Uongozi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania wateta na Rais Dkt.Mwinyi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amekutana na uongozi wa Chuo Kikuu Huria chini ya Makamu Mkuu wake Profesa Elifas Tozo Bisanda ambapo katika mazungumzo yao, uongozi huo umempongeza Dkt. Mwinyi pamoja na chama chake cha CCM kwa ushindi waliopata katika uchaguzi mkuu uliopita, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Zanzibar).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wahadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania wakiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof.Elifas Tozo Bisanda, walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu.(Picha na Ikulu).

Aidha, uongozi huo umempa pole Rais Dkt.Mwinyi kwa misiba iliyotokea ya Kitaifa ukiwemo msiba wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Hayati Maalim Seif Sharif Hamad.

Pia, uongozi huo umetumia fursa hiyo kumuomba Rais Dkt. Mwinyi kuwapelekea salamu zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kupokea vyema majukumu ya Urais sambamba na kuendeleza amani na utulivu nchini.

Uongozi huo umemueleza Rais Dkt.Mwinyi mafanikio makubwa yaliopatikana tokea kuanzishwa kwa chuo hicho hapa Zanzibar mnamo mwaka 1994 ambapo hadi mwaka wa masomo uliomalizika Juni mwaka uliopita wameweza kudahili wanafunzi wapatao 4,534 hapa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Prof.Elifas Tozo Bisanda alipofika Ikulu jijini Zanzibar na Ujumbe wa Uongozi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (haupo pichani) mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu.(Picha na Ikulu).

Katika mazungumzo hayo Profesa Basinda ameeleza kwamba kati ya wanafunzi hao waliohitimu ni 1,855 sawa na asilimia 41 ya waliodahiliwa ambapo hayo ni mafanikio makubwa kwa Zanzibar kwani katika vyuo huria wanafunzi wanaofanikiwa kuhitimu huwa hawazidi asilimia 25.

Nae Rais Dkt.Mwinyi kwa upande wake ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi huo pamoja na chuo hicho kwa juhudi zake kubwa unazozichukuwa katika kutoa elimu kwa wanafunzi wa Zanzibar ambao wamekwua wakifanya vizuri.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania ukiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Prof.Elifas Tozo Bisanda (kulia kwa Rais) na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe.Simai Mohammed Said na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu.(Picha na Ikulu).

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake na chuo hicho ili kizidi kupata mafanikio.

Post a Comment

0 Comments