Washikiliwa kwa kosa la kusafirisha nchi za nje vinyonga 74 na nyoka 6

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inawashikilia Watuhumiwa watatu raia wa Tanzania na kwa kosa la kushirikiana na raia wa Jamhuri wa Czeck kusafirisha nje ya nchi vinyonga 74 na nyoka 6 kinyume na sheria, anaripoti Lusungu Helela (WMU).
Akizungumza na Vyombo vya habari mkoani Iringa, Waziri wa Maliasili na Utali, Dkt.Damas Ndumbaro amesema vinyonga na nyoka hao walikamatwa na Maafisa wa Forodha wa Austria wakiwa kwenye begi ambalo ndani yake waliwekwa kwenye soksi na kuingizwa kwenye vifungashio (container) vya plastiki.

Amesema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani ambapo watakabiliwa na makosa ya kusafirisha nje Wanyamapori hao bila kibali, Uhujumu uchumi pamoja na utakatishaji fedha kupitia Biashara hiyo.

Dkt.Ndumbaro amesema vinyonga na nyoka hao ambao waliokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Vienna nchini Austria inadaiwa wametoka Tanzania katika Milima ya Usambara katika ambako kuna aina mbalimbali za vinyonga.

Akizungumzia jinsi Watuhumiwa hao walivyowanaswa, Waziri wa Maliasili na Utali, Dkt.Damas Ndumbaro amesema baada ya kupata taarifa kupitia mitandao ya kijamii, Wizara kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama na kwa kutumia Kikosi Kazi Taifa Dhidi Ujangili iliunda Kikosi Maalum cha kuchunguza tukio hilo.

Amesema kupitia taarifa za Kiintelijensia Kikosi Maalum kilifanikiwa kupata jina la mtuhumiwa aliyesafirisha vinyonga hao ambaye raia wa Jamhuri ya Czeck.

Hata hivyo, amesema uchunguzi bado unaendelea sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kubaini namna vinyonga na nyoka hao walivyopitishwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere bila kugundulika.

Amesema Watuhumiwa watakaobainika kuhusika na uhalifu huo wataunganishwa na wenzao ambao tayari wamekamatwa.

Pamoja na juhudi hizo, Waziri Dkt.Ndumbaro amesema Serikali ya Tanzania itashirikiana na nchi ya Austria katika uchunguzi unaoendelea ikiwa ni pamoja na kuwarudisha Tanzania vinyonga pamoja na nyoka hao. 

Aidha, Amesema Serikali itawasiliana na Jamhuri ya Czeck ili watuhumiwa hao ambao ni raia wake wachukuliwe hatua.

Katika hatua nyingine , Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro amesema Serikali inakusudia kuifuta kabisa Biashara ya wanyamapori hai ambayo ilizuiwa tangu mwezi Mei, 2016.

Amesisitiza kuwa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kufanya biashara ya wanyamapori hai ndani na nje ya nchi mtu yeyote atakayebainika kufanya biashara hiyo wakati imezuiliwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news