Wadaiwa sugu wa ardhi kufutiwa umiliki kwa mujibu wa sheria

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amewaagiza maafisa ardhi katika halmashauri nchini kuanza kuwafutia umiliki wa ardhi wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango wa ardhi kwa mujibu wa sheria, anaripoti Munir Shemweta (WANMM) Simiyu.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akisisitiza jambo wakati wa kikao chake na watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Simiyu wakati wa ziara ya siku moja katika mkoa huo leo Januari 25, 2021. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi , Festo Kiswaga na kulia ni Kamishna Msaidizi Mkoa wa Simiyu, Essau Mawakatumbula.(Picha na Munir Shemweta-WANMM).

Mmiliki yeyote wa ardhi anapaswa kulipa kodi ya pango la ardhi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa masharti ya umiliki kwa mujibu wa kifungu 33 (1) cha Sheria ya Ardhi Na 4 ya mwaka 1999.

Aidha, kifungu cha 48(1) (g) kinaelekeza kuwa kodi ya ardhi isipolipwa kwa kipindi cha miezi sita mara baada ya mmiliki kutumiwa ilani ya madai mmiliki huyo anaweza kufutiwa milki yake.

Akiwa katika ziara yake ya siku moja leo Januari 25, 2021 Mkoa wa Simiyu kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi na kuzungumza na watendaji wa sekta ya ardhi, Naibu Waziri wa Ardhi amewaelekeza wataalamu wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanatekeleza matakwa hayo ya kisheria Na 4 ya mwaka 1999 kwa kuisimamia vyema.

"Nawaagiza Maafisa Ardhi katika halmashauri zote kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake na msiendelee kuwalea wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi na mzingatie sheria Na 4 ya ardhi wakati mnatekeleza majukumu yenu ikiwemo kufuta umiliki baada ya miezi sita kwa wadaiwa,"amesema Dkt.Mabula.

Amewataka wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba na Wilaya kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kusaidia kuharakisha usikilizaji mashauri ya wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi ili kuweza kutoa haki kwa haraka.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akikabidhi Hati ya Ardhi kwa Wenza Ramadhani na Martha Zongo wakazi wa Bariadi mkoa wa Simiyu wakati wa ziara ya siku moja katika mkoa huo leo Januari 25, 2021.kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga. (Picha na Munir Shemweta-WANMM).

"Hatuhitaji watu wapelekwe kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba na Wilaya halafu mashauri yakae huko kwa miaka mitano tunataka mashauri yaishe haraka kwa mujibu wa sheria,"amesema Naibu Waziri Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amewataka eakurugenzi katika halmashauri za Mkoa wa Simiyu kuzitumia vyema idara za ardhi katika masuala yote yanayohusu ardhi ikiwemo upangaji wa miji kwa kuwa mamlaka za upangaji ziko chini ya halmashauri hizo na kusisitiza kuwa wakurugenzi hao wasipozitumia vyema idara za ardhi kuna hatari ya kuendelea kwa ujenzi holela.

Aidha, Dkt.Mabula ameonesha kutoridhishwa na kasi ndogo ya ukusanyaji kodi ya pango la ardhi katika Mkoa wa Simiyu ambapo hadi sasa mkoa huo umekusanya shilingi 87,654,120 sawa na asilimia 24 huku mkoa ukidai zaidi ya Bilioni 5.5 kutoka kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Ardhi katika Mkoa wa Simiyu, Essau Mwakatumbula amemueleza Naibu Waziri wa Ardhi, Dkt. Mabula kuwa ofisi yake itahakikisha inaongeza kasi ya kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi ili iweze kukusanya madeni na kufikia malengo ya makusanyo ya kodi ya ardhi iliyojiwekea.

Hata hivyo, amesema pamoja na jitihada za mkoa katika kuhakikisha wadaiwa wote wa kodi ya ardhi wanalipa kuna changamoto kwa baadhi ya taasisi kutoonesha jitihada zozote za kulipa na kutolea mfano wa VETA, SIDO na SHIRECU.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news