Chuo cha Utumishi wa Umma chatakiwa kuendelea kujenga nidhamu na uadilifu kwa watumishi wa umma

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Humprey Polepole (Mb) amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kina jukumu la kuhakikisha kinaendelea kujenga nidhamu na uadilifu kwa watumishi wa umma na viongozi katika Utumishi wa Umma ili waweze kutoa mchango katika maendeleo ya taifa, anaripoti James K. Mwanamyoto (OR-Utumishi) Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humprey Polepole (Mb) akiwahimiza Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Kampasi ya Dar es Salaam kutoa mafunzo yatakayowajengea Watumishi wa Umma nchini nidhamu ya Utendaji kazi na uadilifu.

Mhe. Polepole ametoa rai hiyo mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa anayoiongoza kutembelea makao makuu ya Chuo cha Utumishi wa Umma jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho chenye dhamana ya kutoa mafunzo kwa Watumishi wa Umma yanayowawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa na watumishi wa TPSC wakisikiliza maelekezo ya Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Humprey Polepole (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya TPSC.


Mhe. Polepole amesema, chuo hakina budi kuendelea kutoa mafunzo yenye tija ili kizazi kipya kilichoingia na kinachoendelea kuingia katika Utumishi wa Umma kiendelee kuishi katika mila, utamaduni, desturi na miiko ya Utumishi wa Umma.

Mhe. Polepole amefafanua kuwa, Utumishi wa Umma nchini umejengeka katika mila, utamaduni, na desturi, hivyo Chuo cha Utumishi wa Umma pekee ndio kina jukumu la msingi kuhakikisha kinatoa mafunzo ambayo yatajenga utamaduni utakaoimarisha nidhamu ya utendaji kazi, uadilifu na uzalendo kwa Watumishi wa Umma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika Chuo cha Utumishi wa Umma yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuwa, suala la kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma kiutendaji na nidhamu limepewa uzito unaostahili na ofisi yake kwa kuwataka waajiri wote kuhakikisha wanatenga bajeti itakayowawezesha watumishi wao kupata mafunzo yanayotolewa katika Chuo cha Utumishi wa Umma.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewaomba wajumbe wa kamati hiyo kutumia mamlaka waliyonayo kushirikiana na Ofisi yake kuwahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Taasisi za Umma kutenga fedha zitakazowawezesha Watumishi wa Umma kupata mafunzo katika Chuo cha Utumishi wa Umma.

Mhe. Ndejembi ameiahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ili kuboresha huduma zinazotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.

Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo katika Nyanja za uongozi, menejimenti na utawala kwa ngazi za Cheti, Stashada na Astashahada. Pia chuo kinafanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalam.
Baadhi ya watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Dar es Salaam wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humprey Polepole (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya TPSC.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Saashisha Mafue ambaye ni mnufaika wa mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma akitoa ushuhuda wa namna alivyopata mafunzo katika chuo hicho wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya TPSC.
Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Dkt. Emmanuel Shindika akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya chuo chake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya TPSC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news