezaji wa dhamira njema ya kutumia amana ya wanachama wa mfuko wanayokusanya iambatane na mipango imara ya kusimamia uwekezaji huo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akiondoka katika viwanja vya Jengo Jipya la Ofisi za ZSSF la Hifadhi Building, baada ya kulifungua ikiwa ni shamrashamra za sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kulia kwa Rais ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali.(Picha na Ikulu/Diramakini).

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewataka viongozi kuhakikisha kwamba fedha inayowekezwa inazalisha na shughuli zote za uendeshaji wa taasisi hiyo zinafanywa kwa weledi, umahiri na umakini mkubwa.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kwamba uongozi ni lazima kila wakati uhakikishe kwamba idadi ya fedha zinazohitajika kulipa stahiki za wanachama wanaostaafu na mafao mbalimbali zinakuwepo kila wakati bila ya nenda rudi na usambufu wa aina yoyote ile.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mjenzi wa Jengo la Ofisi za ZSSF Hifadhi Building lililopo katika eneo la Tibirinzi Chakechake Pemba Mkurugenzi wa Kampuni ya Quality Building Contractor, Ndg. Khamis Haji akitoa maelezo ya ujenzi huo wakati wa ufunguzi uliofanyika Januari 5, 2021 na kulia kwa Rais ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Maalim Seif Sharif Hamad na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali.(Picha na Ikulu/ Diramakini).

Amesema kuwa, kuwepo kwa majengo ya ofisi za kisasa ni hatua muhimu katika juhudi hizo za kuvutia wawekezaji kisiwani Pemba.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, kazi kubwa imefanywa na Serikali ya Awamu ya Saba ya kuimarisha mazingira ya kufanya kazi kisiwani Pemba ambapo majengo mengi ya serikali yamejengwa na mengine yamefanyiwa matengenezo makubwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza viongozi wa ZSSF kuhakikisha taratibu za ukodishaji wa maduka yaliyomo katika maduka mapya ya Michenzani Mall na jengo la Thabit Kombo kwani ni kipindi kirefu tangu majengo hayo yalipozinduliwa rasmi.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alitoa pongezi kwa wakandarasi wa ujenzi wa jengo hilo Kampuni ya kizalendo ya Quality Building Contractor pamoja na kampuni ya Arqes Africa kwa kazi kubwa waliyoifanya.

Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kutoa pongezi za dhati kwa uongozi wa Wizara ya Fedha, uongozi wa ZSSF pamoja na Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa kwa maandalizi mazuri ya shughuli hiyo na kwa kumualika kuwa mgeni rasmi.

Amesisitiza kwamba ni jukumu la kila mwananchi wa Zanzibar kuendelea na kudumisha fikra njema za waasisi wa nchi wakiongozwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kushoto kwa Rais Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Maalim Seif Sharif Hamad wakimsikiliza Meneja Mipango Uwekezaji na Utafiti wa ZSSF, Ndg. Abdulazizi Ibrahim Iddi akitoa maelezo wakati wa kutembelea moja ya nyumba iliyopo katika jengo la Ofisi za ZSSF “Hifadhi Building “ baada ya kulifunga leo Januari 5, 2021 ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.(Picha na Ikulu/ Diramakini).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali alisema kuwa, kukamilika kwa ujenzi huo ni mafanikio makubwa kwani itaongeza ufanisi na mapato.

Amesema kuwa, kukamilika kwa jeno hilo kunatokana na ushirikiano wa Mfuko wa ZSSF, Wizara na Bodi ya Mfuko huo sambamba na ushauri mkubwa uliokuwa ukitolewa na Rais juu ya Mfuko huo huku akieleza haja kwa taasisi za Serikali kuwa makini katika kutekeleza miradi kama hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya miradi kabla ya ujenzi wake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe.Jamal Kassim Ali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi kuzungumza na wananchi wa Pemba wakati wa hafla ua ufunguzi wa Ofisi za ZSSF Tibirinzi Pemba.(Picha na Ikulu/ Diramakini).

Ameeleza kwamba, fedha zliozotumika ni michago ya wanachama wa ZSSF hivyo, ni vyema zikarudi na kupata tija kwa wanachama wa mfuko huo huku akiwataka wale wote watakao kodi jengo hilo wanapaswa kulipa fedha zinazotakiwa.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Khamis Mussa Omar alisema kuwa, kwa bahati mbaya ZSSF Tawi la Pemba awali ilikuwa ikitoa huduma zake katika maeneo ya kukodi katika majengo ya watu binafsi, ofisi za kudumu zilianzishwa mwaka 2004 katika jengo lake la Kituo cha Mikutano (Pemba Conference Centre) ambalo pia, linatoa huduma za malazi afisi ambayo ilikuwa ndogo sana.

Hivyo, ZSSF iliamua kujenga jengo hilo jipya la kisasa linaloendana na mahitaji ya sasa na hapo baadae ambapo mkataba wa ujenzi ulitiwa saini tarehe 4 Julai 2019 baina ya ZSSF na Kampuni ya Kizalendo ya Quality Building Contractors baada ya Kampuni hiyo kuwa mshindi wa zabuni.
Kufuatia kusainiwa kwa mkataba huo, ujenzi ulianza rasmi tarehe 1 Agosti 2019 ambao ni mradi uliokuwawa miezi 12 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 31 Julai,2020 lakini kutokana na changamoto zilizobainika wakati wa ujenzi na athari ya maradhi ya COVID 19 lakini hata hivyo, ujenzi ulikamilika rasmi Oktoba 2020.

Mapema Rais Dkt. Mwinyi mara baada ya kulifungua jengo hilo alipata fursa ya kulitembelea na kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa ZSSF pamoja na maelezo kutoka kwa Mkandarasi wa jengo hilo Khamis Ali kutoka Kampuni ya Quality Building Contractor Limited.

Kwa maelezo ya uongozi wa ZSSF jengo hilo la ghorofa tatu limegharimu jumla ya sh. Bilioni 7.9 zimetarajiwa kutumika katika ujenzi wa jengo hilo ambapo hadi sasa jumla ya sh.Bilioni 5.3 ameshalipwa mjenzi huku mjenzi huyo mzalendo akitoa shukurani kwa Rais kwa Dkt. Mwinyi kuwapa kipaumbele wajenzi wazalendo.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi ametembelea ujenzi wa barabara unaoelekea katika maeneo huru ya vitega uchumi Micheweni na kufika eneo la Maziwangombe na kuwaeleza wananchi wa Micheweni kwamba fursa za ajira zitakapoanza wao watapewa kipambele.

Amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kwa kila wilaya kutafuta maeneo ya uwekezaji huku akisisitiza kwamba kuna haja ya eneo hilo la Micheweni kuweka viwanda vinavyohusiana na uchumi wa buluu zaidi kutokana na mazingira yake.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza haja ya kusogezwa kwa huduma nyingine muhimu zikiwemo maji na umeme ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kurahisisha uwekezaji katika eneo hilo na kuwataka wizara husika kupanga na kuweka fedha kwa ajili ya mchakato huo.

Amesema, miezi minane kwa barabara ya kilomita 2.8 iliyoelezwa na wajenzi wa barabara hiyo kutoka uongozi wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi ni mingi sana na kuutaka wapunguze ili shughuli ziweze kuendelea. 

Amesisitiza kwamba ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni zitafanyiwa kazi huku akieleza haja ya kujengwa barabara yote badala ya kujengwa eneo hiyo ya ambayo ujenzi wake unaendelea hivi sasa.

Ameeleza azma ya Serikali ya kuweka viwanda katika eneo hilo kwa ajili ya kupata ajira zikiwemo zile ajira 300,000 zilizoelezwa katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 ili nyingine zitoke katika eneo hilo huku akiwapongeza wananchi wa Micheweni kwa kuupokea mradi huo.

Mapema Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Maendeleo ya Uwekezaji (ZIPA), Shariff Ali Shariff amemueleza Rais, Dkt. Mwinyi mipango na mikakati iliyowekwa na ZIPA juu ya eneo hilo la uwekezaji.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib kwa niaba ya wananchi wa Micheweni ametoa shukurani kwa Rais Dkt. Mwinyi kwa uamuzi wake wa kuijenga barabara hiyo na kusema kwamba wananchi wamefarijika.

Post a Comment

0 Comments