Rais Dkt.Mwinyi atoa wito kwa wafanyabiashara kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wafanyabiashara kuhakikisha kwamba bei za bidhaa hazipandishwi kwa sababu ya mwezi mtukufu ujao wa Ramadhani, anaripoti Mwandishi Maalum DIRAMAKINI.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akifuatilia hotuba ya Sala ya Ijumaa ikisomwa na Khatibu Sheikh Rajab Mohammed Faki (hayupo pichani) kabla ya Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Msikiti wa Amaan jijini Zanzibar leo Aprili 2,2021 na kushoto kwa Rais ni Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume na kulia kwa Rais ni Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh.Saleh Omar Kabi.(Picha na Ikulu).
Waumini wa Kiislam wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akizungumza na kutoa salamu baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Msikiti wa Amaan jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa salamu zake wa Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Msikiti wa Amani, Jijini Zanzibar.

Katika salamu hizo Alhaj Dkt. Mwinyi alieleza kwamba tayari dalili zimeshaanza kuonekana za wafanyabiashara kuanza kupandisha bei za bidhaa wakitarajia kwamba Ramadhani inakuja ili wapate faida zaidi jambo ambalo si zuri kufanyika mwezi huo mtukufu.

Hivyo, aliwasihi wafanyabiashara kutambua kwamba wakati wa Ramadhani ni wakati wa kuvuna thawabu kwa kuwatumikia watu kwa kupunguza faida wanazoziweka ili watu waweze kufunga vizuri na kuweza kumcha Mola wao badala ya kuanza kupandisha bei za bidhaa kama walivyoanza kufanya hivi sasa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Waumini wa Kiislam baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Msikiti wa Amaan jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu) Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi (kulia kwa Rais) baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Msitiki wa Amaan Jijini Zanzibar na (kushoto kwa Rais) Sheikh Rajab Mohammed Faki na Meya wa Jiji la Zanzibar Mhe. Mahmoud Mohammed Mussa.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kuwa anatambua kwamba hivi sasa dunia imeingia katika changamoto ya kibiashara kutokana na maradhi ya COVID 19 hivyo kupelekea bidhaa nyingi kuwa adimu huko zinakotoka sambamba na usafirishaji kuongezeka gharama jambo ambalo haliepukiki.

Hata hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba kwa wale wanaopandisha bei kwa makusudi kwa kisingizio cha kwamba Ramadhani inakuja hilo linaepukika.

Hivyo, aliwataka wafanyabiashara watizame maslahi ya watu na badala yake wapunguze faida wanazoziweka ili wananchi waweze kupata bidhaa kwa bei wanazozimudu na isiwe kisingizio kwamba Ramadhani ni wakati wa kupandisha bei za bidhaa.

Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili Waumini wa Dini ya Kiislamu waweze kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa amani na usalama ili kuweza kufutiwa madhambi yao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi (kulia kwa Rais) baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Msitiki wa Amaan Jijini Zanzibar na (kushoto kwa Rais) Sheikh Rajab Mohammed Faki.(Picha na Ikulu).

Kuhusu suala la Uchaguzi uliofanyika hivi karibuni wa Uwakilishi kisiwani Pemba na Udiwani kwa upande wa Unguja, Alhaj Dk. Mwinyi alitoa shukurani na pongezi kutokana na uchaguzi huo kufanyika kwa amani na utulivu mkubwa.

Alisema kuwa walio wengi wameshukuru kwa uchaguzi uliofanyika pande zote mbili kwenda vizuri na matokeo yamepatikana kwa amani na utulivu mkubwa. 

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi walio wengi kutoshawishika na maneno yanayohatarisha amani hapa nchini na badala yake wawapuza wale wanaoashiria uvunjifu wa amani na utulivu.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa hakuna jambo lolote muhimu la maendeleo linaloweza kufanyika katika nchi yoyote duniani bila ya kuwepo kwa amani na utulivu.

Alisema kuwa tayari hapa nchini amani, umoja wa wananchi mambo ambayo yataweza kuleta maendeleo na lililobaki ni watu kuwajibika katika kufanya kazi.

Aliongeza kuwa uongozi wa Awamu ya Nane ambao una miezi minne tu kuwepo madarakani itachukua muda wa kulibadilisha mazoea lakini aliahidi juhudi zitafanyika katika kuhakikisha kila aliepewa dhamana afanye kazi kwa maslahi ya waliowengi.

Alhaj Dk. Miwnyi alisisitiza kwamba ataendelea kuwasimamia ili kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika nafasi yake aliyopewa huku akitumia fursa hiyo kuipongeza Kamati ya Msikiti huo kwa kumpa fursa hiyo ya kutoa salamu zake kwa Waumini mara baada ya sala ya Ijumaa.

Mapema akisoma hotuba ya Sala ya Ijumaa Khatibu wa Msikiti huo Rajab Mohammed Faki alieleza suala zima la amani na umoja mambo ambayo yametiliwa mkazo katika dini ya Uislamu. 

Sambamba na hayo, Khatib huyo alimtaka Alhaj Dk. Mwinyi kuwa na subira kwa kuondokewa na viongozi wenziwe wakuu wa nchi hivi karibuni ambao wote kwa umoja wao walikuwa wakisisitiza suala zima la amani, umoja na mshikamano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news