Serikali kuboresha mazingira yatakayowaneemesha wakulima wa maparachichi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali inatarajia kujenga chumba maalumu cha kuhifadhi baridi (cold room) katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe kwa ajili ya kuhifadhia maparachichi pamoja na mazao mengine kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Bw. Steven Mlimbira (kulia) ambaye ni mkulima wa Parachichi wakati alipotembelea shamba la mkulima huyo katika kijiji cha Maheve wilayani Njombe, Machi 12, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Machi 12, 2021 wakati akizungumza na wananchi baada ya kutembelea shamba la mkulima wa parachichi Bw. Steven Mlimbira katika kijiji cha Maheve wilayani Njombe.

Pia, Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote za mkoa wa Njombe zinazolima zao la parachichi zianzishe vitalu vya kuotesha miche katika eneo la kuanzia ekari tatu na kuigawa bure kwa wakulima, lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi wengi kulima zao hilo na kuongeza uzalishaji.

Kufuatia umuhimu za zao hilo, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Mwita Rubirya afuatilie maendeleo ya vikundi vya wakulima wa parachichi na kushirikiana nao katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama parachichi wakati alipotembelea shamba la Bw. Steven Mlimbira katika kijiji cha Maheve wilayani Njombe, Machi 12, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu amesema zao la parachichi ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na linazalishwa kwa gharama nafuu, hivyo amewahimiza wananchi kulima zao hilo kwa ajili ya kujipatia fedha zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.

Amesema zao la parachichi limechangia katika kutatua tatizo la ajira nchini ambapo watu wengi wameweza kujiajiri na kuajiriwa, hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata zao hilo kwa kuwa linafaida kubwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama miche ya parachichi wakati alipotembelea shamba la Bw. Steven Mlimbira (kushoto) katika kijiji cha Maheve wilayani Njombe, Machi 12, 2021.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kadhalika, Waziri Mkuu amempongeza Bw. Mlimbira kwa kuwa na shamba kubwa la parachichi ambalo limewezesha kutoa ajira kwa wananchi wengi pamoja na kuwahamasisha walime zao kwa kuwagawia miche kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake, Bw. Mlimbira amesema ekari moja hupandwa miti 64 ya parachichi kwa nafasi ya mita nane kwa mita nane na mche mmoja huuzwa kati ya shilingi 2,000 hadi 5,000 kwa kutegemea na ukubwa wa mche.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama miche ya parachichi wakati alipotembelea shamba la Bw. Steven Mlimbira katika kijiji cha Maheve wilayani Njombe, Machi 12, 2021.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema mti mmoja wa parachichi unatoa kiasi cha wastani wa kilo 150 hadi 500 ambapo inakadiriwa kuzalisha parachichi zenye thamani ya shilingi 200,000 hadi 750,000 kwa mti wenye umri wa miaka mitano hadi 10 na huanza kuzaa baada ya mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news