Rais Samia aagiza mawaziri, wataalamu kutoka Kenya na Tanzania kukutana mara moja


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Aprili 10, 2021 amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta uliowasilishwa na Waziri wa Michezo, Utamaduni na Urithi wa Kenya, Balozi Dkt. Amina Mohamed.

Pamoja na kupokea ujumbe huo Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais Samia amefanya mazungumzo na Mhe. Balozi Amina kuhusiana na dhamira ya Tanzania na Kenya kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano katika nyanja mbalimbali hususani kiuchumi na kijamii.

Rais Samia amemhakikishia Rais Kenyatta kuwa Serikali anayoiongoza ipo tayari kuendeleza mambo mazuri yote yaliyokuwa yakifanywa na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kutatua changamoto kati ya Tanzania na Kenya kwa kuwa nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ndugu, majirani na marafiki wa kihistoria.

Amewataka Mawaziri na Wataalamu wa Tanzania na Kenya wanaounda Kamati ya Ushirikiano wa Pamoja (Joint Permanent Commission – JPC) ambao hawajakutana tangu mwaka 2016 kukutana mara moja ili kufanyia kazi masuala mbalimbali ya kuimarisha uhusiano.

Rais Kenyatta amemwalika Rais Samia kufanya ziara rasmi nchini Kenya ili kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano.

Amemhakikishia Rais Samia kuwa Kenya ipo tayari wakati wote kushirikiana na Tanzania kwa kuendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Amina ameongozana na Balozi wa Kenya hapa nchini, Dan Kazungu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news