CCM Taifa yaomboleza kifo cha Balozi Abbas Kleist Sykes

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan amepokea kwa masikitiko, huzuni na majonzi taarifa ya kifo cha Mwanasiasa mkongwe na Kiongozi, Balozi Abbas Kleist Sykes.

"Ni msiba mkubwa kumpoteza Kiongozi, ambaye licha ya kuwa kijana enzi za kuasisiwa na kuundwa kwa TANU, alishiriki, alishuhudia na aliunga mkono harakati za kupigania Uhuru wa Nchi yetu uliopatikana Disemba 9 mwaka 1961" - amesema Ndugu Samia Suluhu Hassan.

Balozi Abbas aliyatumia maisha yake ya ujana katika kuijenga TANU, akiwa pamoja na Kaka zake Hayati Abdulwahid Sykes aliyewahi kuwa Rais wa TAA na Marehemu Ally Sykes aliyekuwa Mweka hazina wa Chama hicho.

Msingi uliowekwa na TAA mwaka 1929 ndio ulitumika kuanzisha TANU Julai 7 mwaka 1954 chini ya uongozi wa Rais wa kwanza wa TANU Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na baadae kuungana na ASP ya Zanzibar kuunda CCM mnamo Februari 5 Mwaka 1977.

Balozi Abbas Sykes ambae alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kwanza wa Dar es salaam, ametumikia Taifa akiwa Balozi katika Mataifa ya Canada, Ufaransa, Ubelgiji, Sudan Marekani, Mexico Hispania, Ureno, Morocco, Tunisia na Jamhuri ya Demokrasia ya Saharawi. Kazi aliyoifanya kwa uzalendo, uaminifu na uadilifu mkubwa. Pia, amekuwa Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika Shirika la Elimu na Utamaduni (UNESCO).
Chama Cha Mapinduzi kinatoa pole kwa familia ya Marehemu, Ndugu, Jamaa, Marafiki na Wananchi wote kwa msiba huu.

Mwenyezi Mungu mtukufu kwa uweza wake amlaze mahali pema peponi Balozi Abbas Kleist Sykes.
Hakika Sisi ni wa MwenyeziMungu na Kwake ni Marejeo Yetu.

Imetolewa na:


Shaka Hamdu Shaka
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
16 Mei 2021

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news