WAZIRI BITEKO AWATAKA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI KUITUMIA GST

Waziri wa Madini Doto Biteko, amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini kuitumia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kutumia wataalam, vifaa na taarifa za jiolojia zinazoandaliwa na GST katika kufanya shughuli za utafutaji , uchimbaji na uchenjuaji madini ili kufanya uchimbaji wenye tija kiuchumi na wenye kulinda mazingira,wanaripoti Samwel Mtuwa na Steven Nyamiti (WM).
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza jambo wakati wa Uzinduzi wa Kitabu cha Mwongozo wa Uchukuaji wa Sampuli za Miamba na Madini kwa Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika tarehe 11 Machi, 2021 Katika Ofisi zab GST Dodoma.

Waziri Biteko amesema hayo Machi 11,2021 wakati akifanya uzinduzi wa kitabu cha Mwongozo na Mafunzo kwa Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wadogo wa madini Tanzania (FEMATA), mwongozo huo unaoelezea namna bora ya uchukuaji wa sampuli za uchunguzi wa kimaabara pamoja na namna bora ya kufanya uchenjuaji madini.

Waziri Biteko ameeleza kuwa, kwa kipindi kirefu GST imekuwa ikifanya kazi zake za kitaalamu na wachimbaji wadogo kwa kuwapa elimu ya kitaalam kwa kutumia machapisho mbalimbali kama vile Vipeperushi, vitabu pamoja na kuwatembelea katika maeneo ya uchimbaji kwa lengo la kuwaelimisha wachimbaji wadogo juu ya utafutaji na uchimbaji bora wa madini, kwa kufanya hivyo GST kupitia tafiti za awali imekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa Sekta Madini nchini kwa kuzingatia mchango wake mkubwa katika pato la taifa ambao umefikia asilimia 5.2 kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

“Ndugu zangu wachimbaji, Madini ni sayansi hivyo ni vyema kutumia mafunzo haya ili kujifunza namna bora ya kutafuta, kuchimba na kuchenjua madini kwa kufuata maelekezo ya kisayansi kwa kufanya hivyo mtatua changamoto ya kuchukua sampuli na kufanya uchimbaji wa madini ulio na tija kiuchumi na kuleta maendeleo zaidi katika sekta hii kwa sababu mchimbaji atachimba bila kupoteza muda au mtaji,” Biteko alisisitiza.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dkt. Mussa Budeba akizungumza jambo wakati wa Uzinduzi wa Kitabu cha Mwongozo wa Uchukuaji wa Sampuli za Miamba na Madini kwa Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika tarehe 11 Machi, 2021 Katika Ofisi zab GST Dodoma.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba, alisema kuwa GST ilibaini uwepo wa changamoto ya uchukuaji sampuli za miamba zisizo zingatia taratibu za ubora kwa ajili ya uchunguzi wa maabara, kwa kutambua hilo GST imeamua kuandaa kitabu cha Mwongozo na Mafunzo ya siku mbili kwa Viongozi wa FEMATA juu ya namna bora ya uchukuaji sampuli za uchunguzi na uchenjuaji madini.

Akielezea kuhusu mwongozo huo, Dkt. Budeba alifafanua kuwa uchukuaji wa sampuli ndio nguzo kuu ya uchimbaji wa uhakika kwa kupitia mwongozo huu utawawezesha wachimbaji wadogo wengi kuwa na uwezo wa kutambua Mbale zenye uzalishaji mdogo, wa kati na wa kiwango cha juu hii itawawezesha kufanya kazi kwa kujiamini , kuongeza uzalishaji na kuokoa muda.
Waziri wa Madini Doto Biteko (Katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini, GST, Tume ya Madini na FEMATA wakati wa Uzinduzi wa Kitabu cha Mwongozo wa Uchukuaji wa Sampuli za Miamba na Madini kwa Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika tarehe 11 Machi, 2021 Katika Ofisi zab GST Dodoma.

Uzinduzi wa Mwongozo na Mafunzo kwa Viongozi wa FEMATA yameudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Madini akiwemo Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya,Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, GST , Tume ya Madini pamoja na Viongozi na Wachimbaji wa FEMATA kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Post a Comment

0 Comments