Waziri Biteko atoa mwongozo kwa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi (NMCC)

Asisitiza Pendekezo la kuweka Hati Fungani ya GGM kusimamiwa, Aelekeza Kamati Kufanya Utafiti wa kisayansi Ufungaji Migodi

Imeelezwa kuwa, Mpango wa Ufungaji Mgodi ni takwa la kisheria ambalo kila mmiliki wa leseni ya Uchimbaji wa kati (ML) na Mkubwa (SML) anapaswa kuzingatia Mwongozo wa kuandaa Mpango wa Ufungaji Migodi,anaripoti Steven Nyamiti (WM).
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini Doto Biteko, wakati akipokea taarifa ya Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi (NMCC) kilichofanyika Machi 12, jijini Dodoma.

Waziri Biteko ameongeza kuwa, Kamati itoe mapendekezo ya kudumu na kufanya kazi kubwa ili Taifa lipate majibu yenye manufaa na ione utofauti wakati wanapoandaa na kuboresha Mpango wa Ufungaji Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Amesisitiza kuwa, kulikuwa na udhaifu mkubwa wa kusimamia Sheria za ufungaji migodi huku akielekeza kuandaa taarifa ili Mpango wa Ufungaji Mgodi wa Dhahabu wa Geita utoe faida kwa Nchi na kusisitiza Ukaguzi wa Mgodi ufanyike kwa kina na kuandaa maswali yatakayoboresha Ufungaji Migodi kuwa wenye faida zaidi.

Aidha, Waziri Biteko ameieleza Kamati hiyo ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi kuwa, Mpango huo unatakiwa uzingatie masuala ya utunzaji wa mazingira, usalama, stahili na mafao ya wafanyakazi, na kuendeleza shughuli za kiuchumi na jamii kwa kuandaa miradi ya maendeleo mbadala ili kuhakikisha jamii inayozunguka mgodi inaendelea kunufaika baada ya mgodi kufungwa.
Naye, Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya akichangia katika taarifa hiyo ameieleza Kamati hiyo kueleza kama kuna changamoto za kiutendaji au uelewa kamati iwezeshwe ili kutatua changamoto zinazojitokeza. 

Na pia kamati inapaswa kuchukua uzoefu wa kujifunza kutoka katika Nchi zenye migodi ya muda mrefu ikiwepo South Africa na Canada kuhusu Ufungaji bora wa Migodi ili kwa kutumia mifano hiyo na sisi tuweze kuboresha zaidi na kujua njia wanazotumia wenzetu kwa maslahi ya taifa.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Migodi, Dkt. Abdulrahman Mwanga akiwasilisha taarifa Kuhusu taratibu zilizotumika kupitisha Mpango wa Ufungaji Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) ameeleza kuwa, Maeneo ya ufungaji hutofautiana kutoka mgodi mmoja na mwingine kutegemea na aina ya madini, uchimbaji, uchenjuaji na kiwango cha uharibifu wa mazingira.

Dkt. Mwanga amesisitiza kuwa, Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji ilipendekeza Ukarabati wa mazingira na Ufungaji Mgodi, Masuala ya kiuchumi na kijamii pamoja na Stahili na mafao ya wafanyakazi watakaosimamishwa kazi yatazingatiwa katika Ufungaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita.

Katika kikao hicho, Kamati ya Kitaifa imetoa mapendekezo juu ya utekelezaji wa Mpango wa Ufungaji Mgodi wa GGM na imeshauri Waziri wa Madini aridhie Hati Fungani itakayopendekezwa na kuidhinishwa kwa ajili ya gharama za ufungaji wa mgodi wa GGM kwa kuwa mgodi huo bado una uhai wa muda mrefu. Pia Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za serikali kuandaa Mwongozo wa Uwekaji na Matumizi ya Hati Fungani kwa ajili ya Ufungaji Migodi hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments