TPDC HAIKAMATIKI MICHUANO YA MEI MOSI 2021, YAICHAPA WIZARA YA KILIMO 2-0

Timu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) maarufu TPDC HEROES imeendeleza rekodi yake ya kugawa dozi katika kila mchezo inayoshuka dimbani, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.

Hatua hii inakuja baada ya TPDC kuwafungisha virago wazee wa Viuatilifu-Wizara ya Kilimo baada ya kuwachabanga mabao 2 bila majibu.

Mabao ya TPDC yamefungwa na mshambuliaji wake hatari Barnabas Mwashambwa (1), huku Captain mwenye kasi zaidi katika michuano hii Dalushi Shija akipachika bao 1.

Kwa matokeo haya, TPDC sasa imetinga hatua ya nusu fainali ambapo anasubiri mshindi kutoka katika mchezo unaofuata. TPDC imetinga hatua hiyo baada ya kufungwa goli 1 katika michezo minne iliyocheza, huku ikipachika jumla ya magoli nane.

Hadi sasa TPDC katika mashindano hayo imecheza Mechi  4 kama ifuatavyo; TPDC Vs Ulinzi 3-0, TPDC Vs Uchukuzi 1-1,TPDC Vs Mambo ya Nje  2-0 na TPDC Vs Kilimo 2-0.

TPDC inajali michezo

Mwishoni mwa mwaka jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC),Dkt.James Mataragio alisema wataendelea kuipa michezo ya aina mbalimbali kipaumbele kwani licha ya michezo kuwa afya pia ni njia ya kulitangaza shirika hilo ambalo lina jukumu kubwa kwa Taifa katika biashara ya kuuza gesi na shughuli za kutafuta mafuta.

Aliyasema hayo baada ya kufika jijini Tanga katika mashindano ya Shimuta ambapo timu za shirika hilo zilifanya vizuri.

Dkt.Mataragio aliyasema hayo wakati akizungumza na wachezaji wa timu za shirika hilo ambazo zilishiriki kwenye michuano ya Shimuta iliyotimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali mjini Tanga ambapo wamekuwa washiriki wazuri kwa miaka mingi.

Alisema kila siku shirika hilo limekuwa na timu ya ushindi ambapo wamekuwa wakifanya hivyo katika mashindano mbalimbali huku.

Pia alisema umahiri huo umesaidia kuleta ushindani kwenye michezo mbalimbali kwa mfano mchezo wa Wavu,Kikapu,Riadhaa,Karata ,Pete na Mpira wa Miguu ambapo wameshiriki kote na kuweza kushinda vikombe vingi na kupata medali, lakini kikubwa zaidi wamejenga afya ya wafanyakazi wao.

“Ushiriki wetu umekuwa na umuhimu kwa sababu michezo ni afya na inaongeza tija kwa hiyo mimi kama Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC nalitambua hilo na ndio maana siku zote nawatia moyo vijana wetu kushiriki kwenye michezo kwa sababu najua michezo inaleta tija,”alisema Dkt.Mataragio mwishoni mwa mwaka jana.

“Lakini kikubwa zaidi sisi kama TPDC ni shirika la Serikali ambalo linafanya biashara ya kuuza gesi na shughuli za kutafuta mafuta hivyo kushiriki kwenye michezo hiyo ni kuitangaza TPDC na shughuli ambazo tunazifanya,"aliongeza.

Alisema kwa sababu wanatumia fedha nyingi kujitangaza, lakini kwa vijana wao kushiriki kwenye michezo hiyo wanatangaza bidhaa zao kwa namna moja au nyingine kwa sababu wanakutana na watu wengi kutokana na michezo ambayo huwakutanisha watu wengi na wanajitangaza na kufahamika wanafanya nini na ni nani.

Kuhusu TPDC

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ni Shirika la Umma lililoanzishwa mwaka 1969 kwa Agizo la Rais Na. 140 chini ya sheria ya Mashirika ya Umma. Shirika lilianzishwa pamoja na mambo mengine kwa ajili ya kulinda maslahi ya Taifa katika shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania linajishughulisha na utafutaji, uchimbaji, uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia pamoja na ujenzi wa miundombinu ya mafuta na gesi na usambazaji kwa wateja.

Majukumu makuu ya Shirika ni pamoja na kukuza uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi na uzalishaji wake;

Kufanya shughuli za utafutaji, uzalishaji, usafishaji, uhifadhi na usambazaji wa mafuta ya petroli;kushiriki katika shughuli za utafutaji wa mafuta;kuwa na hisa kwa makubaliano kwenye kampuni au miradI.

Pia kuendesha na kusimamia shughuli za shirika/kampuni; na kuendesha biashara, shughuli au huduma yeyote ama ndani ya Serikali ya Muungano wa Tanzania au mahali pengine.

Shirika limejenga uwezo katika taaluma mbalimbali na linashiriki katika miradi yote inayohusisha utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi ikiwa na lengo la kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa yanalindwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news