SERIKALI YAANZISHA KITUO CHA KIMATAIFA CHA KUENDELEZA VIPAJI VYA MICHEZO

Serikali inatekeleza mradi wa kupanua eneo la Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya ikiwa ni mkakati maalum wa kuanzisha Kituo cha Kuendeleza Vipaji vya Michezo ili kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo hapa nchini, anaripoti John Mapepele (Dodoma).

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo Omary ameyasema haya wakati alipokuwa na Timu ya wataalam walipotembelea na kukagua eneo hilo hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya kufanya maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kitakuwa na hadhi ya kimataifa.
Mkurugenziwa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo Omari (kushoto) akiwa na aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF na Kocha wa Timu ya Taifa Stars, Ami Ninje (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Dkt. Richard Masika wakikagua eneo la chuo kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa chuo hicho ili kujenga Kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo.
Timu ya wataalam mbalimbali wa michezo na ardhi ikipitia ramani ya maeneo ya ujenzi wa madarasa na hosteli.

“Niseme tu kwamba kukamilika kwa kituo hiki kutaifanya nchi yetu kusonga mbele kwenye Sekta ya Michezo kwa kuwa vipaji vya wanamichezo wetu vitaibuliwa na tutaweza sasa kushindana na mataifa mengine duniani sasa” amefafanua Mkurugenzi Omary

Amesema Tanzania ina hazina kubwa ya vipaji kilichokuwa kinakosekana ni kituo maalum cha michezo cha kuwanoa wachezaji na kwamba kukamilika kwa kituo hiki ni suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.

Awali, Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema Wizara imeendelea kufanya mageuzi makubwa ili kutimiza ahadi za Serikali na matarajio ya wananchi kwa ujumla.

Amesema Wizara inatekeleza kwa kwa kasi masuala yote yaliyobainishwa kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 ikiwemo ibara125(a)-(h) kwa Sekta ya Habari, ibara239 (a)-(m) kwa Sekta ya Utamaduni, ibara 249 (a)-(j) Sekta ya Sanaa na ibara 243(a)-(k) kwa Sekta ya Michezo.
Timu ya wataalam ikiangalia eneo la ujenzi wa madarasa wa Kituo cha kuendeleza vipaji vya Michezo

Akihutubia kwenye kikao cha Wafanyakazi wa wa Wizara hiyo hivi karibuni, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema tayari Wizara yake imeshakamilisha agizo la Serikali la kuanzisha Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ikiwa pia ni mkakati wa kukuza sekta ya Michezo nchini.

“Wizara imekamilisha agizo hili kwa kuhuisha Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni ambao umetengewa shilingi bilioni 1.5.

Mfuko huu kwa mwaka ujao wa fedha utajikita katika ujenzi wa miuondombinu muhimu ikiwemo jengo la SANAA HOUSE hapa Dodoma, pia utaendelea kutengewa fedha zaidi kwa lengo la kutekeleza majukumu mawili adhimu; kuwajengea uwezo wanatasnia hizo za Sanaa na Utamaduni kupitia mafunzo na kuwawezesha kupata mikopo na ruzuku katika kazi zao” amesisitiza Waziri Bashungwa

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news