WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA MPANGO WA TATU WA MAENDELEO YA TAIFA WA MIAKA MITANO 2021/22-2025/26

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwasilisha bungeni Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, jijini Dodoma.

1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya na kuweza kukutana tena kwa ajili ya kupokea na kujadili kwa mara ya pili na kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 kwa mujibu wa ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kanuni ya 113 ya Kanuni za Kudumu za Bunge. 


Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee na kwa masikito makubwa napenda kutumia fursa hii kutoa pole kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge Wote, Chama cha Mapinduzi pamoja na Watanzania wote kwa kuondokewa na mpendwa wetu, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Msiba huu umekuwa pigo na umeleta majonzi kwa Taifa letu kutokana na uongozi wake mahiri, uchapakazi na uzalengo uliotukuka kwa Taifa. Mwenyezi Mungu ampumzishe mahali pema peponi, Amina. 

Vile vile, napenda kutoa pole kwa Taifa kwa kuondokewa na Viongozi Wakuu, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, na Balozi Mhandisi John Kijazi, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema paponi.
 

Mheshimiwa Spika, kwa dhati naomba kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu,

Aidha, ninampongeza Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Isdori Mpango kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile, napenda kumpongeza Balozi Hussein Katanga na Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wote kwa kuteuliwa kushika nafasi hizo muhimu katika uongozi wa nchi yetu. Kipekee nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuonesha imani yake kwangu na kuniteuwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

I
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Jangómbe, Mhe. Ali Hassan Omar King kuhusu wajibu wa kumlipa mteja anayeibiwa fedha kwenya akaunti ya benki muda mchache kabla ya uwasilishaji wa Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 Р2025/26, bungeni jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akifurahia jambo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba baada ya kuwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, kulia ni baadhi ya viongozi wa Wizara hiyo, bungeni jijini Dodoma. Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WFM.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza na baadhi ya viongozi wa Wizara hiyo baada ya kuwasilisha bungeni Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara wa Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, baada ya kuwasilisha bungeni Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, jijini Dodoma.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa shukrani za dhati kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Eng. Hamad Yussuf Masauni (Mb), na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu, Bw. Emmauel Mpawe Tutuba kwa ushirikiano walionipa katika maandalizi ya kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26. 

Aidha, ninawashukuru sana Wizara, Taasisi, Idara za Serikali, Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeleo, Asasi Zisizo za Kiserekali na wadau mbalimbali waliotoa maoni na michango yao katika kukamilisha Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.
 

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini (CCM) na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi (CCM) kwa maoni yao wakati wa majadiliano ya vikao vya kamati. Aidha, maoni na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti yaliyotelewa katika vikao vya mwezi Januari na Machi 2021 pamoja na mjadala wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipojadili Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 kwa muda wa siku tano (5) kuanzia tarehe 02 Februari, 2021 yamezingatiwa katika uandaaji wa Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.
Mheshimiwa Spika, Serikali imezingatia kikamilifu maoni na ushauri wa Kamati na Bunge katika taarifa niliyowasilisha. Majibu ya hoja zilizoibuliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yameambatishwa (Kiambatisho I).

Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 yameandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025; Mpango Elekezi wa Muda Mrefu 2011/12 – 2025/26; Matokeo ya Tathmini Huru ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21; Sera na Mikakati mbalimbali ya Kisekta; Dira ya Afrika Mashariki 2050; Dira ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika 2050; Ajenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika; na Malengo ya Maendeleo Endelevu, 2030.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 una dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Mpango huu una maeneo makuu matano (5) ya kipaumbele ambayo ni: (i) kuchochea uchumi shindani na shirikishi; (ii) kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; (iii) kukuza uwekezaji na biashara; (iv) kuchochea maendeleo ya watu; na (v) kuendeleza rasilimali watu.

Mheshimiwa Spika, Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kimegawanyika katika sura nane (8): Sura ya kwanza ni Utangulizi ambao unaelezea chimbuko na historia ya Dira ya Maendeleo 2025 na Mipango ya Maendeleo; Sura ya Pili inahusu Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa 2016/17 – 2020/21 ambayo yanajenga msingi wa maandalizi ya Mpango wa Tatu ambao unaendeleza mafanikio yaliyopatikana na kutatua changamoto zilizokabili utekelezaji wa Mpango wa Pili; Sura ya Tatu imejikita katika masuala ya maendeleo ya sekta binafsi ikiwa na msukumo wa kuijenga Sekta Binafsi na kuishirikisha katika utekelezaji wa mpango; Sura ya Nne inaelezea dhana ya kujenga uchumi shindani, maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu; Sura ya Tano inaainisha hatua mahususi za kuchukuliwa katika maeneo ya kipaumbele ya Mpango; Sura ya Sita inahusu ugharamiaji wa utekelezaji wa Mpango; Sura ya Saba inaanisha mpangilio wa utekelezaji wa Mpango; na Sura ya Nane inaainisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha Mpango huu unatekelezwa kikamilifu, Serikali inaendelea na maandalizi ya Mikakati ya Utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ikijumuisha Mkakati wa Utekelezaji, Mkakati wa Ugharamiaji na Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Mpango.

2.0 TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA PILI WA MAENDELEO WA TAIFA WA MIAKA MITANO 2016/17 – 2020/21

2.1 Viashiria vya Uchumi Jumla

Mheshimiwa Spika, Tathmini ya Utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 inaonesha kuwa, katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa Mpango (2016/17 – 2019/20): Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.9; mfumuko wa bei ulikuwa wa wastani wa asilimia 4.1 kwa mwaka ikiwa ni ndani ya lengo la kutozidi asilimia 5; akiba ya fedha za kigeni ilitosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 4.9 ikiwa ni zaidi ya lengo la miezi minne (4); na nakisi ya bajeti ilikuwa ndani ya lengo la kutozidi asilimia 3 kwa kipindi chote. 

Katika kipindi hicho, deni la Serikali lilikuwa himilivu katika muda mfupi, wa kati na mrefu. Vile vile, Pato la Wastani la Kila Mtu liliongezeka kutoka shilingi 2,225,099 (sawa na dola za Marekani

1,022) mwaka 2016 hadi shilingi 2,577,967 (sawa na dola za Marekani 1,080) mwaka 2019. Kielelezo kikuu cha mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ni Tanzania kufanikiwa kuingia katika kundi la nchi zenye uchumi wa kipato cha kati cha chini mwezi Julai 2020.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ulikadiriwa kutumia jumla ya shilingi trilioni 107 ambapo shilingi trilioni 59 ni kutoka sekta ya umma na shilingi trilioni 48 kutoka Sekta Binafsi. Katika miaka minne ya utekelezaji wa mpango huo, sekta ya umma imetumia jumla ya shilingi trilioni 34.9, sawa na asilimia 76.5 ya lengo la miaka minne la shilingi trilioni 45. 

Aidha, sekta binafsi imetumia jumla ya shilingi trilioni 32.6 sawa na asilimia 85 ya lengo la miaka minne la shilingi trilioni 38.4

2.2 Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ulijikita katika kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini hususan za kilimo, madini na gesi asilia. 

Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ni kama ifuatavyo:

(i) Uzalishaji Viwandani: kujengwa kwa jumla ya viwanda vipya 8,477 kati ya mwaka 2015 – 2019 ambapo viwanda vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406 na vidogo sana 4,410. Ujenzi wa viwanda hivyo umeongeza idadi ya viwanda nchini kutoka 52,633 mwaka 2015 hadi viwanda 61,110 mwaka 2019. 

Viwanda hivyo vimechangia ongezeko la uzalishaji wa bidhaa mbalimbali katika soko la ndani na la nje ikijumuisha bidhaa za ngozi, nguo, ujenzi (nondo, mabati, saruji, misumari, marumaru na rangi), plastiki, zana za kilimo na vinywaji.

Uwekezaji huo umeleta mafanikio yafuatayo: Kuongezeka kwa mchango wa Sekta ya Viwanda katika Pato la Taifa kutoka asilimia 7.9 mwaka 2015 hadi asilimia 8.5 mwaka 2019; kukua kwa sekta ya uzalishaji viwandani kwa wastani wa asilimia 8.3; kuzalishwa kwa fursa za ajira kutoka ajira 254,786 mwaka 2015 hadi ajira 482,601 mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 47.2; na kuchangia katika mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi kutoka asilimia 13.8 mwaka 2016/17 hadi asilimia 14.2 mwaka 2019/20. 

Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 45.3 kimetumika kuchochea miradi ya uzalishaji viwandani;

(ii) Kilimo: Baadhi ya shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na: kujengwa na kuboreshwa kwa miundombinu ya umwagiliaji ambayo imeongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,376 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020; kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 36,614 mwaka 2015 hadi tani 76,726 mwaka 2020;

kukamilika kwa ujenzi wa maabara ya mbegu katika makao makuu ya Wakala wa Mbegu za Kilimo – Morogoro; na kuanzishwa kwa soko la bidhaa (Tanzania Mercantile Exchange – TMX).

Hatua hizi zimechangia kupatikana kwa mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kuongezeka kwa utoshelevu wa chakula kufikia asilimia 118 mwaka 2019/20; kupungua kwa mfumuko wa bei za chakula kufikia wastani wa asilimia 5.0 mwaka 2020 kutoka asilimia 8.6 mwaka 2015; na kupungua kwa Umaskini wa Chakula kutoka asilimia 9.7 mwaka 2011/12 hadi asilimia asilimia 8.0 mwaka 2017/18. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 188.9 kimetumika kuendeleza sekta ya kilimo;

(iii) Mifugo: kujenga kiwanda kipya cha Kilimanjaro International Leather Industries Co Ltd; kuimarisha kituo cha Taifa cha Uhimilishaji cha NAIC (Arusha); kujengwa kwa viwanda vipya vya kimkakati vya nyama vya Tanchoice (Pwani), Elia Food Oversees Limited (Arusha) na Binjiang Company Limited (Shinyanga); kujengwa kwa kiwanda cha maziwa cha Galaxy Food and Beverage Company Limited (Arusha); kujengwa kwa kiwanda cha kuzalisha chanjo cha Hester Bioscience Africa Limited (Pwani); na kuendelea kuboresha huduma za malisho ya mifugo na majosho.

Utekelezaji huu umewezesha mafanikio yafuatayo: kuongezeka kwa viwanda vya kusindika nyama nchini kutoka 25 mwaka 2015/16 hadi viwanda 32 mwaka 2019/20 na viwanda vya kusindika maziwa kutoka 82 mwaka 2015/16 hadi 99 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa usambazaji wa mitamba katika mashamba ya Serikali kutoka mitamba 11,449 mwaka 2015/16 hadi mitamba 18,255 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa maeneo ya malisho ya mifugo kutoka hekta milioni 1.4 mwaka 2015/16 hadi hekta milioni 2.85 mwaka 2019/20; na kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na zao la ngozi kutoka shilingi bilioni 1.73 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 9.1 mwaka 2019/20. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 5.66 kimetumika kutekeleza miradi na programu za sekta ya mifugo;

(iv) Uvuvi: Kuimarisha usimamizi wa shughuli za uvuvi kupitia utekelezaji wa Sera ya Uvuvi ya Mwaka 2015, Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009; kutungwa kwa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu Na. 5 ya mwaka 2020; na kupambana na uvuvi haramu kupitia doria na kaguzi mbalimbali. Hatua hizi zilifanikisha: Kuongezeka kwa uzalishaji wa samaki katika maji ya asili kutoka tani 362,645 mwaka 2015/16 hadi tani 497,567 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa usindikaji wa minofu ya samaki aina ya Sangara kutoka tani 23,000.58 mwaka 2015/16 hadi tani 27,596.27 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa huduma za usafirishaji wa mazao ya uvuvi kwenda masoko ya Ulaya ambapo katika mwaka 2019/20, jumla ya tani 777.750 za mabondo zilisafirishwa; kuongezeka kwa mauzo ya samaki na mazao ya uvuvi nje ya nchi kutoka shilingi bilioni 379.25 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 506.24 mwaka 2019/20; na kuanza maandalizi ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na ununuzi wa meli nne (4) za uvuvi. 

Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, jumla ya shilingi bilioni 33.5 zimetumika kwa ajili ya kuendeleza sekta ya uvuvi;

(v) Madini: kupitia na kutunga sheria, sera na mikataba ya madini ambapo imewezesha kuundwa kwa kampuni ya ubia ya Twiga Minerals Corporation ambapo imetoa gawio la shilingi bilioni 100; kuanzishwa kwa kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited; kujengwa kwa masoko 39 ya madini na vituo 41 vya kuuzia madini; kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika maeneo ya Bariadi, Musoma, Bukoba na Handeni na kuendelea na ujenzi wa vituo vya Songea, Mpanda na Chunya; kujenga ukuta wenye mzingo wa kilomita 24 wa Mirerani mkoani Manyara; na kukamilisha ujenzi wa vituo vitatu (3) vya mfano vya uchenjuaji wa madini ya dhahabu kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika maeneo ya Lwamgasa (Geita), Katente (Bukombe) na Itumbi (Chunya).

Hatua hizi zimechangia kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni kutokana na mauzo ya madini kutoka dola za Marekani bilioni 1.91 (sawa na shilingi trilioni 4.46 mwaka 2015/16 hadi dola za Marekani bilioni 2.9 (sawa na shilingi trilioni 6.77) mwaka 2019/20; na kuongezeka kwa maduhuli kutoka shilingi bilioni 196 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 528.3 mwaka 2019/20. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, jumla ya shilingi bilioni 83.4 zimetumika kugharamia miradi mbalimbali ya madini;

(vi) Maliasili na Utalii: kuongeza idadi ya watalii na mapato kupitia Mradi wa Kujenga Uwezo katika Hifadhi za Taifa; kudhibiti ujangili kwa asilimia 90; kubadilishwa na kupandishwa hadhi kwa mapori ya akiba ya Nyerere, Burigi, Kigosi, Ugala, Ibandakyerwa na Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa; na kuendelea kutangazwa kwa vivutio vya utalii katika nchi mbalimbali duniani.

Hatua hizi zimechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii walioingia nchini kutoka watalii 1,137,182 mwaka 2015 hadi 1,527,230 mwaka 2019; kuongezeka kwa wastani wa idadi ya siku zinazotumiwa na watalii kukaa nchini kufikia siku 13 mwaka 2019 kutoka siku 10 mwaka 2015; nakuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii kutoka dola za Marekani bilioni 1.9 (sawa na shilingi bilioni 4,436.7) mwaka 2015 hadi dola za Marekani bilioni 2.6 (sawa na shilingi bilioni 6,071.3) mwaka 2019. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, jumla ya shilingi bilioni 269.7 zimetumika kuboresha na kuendeleza sekta ya Maliasili na Utalii.

2.3 Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miundombinu na upatikanaji wa huduma za afya, maji na elimu, umeongeza kasi ya ufungamanishaji wa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni kama ifuatavyo:

(i) Afya: Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kuendelea kutoa huduma za kupandikiza uloto (bone marrow transplant); kukamilika kwa ujenzi wa jengo la huduma za dharura na ukarabati wa jengo la X-ray katika Hospitali ya Rufaa Dodoma; kukamilika kwa asilimia 98.2 ya ujenzi wa Hospitali ya Uhuru – Dodoma; kununuliwa kwa mashine za digital X-ray na ultrasound, vifaa vya maabara na mashine za uchunguzi wa kifua kikuu kwa kuotesha vimelea BACTEC 960 (Mycobacteria Growth Indicator Tube – MGIT) na Blood culture machine katika Hospitali ya Rufaa ya Magonjwa ya Kifua Kikuu –

Kibong’oto; ununuzi wa mashine ya Positron Emmission Tomography (PET Scan) kwa ajili ya Hospitali ya Ocean Road; kujenga na kuboresha miundombinu ikijumuisha: jengo la huduma za upasuaji; radiolojia; jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje; maabara; na jengo la mama na mtoto katika hospitali za rufaa za Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure (Mwanza), na hospitali za rufaa za kanda ya kusini Mtwara na kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya na Hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na Hospitali ya Kanda ya Ziwa ya Burigi (Geita).

Vile vile, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya sekta ya afya ambayo imefikia hatua mbalimbali ikiwemo: kufikia asilimia 98 ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Mwananyamala; kukamilika na kuanza kutumika kwa jengo la wagonjwa wa nje na kufikia asilimia 73 ya ujenzi wa jengo la maabara katika Hospitali ya Rufaa Njombe; na ujenzi wa jengo la ghorofa moja la huduma za upasuaji, radiolojia na maabara na kufikia asilimia 50 ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Simiyu. 

Aidhaa, mafanikio mengine ni pamoja na: ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi; na kuongezeka kwa idadi ya zahanati kutoka 4,922 mwaka 2015 hadi 6,120 mwaka 2020, vituo vya afya kutoka 535 mwaka 2015 hadi kufikia vituo 710 mwaka 2020 na Hospitali za Halmashauri za Wilaya kutoka 77 mwaka 2015 hadi 179 mwaka 2020.

Hatua hizi zimechangia: Kuongezeka kwa wastani wa umri wa kuishi kutoka miaka 62 mwaka 2015/16 hadi miaka 66 mwaka 2019/20; kupungua kwa idadi ya vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kutoka wastani wa vifo 67 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2014/15 hadi wastani wa vifo 50.3 mwaka 2019/20; kupungua kwa vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua kutoka vifo 432 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 hadi vifo 321 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2019/20; na kuongezeka kwa watoto wanaozaliwa kwa kuhudumiwa na wahudumu wa afya wenye ujuzi kutoka asilimia 51 mwaka 2015/16 hadi asilimia 80 mwaka 2019/20. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 736.67 kimetumika katika utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za afya;

(ii) Elimu: Ujenzi wa miundombinu muhimu katika shule 3,904 (Msingi 3,021 na Sekondari 883), mabweni 547, nyumba za walimu 101, majengo ya utawala 25 na maktaba 43; kukamilika kwa ujenzi wa maboma 2,815 katika shule za msingi 2,133; kuendelea kugharamia elimu msingi bila ada ambapo shilingi trilioni 1.24 zilitolewa;

kukarabatiwa kwa shule kongwe 84 kati ya 89; kuboreshwa kwa miundombinu ya vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi (Folk Development Colleges – FDC); na kutolewa kwa mikopo ya elimu ya juu ya jumla ya shilingi trilioni 2.29.

Hatua hizi zimechangia: Kuongezeka kwa kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya msingi kutoka asilimia 93.3 mwaka 2015 hadi asilimia 110.6 mwaka 2020; kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya ufundi stadi kutoka 196,091 mwaka 2015/16 hadi 320,143 mwaka 2019/20 na elimu ya ufundi kutoka 117,067 mwaka 2015/16 hadi 151,379 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu nchini kutoka 65,064 mwaka 2015/16 hadi kufikia 87,813 mwaka 2019/20; na kuongezeka kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kutoka wanafunzi 125,126 mwaka 2015 hadi kufikia 132,392 mwaka 2020. Aidha, kiwango cha ufaulu wa mitihani ya Darasa la Saba kimeongezeka kutoka asilimia 67 mwaka 2015 hadi asilimia 81.5 mwaka 2019 na Sekondari (Kidato cha nne) kutoka asilimia 68 mwaka 2015 hadi asilimia 80.7 mwaka 2019. Vile vile, wanafunzi waliohitimu elimu ya juu walifikia 60,940 mwaka 2019/20, elimu ya mafunzo stadi 90,849 mwaka 2018/19 na elimu ya ufundi 86,547 mwaka 2019/20. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi trilioni 3.19 kimetumika kuboresha miundombinu na huduma za sekta ya elimu;

(iii) Maji: Kukamilika kwa miradi 1,845 ya maji iliyotekelezwa mijini na vijijini. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa na hatua zilizofikiwa ni: kukamilika kwa miradi ya maji katika miji ya Geita, Njombe na Songwe na kuendelea kwa ujenzi wa mradi wa maji katika mji wa Kigoma (asilimia 90); kukamilika na kuzinduliwa kwa Mradi mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega; kukamilika kwa asilimia 76 ya ujenzi wa mradi wa maji katika Jiji la Mwanza; kukamilika kwa asilimia 62 ya ujenzi wa mradi wa maji katika Jiji la Arusha; na kuendelea na ujenzi wa mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 65. Aidha, katika eneo linalohudumiwa na DAWASA (mikoa ya Dar es Salaam na Pwani) utekelezaji wa miradi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na umehusisha maeneo ya Kibamba hadi Kisarawe, Mlandizi hadi Chalinze, Kisarawe-Pugu Ukonga, Mbezi Luis, Kiluvya, Tegeta, Wazo, Madale, Mivumoni, Mabwepande na Bagamoyo (maeneo ya Vikawe, Zinga, Mapinga na Kerege).

Kwa ujumla miradi yote iliyotekelezwa imewezesha wananchi zaidi ya milioni 25 kupata huduma ya maji ambapo wastani wa idadi ya watu wanaopata huduma ya maji safi na salama imeongezeka kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 84 mwaka 2020 kwa mijini na kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi asilimia 70.1 mwaka 2020 kwa vijijini. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi trilioni 2.03 kimetumika kuboresha huduma ya maji vijijini na mijini; (iv) Utawala Bora: kukamilika kwa ujenzi wa ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi – Dodoma; Mahakama Kuu mbili (2) katika mikoa ya Mara na Kigoma na ukarabati wa Mahakama Kuu tatu (3) katika mikoa ya Mbeya, Tanga na Rukwa; Mahakama za Hakimu Mkazi tano (5) katika mikoa ya Pwani, Geita, Simiyu, Manyara na Njombe; Mahakama za Wilaya 15; Mahakama za Mwanzo 18; na kuanzishwa kwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Hatua hizi zimechangia kuongezeka kwa idadi ya kesi za rushwa zilizotolewa maamuzi kutoka asilimia 10.4 mwaka 2015/16 hadi asilimia 82.0 mwaka 2019/20; kupungua kwa mlundikano wa mashauri katika mahakama ya Tanzania kutoka asilimia 13 ya mashauri yaliyokuwepo mahakamani mwaka 2015 hadi asilimia tano (5) mwaka 2019; na

kuongezeka kwa upatikanaji wa haki karibu na wananchi; uwiano wa halmashauri zilizobandika bajeti kwenye mbao za matangazo za umma ulifikia asilimia 86 ya lengo la halmashauri zote; kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 bila kutegemea misaada kutoka nje ya nchi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 268.5 kilitumika; na kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 530.8 kilitumika kutekeleza miradi hii; na

(v) Ajira: Jumla ya ajira 12,773,126 zimezalishwa, ambapo ajira za moja kwa moja ni 11,891,772 na ajira zisizo za moja kwa moja ni 881,354. Aidha, jumla ya vijana 65,008 katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2020 wamepatiwa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi ikiwemo mafunzo ya uanagenzi katika fani za ujenzi, useremala, umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa jua, ufundi magari, ufundi bomba, utengenezaji wa vifaa vya aluminium, uchomeleaji na uungaji vyuma, kilimo na ufugaji, ushonaji, uchorongaji vipuli, uchapaji nyaraka na TEHAMA. Serikali imeendelea kulinda ajira za wazawa kwa kuhakikisha kuwa wageni wanaokuja kufanya kazi nchini wanakidhi vigezo vilivyoainishwa katika Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Na. 1 ya mwaka 2015.

2.4 Mazingira Wezeshi kwa Uwekezaji na Uendeshaji Biashara
Mheshimiwa Spika, baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika eneo hili ni kama ifuatavyo:

(i) Nishati ya Umeme: Kuendelea na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere MW 2,115 ambapo kwa ujumla utekelezaji umefikia asilimia 30.1. Kiasi cha shilingi trilioni 1.97 kimetumika kutekeleza mradi huu.

Hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi mingine ni: Kukamilika kwa miradi ya Kinyerezi I MW 150 na II MW 240, mradi wa njia ya kusafirisha umeme kV 220 kutoka Makambako hadi Songea, ujenzi na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme na njia za kusafirisha umeme katika Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 220 Bulyanhulu – Geita; kukamilika kwa asilimia 73.3 ya utekelezaji wa mradi wa Kufua Umeme – Rusumo MW 80; kukamilika kwa asilimia 86 kwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 Singida – Arusha – Namanga; kuendelea na utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi I Extension MW 185 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 84; kukamilika kwa usanifu wa miradi ya Kakono MW 87 na Malagarasi MW 45; kuendelea na kuhuisha upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya Kufua Umeme wa Maji ya Ruhudji MW 358 na Rumakali MW 222; na kukamilika kwa upembuzi yakinifu na kuendelea na uthamini wa mali za wananchi watakaopisha mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Dodoma na Chalinze – Kinyerezi.

Miradi iliyokamilika imechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa nishati ya umeme kufikia MW 1,602.3 mwaka 2019/20 kutoka MW 1,308 mwaka 2015/16; kupungua kwa kiwango cha upotevu wa umeme kutoka asilimia 19.0 mwaka 2015/16 hadi asilimia 16.4 mwaka 2019/20; na kuunganishwa umeme kwa jumla ya vijiji 10,018 kati ya vijiji 12,317 hadi Januari 2020, sawa na asilimia 81.3. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi trilioni 2.98 kimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme;

14

(ii) Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: Kujengwa kwa mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita 3,537 (barabara kuu na za mikoa kilomita 2,209 na barabara za halmashauri kilomita 1,328) na hivyo kufanya mtandao wa barabara uliojengwa kwa kiwango cha lami hadi mwaka 2019/20 kufikia kilomita 13,044 ambapo kilomita 10,939 ni barabara kuu na kilomita 2,105 ni barabara za mikoa. Vile vile, kukamilika kwa ujenzi wa madaraja 13 katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili. Kiasi cha shilingi trilioni 8.8 kimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara na madaraja makubwa katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo.

(iii) Reli: Serikali inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kati ya kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railways – SGR) ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 90 na kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) umefikia asilimia 52.2; kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa kipande cha Mwanza – Isaka (km 341) wenye thamani ya shilingi trilioni 3.07 na kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya Makutupora – Tabora (km 294) na Tabora – Isaka (km 133). Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi trilioni 4.04 kimetumika kutekeleza mradi.

Aidha, ukarabati wa miundombinu ya reli ya kati kutoka Dar es Salaam – Isaka (km 970) sehemu ya Dar es Salaam – Kilosa (km 283) na Kilosa – Isaka (km 687) umekamilika. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 728.3 kimetumika kukarabati miundombinu ya reli ya kati.

Shughuli nyingine zilizofanyika ni pamoja na: kukarabati na kurejesha huduma za reli ya Tanga hadi Arusha (km 439); na kurejesha huduma ya kusafirisha shehena za mizigo kwa njia ya reli kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Uganda.

(iv) Bandari: Katika Bandari ya Dar es Salaam shughuli zilizofanyika ni: Kuboreshwa kwa gati namba 1 – 5; kukamilika kwa ujenzi wa gati la kupakia na kushushia magari (RoRo); na kuendelea na uboreshaji wa gati Na. 6 hadi 7. Hatua hizi zimechangia kupungua kwa idadi ya siku za meli kukaa bandarini kutoka siku saba (7) hadi siku tano (5) na kuongezeka kwa shehena ya mizigo iliyohudumiwa kutoka tani milioni 15.4 hadi tani milioni 19.52. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 253.7 kimetumika kutekeleza mradi huu.

Katika Bandari ya Mtwara, ujenzi wa gati jipya lenye urefu wa mita 300 na yadi ya kuhudumia makasha umekamilika. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 88.6 kimetumika kutekeleza mradi huu.

Mafanikio yaliyopatikana katika Bandari ya Tanga ni uongezaji wa kina cha lango la kuingia meli kutoka mita nne (4) hadi mita 13 na kuweka vifaa vya kuongezea meli; na kukamilika kwa ujenzi wa gati mbili (2) kwenye kina kirefu. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 86.9 kimetumika kutekeleza mradi huu.

(i) Kuboresha Usafiri wa Abiria na Mizigo katika Maziwa Makuu: Ziwa Victoria na Tanganyika: Kukamilika kwa ukarabati wa meli mbili (2) za New Butiama Hapa Kazi Tu na New Victoria Hapa Kazi Tu; kuendelea na ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa kazi Tu ambapo utekelezaji umefikia asilimia 35; na kukamilika kwa ujenzi wa Chelezo cha kujengea na kukarabati meli katika Bandari ya Mwanza chenye uwezo wa kubeba meli yenye uzito wa kuanzia tani 1 hadi 4,000, kikiwa na reli na mfumo unaowezesha kupandisha meli zaidi ya moja kulingana na ukubwa. Shughuli nyingine zilizokamilika ni: ukarabati wa meli za MV. Clarias na ML. Wimbi; Ujenzi wa magati ya Lushamba, Ntama, Nyamirembe, Magarine na Gati la majahazi Mwigobero; na ununuzi wa vifaa vya kuhudumia mizigo na meli.

Katika Ziwa Tanganyika, mikataba kwa ajili ya Ujenzi wa Meli Mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 imesainiwa pamoja na ukarabati wa meli ya MV Liemba; na ukarabati wa meli ya MT. Sangara. Katika katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 148.0 kimetumika kuboresha na kuendeleza hali ya usafiri katika Ziwa Victoria na Tanganyika.

Ziwa Nyasa: Kukamilika kwa ujenzi wa matishari mawili (2) yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja; na kukamilika na kuanza kufanya kazi kwa meli moja mpya ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 17.5 kimetumika kuboresha na kuendeleza hali ya usafiri na usafirishaji katika Ziwa Nyasa;

(v) Viwanja vya Ndege na Rada: Baadhi ya shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na kukamilika kwa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere – JNIA chenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka; na kuendelea na ujenzi wa viwanja vya Geita (asilimia 98), Songea (asilimia 95) na Mtwara (asilimia 53.2). Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 411.2 kimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya viwanja vya ndege.

Kununuliwa kwa rada nne (4) za kuongoza ndege za kiraia na kufungwa katika viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Songwe na Mwanza na hivyo kuongeza kiwango cha usalama wa abiria na mizigo katika viwanja vya ndani. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 79.8 kimetumika kuimarisha usafiri wa anga nchini;

(vi) Uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL): Baadhi ya mafanikio ni pamoja na kununuliwa kwa ndege mpya 11 kutoka ndege moja (1) iliyokuwepo mwaka 2015 na kuifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 12; na kuimarishwa kwa Shirika la Ndege Tanzania. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi trilioni 1.27 kimetumika kutekeleza mradi;

(vii) Mawasiliano na Uchumi wa Kidigitali: Ujenzi wa mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaendelea ambapo awamu ya tatu ya ujenzi imekamilika; Mradi wa mfumo wa Anuani za Makazi na Postikodi unaendelea kutekelezwa; na ufungaji wa nguzo zenye majina ya barabara umefanyika katika halmashauri 12 za majiji ya Dodoma, Mwanza na Tanga.

Uwekezaji huu umechangia kuongezeka kwa idadi ya laini za simu kutoka milioni 39 hadi milioni 48.6; idadi ya watumiaji wa mitandao ya simu kuongezeka kutoka milioni 9 hadi milioni 27 na kupungua kwa gharama za kupiga simu za mkononi kutoka shilingi 274 kwa dakika kwa mwaka 2015 hadi shilingi 70 kwa dakika mwaka 2020. Aidha, huduma za mawasiliano kwa njia ya simu za viganjani zimeenda sanjari na ongezeko la huduma jumuishi za fedha (financial inclusion), na biashara mtandao (e-commerce). Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 874 kimetumika kutekeleza miradi hii; na

(viii) Serikali Mtandao na Mifumo ya Kielektroniki: Huduma za Serikali Mtandao zimeimarishwa kwa kuongeza kiwango cha ubora wa huduma zinazotolewa na Serikali kwa wadau mbalimbali ambapo mifumo ya Serikali mtandao imeongezewa mawanda.

Hatua hizi zimechangia mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za miamala, hususan utunzaji wa kumbukumbu za wateja utoaji wa ankara, kupunguza matumizi ya shajala kurahisisha malipo ya ada, tozo na kodi. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 1.4 kimetumika kuboresha Serikali Mtandao na mifumo ya kielektroniki.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ulikabiliwa na changamoto mbalimbali kama ifuatavyo: Uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mafuriko; kupungua kwa shughuli za kibiashara duniani kulikotokana na athari za COVID-19; na ukwepaji kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu hususan kupitia njia za magendo, uhamishaji wa faida (transfer pricing) kwa kampuni zenye mtandao wa kimataifa na kutokutoa na kudai stakabadhi za kielektroniki (EFD receipt) wakati mauzo yanapofanyika.
Mheshimiwa Spika, Hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na: kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko pamoja na kuimarisha ukaguzi wake; kuendelea kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa biashara duniani ili kutumia fursa zilizotokana na athari za COVID-19 kwa manufaa mapana ya nchi pamoja na kuchukua hatua za kisera na kiutawala kurejesha biashara zilizoathirika; na kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa mapato ili kudhibiti ukwepaji kodi pamoja na kuendelea kuhamasisha umma juu ya matumizi ya stakabadhi za kielektroniki.

3.0 MAPENDEKEZO YA MPANGO WA TATU WA MAENDELEO WA TAIFA WA MIAKA MITANO 2021/22 – 2025/26
Mheshimiwa Spika, misingi iliyozingatiwa ni pamoja na: Kuendelea kuwepo kwa amani, usalama, umoja, utulivu wa ndani na nchi jirani; Kuhimili athari za majanga ya asili kama vile mafuriko na magonjwa ya mlipuko; Ushiriki mpana wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi; Hali nzuri ya hewa itakayowezesha uzalishaji wa chakula cha ziada; na Kuimarika kwa uchumi wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, Shabaha za Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ni pamoja na:

(i) Kiwango cha ukuaji wa uchumi kwa mwaka kuongezeka kutoka asilimia 6.0 mwaka 2021 na kufikia wastani wa asilimia 8.0 ifikapo mwaka 2026;


(ii) Mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri kuongezeka kutoka asilimia 15.9 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 hadi asilimia 16.8 mwaka 2025/26;

(iii) Mfumuko wa bei kuendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 – 5.0 katika kipindi cha muda wa kati;

(iv) Akiba ya fedha za kigeni kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne; na

(v) Sekta binafsi kuzalisha ajira mpya zipatazo milioni nane kati ya Julai 2021 na Juni 2026.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali, Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano yana maeneo makuu matano (5) ya kipaumbele. Maeneo hayo ni kama ifuatavyo:

(i) Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi: Eneo hili linajumuisha miradi ambayo itajikita katika: kujenga jamii yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa; kuchochea utulivu wa viashiria vya uchumi jumla; kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji; kuchochea uvumbuzi na uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje; na kuendeleza miundombinu na huduma za reli, barabara, madaraja, usafiri wa majini na angani, TEHAMA, nishati, bandari na viwanja vya ndege;

(ii) Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na Utoaji Huduma: Eneo hili linajumuisha miradi ya viwanda inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuzalisha bidhaa zitakazotumia malighafi na rasilimali zinazopatikana nchini. Aidha, eneo hili linajumuisha pia miradi na programu inayolenga kuboresha huduma za utalii, fedha na bima;

(iii) Kukuza Uwekezaji na Biashara: Eneo hili linajumuisha programu zitakazoimarisha masoko ya ndani na kutumia fursa za masoko ya kikanda na kimataifa katika kukuza biashara. Aidha, masoko yanayolengwa ni yale yatakayotoa fursa kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, ikiwemo bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu;

(iv) Kuchochea Maendeleo ya Watu: Eneo hili linajumuisha utekelezaji wa miradi ambayo inajikita katika kuboresha maisha ya watu ikiwemo: elimu na mafunzo kwa ujumla; afya na ustawi wa jamii; kinga ya jamii; huduma za maji na usafi wa mazingira; mipango miji, nyumba na maendeleo ya makazi; na athari dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi; na

(v) Kuendeleza Rasilimali Watu: Eneo hili linajumuisha programu na mikakati inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasimali watu nchini, kuanzia ngazi za elimu ya awali hadi elimu ya juu ikiwemo kuwawezesha vijana kujiajiri. Vile vile, eneo hili linajumuisha hatua za kuboresha viwango vya utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ujuzi adimu kwa lengo la kuongeza tija na ushindani wa wananchi katika kutumia rasimali zilizopo nchini ili kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Spika, vile vile, Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 yatajumuisha utekelezaji wa miradi ya kielelezo. Miradi hiyo ni: Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge); Makaa ya Mawe – Mchuchuma na Chuma – Liganga ikijumuisha ujenzi wa reli ya kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway – SGR) kutoka Mtwara hadi Mbambabay na matawi ya Mchuchuma na Liganga; Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania); Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji –

Ruhudji MW 358; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Rumakali MW 222; Uchimbaji wa madini ya Nickel; Ujenzi wa Madaraja Makubwa na Barabara za Juu za Daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza), Tanzanite (Dar es Salaam) na Interchange ya Kamata (Dar es Salaam); Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na Ununuzi wa Meli za Uvuvi; Kiwanda cha Sukari Mkulazi; Utafutaji wa mafuta katika vitalu vya Eyasi Wembere na Mnazi Bay North; Mradi wa Magadi Soda – Engaruka; Kuongeza Rasilimali Watu yenye Ujuzi Adimu na Maalum (Ujuzi wa Kati na Wabobezi) kwa Maendeleo ya Viwanda na Ustawi wa Jamii; na Kanda Maalum za Kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mchango na umuhimu wa sekta binafsi, Mpango huu umeipa sekta binafsi uzito mkubwa. Mpango unalenga kujenga mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukua lakini pia Mpango unalenga kushirikisha sekta binafsi katika ugharamiaji na utekelezaji wa Mpango.
Mheshimiwa Spika, Mpango unakadiriwa kugharimu jumla ya shilingi trilioni 114.8, zikijumuisha mchango wa sekta binafsi wa shilingi trilioni 40.6 na sekta ya umma shilingi trilioni 74.2 kutoka vyanzo vya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, misaada na mikopo. Aidha, vyanzo mbalimbali bunifu vinavyoweza kutumika katika kugharamia shughuli za maendeleo vimeanishwa vikiwemo Ugharamiaji wa Pamoja (joint venture), Hati Fungani za Mashirika, Mitaji Binafsi (private equity) na Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mgawanyo wa majukumu ya utekelezaji wa Mpango, Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zitawajabika kutafsiri Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano katika mipango yao ya kila mwaka na kuwasilisha taarifa za utekelezaji Wizara ya Fedha na Mipango. Aidha, Baraza la Taifa la Biashara litaratibu na kusimamia ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa Mpango. Vile vile, Washirika wa Maendeleo watahamasishwa kushiriki katika utekelezaji wa Mpango kupitia vikao rasmi vya ushirikiano.
Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, Serikali itaweka mfumo thabiti wa Ufuatiliaji na Tathmini ambao ni msingi mkuu wa usimamizi wa utendaji. Lengo la Serikali ni kuhakikisha mapato yanatumika kwa ufanisi na hatimae miradi kuwa na thamani halisi ya fedha, uwajibikaji na uwazi katika hatua zote za maendeleo.

4.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 yatawezesha nchi kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo ni: maisha bora na mazuri; amani, utulivu na umoja; utawala na uongozi bora; jamii iliyoelimika na inayopenda kujifunza; na uchumi wenye uwezo wa ushindani. Aidha, Mpango huu unaweka msingi wa maandalizi ya Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako lipokee na kujadili Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

Post a Comment

0 Comments