HOTUBA YA TAASISI ZA KIHABARI KATIKA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI (WPFD) ILIYOADHIMISHWA KITAIFA MEI 3, 2021 JIJINI ARUSHA, TANZANIA

Mhe. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa;

Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Mhe. Iddi Hassan Kimata;

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari;Mhe.Eng.Kundo Andrea Mathew;

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Peter Mutuku Mathuki;Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Anders Sjoberg;

Mwakilishi Mkazi wa Unesco nchini Tanzania, Mhe. Titso Dos Santos;

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Legal Service Facility, Lulu Ng’wanakilala;

Wawakilishi wa Jumuiya ya Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT);

Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwaAfrika Tawi la Tanzania (MISA-Tan), Salome Kitomari;

Mwenyekiti wa Mtandao wa Radio za kijamii Tanzania (TADIO) Prosper Kwigize;

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben;

Wawakilishi wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF)Mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT);

Wawakiliishi wa Umoja wa Club za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)Mwenyekiti wa Arusha Press Club, Claud Gwandu;

Wahariri na Waandishi wa habari;Mabibi na Mabwana,

Mheshimiwa mgeni Rasmi, kwanza tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai, na ni kwa neema zake kuwa leo tuko hapa kufanya shughuli hii muhimu ya kukumbushana utendaji wa vyombo vyabari nchini na duniani, ambapo hatimaye tutaimarisha ushirikiano kati ya dola, jamii na vyombo vya habari kwa masilahi mapana ya maendeleo ya taifa letu.

Nakushukuru kwa kukubali mwaliko wetu, kwani kwa kufanya hivi Mhe. Waziri unadhihirisha kwa matendo kauli ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati akiwaapisha makatibu wakuu kwamba serikali chini ya uongozi wake itaendelea kuenzi uhuru wa habari.

KUMKUMBUKA RAIS MAGUFULI NA WANAHABARI WALIOFARIKI DUNIA MWAKA 2020

Ndugu Mgeni rasmi,Kabla hatujaendelea, sote tunayo kumbukumbukuwa Tanzania ilipata janga la kuondokewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dk. John Pombe Magufuli, aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Pamoja na Rais Magufuli, kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ) katika mwaka tulioumaliza wa 2020, jumla ya waandishi 66 wameuawa ikilinganishwa na waandishili 49 waliouawa kwa mwaka 2019.

Hizi ni taarifa mbaya kwani mauaji ya waandishi duniani yanaongezeka kwa sasa.

Nchi ambazo ni hatari kwa mauaji ya waandishi ni Mexico (14), Afghanistan (10), Pakistan (9), India (8), Philippines (4) na Syria (4).

Kwa heshima ya Rais Magufuli aliyefariki dunia na waandishi wenzetu 66 waliouawa, naomba tusimame dakika moja kuwakumbuka..... Raha ya Milele uwape Ee Bwana, (na Mwanga wa Milele uwaangazie), Wapumzike kwa Amani (Amina).

SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI

Mhe. Mgeni rasmi, leo ni siku ya maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari. Kauli mbiu ya mwaka huu ni“Habari kwa Manufaa yaUmma” (Information as a Public Good). Siku hii inaadhimishwa kidunia katika Jiji la Windhoek, nchini Namibia. Kwa Tanzania, kitaifa inaadhimishwa hapa jijini Arusha.

Mwaka jana hatukuweza kuwa na maadhimisho ya aina hii (kwa maana ya kukutanika pamoja) kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona.

Mhe. Mgeni rasmi, naomba kutumia fursa hii kuwapongeza waandishi wa habari wote nchini wanaofanya kazi hii ngumu ya kukusanya, kuchakata na kuchapisha habari na taarifa kwa nia ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha.

Hongereni sana kwa siku hii muhimu katika historia ya uandishi wa habari nchini na duniani kwa ujumla.

Kila Mei 3, waandishi wa habari duniani kote huadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari; Siku hii inaadhimishwa kwa nia ya kupitia kiwango cha uhuru wa vyombo vya habari duniani, kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kutoa heshima kwa waandishi waliouawa wakiwa kazini.Mhe. Mgeni rasmi, Mwaka 1993, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) ulipitisha azimio la Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, kutokana na Mapendekezo ya Mkutano wa 26 wa UNESCO uliofanyika mwaka 1991.

UNESCO ilitoa maazimio hayo, baada ya Waadishi wa Magazeti barani Afrika kuwa wamekutana jijini Windhoek, Namibia, mwaka 1991 na kutoa azimio hili. Mwaka huu azimio la Windhoek limetimiza miaka 30.

Kwa maana hiyo maadhimisho ya mwaka huu hapa nchini pamoja na yale yanayofanyika katika ngazi ya Jumuiya za kikanda na kwingineko duniani, yanatumika kufanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya Windhoek.

KAULI MBIU YA MWAKA HUU

Mhe. Waziri, Kaulimbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari Vyombo vya Habari ni“Habari kwa Manufaa ya Umma” (Information as a public good).

Kaulimbiu hii inaturejesha kutafakari iwapo mazingira yetu ya kikazi na uhusiano baina ya vyombo vya Habari na serikali, vinawezesha kufikiwa kwa lengo hili muhimu; yaanimanufaa ya umma. Wakati tunapoadhimisha siku hii, tunauona umuhimu wa kuwapo kwa ushirikiano baina ya pande zetu mbili kwa lengo la kuhakikisha kwamba utumishi wetu unakuwa wa thamani mbele ya umma tunaoutumikia.

HALI YA UHURU WA HABARI NCHINI TANZANIA

Mheshimiwa Waziri, kwa nyakati tofauti taasisi zetu za kihabari zimekutana mara kadhaa kujadili uhuru wa vyombo vya habari kwa dhana pana ya uhuru wa wananchi kutoa mawazo yao (freedom of expression).

Mwelekeo wa Tanzania katika Uhuru wa Habari, umekuwa si wa kujivunia. Katika ngazi ya Kimataifa tukiangalia taarifa ya“Waandishi Wasio na Mipaka” (Reporters Without Boarders Report)inaonyesha kwa miaka mitano mfululilizo Tanzania imekuwa na anguko la Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Wakati Mwaka 2016 Tanzania ilikuwa nafasi ya 71 kati ya nchi 180 kwa Uhuru wa Vyombo vya Habari, mwelekeo umekuwa ni wa kushuka kwa kuelekea kusiko.

Mwaka 2017, nchi yetu ilishuka na kuwa ya 83, mwaka 2018 ikwa ya 93, Mwaka 2019, ikawa ya 118 na Mwaka 2020, ikawa ya 124.

Hili ni anguko la nafasi 53, ambalo si la kujivunia.Mhe. Mgeni rasmi, matukio yanayotuangusha ni pamoja na kufungia magazeti, waandishi kupigwa, redio kutozwa faini kiholela, mitandao ya kijamii kufungiwa, kesi zinazotokana na uchapishaji wa habari kufunguliwa kama jinai badala ya madai, watu kufikishwa mahakamani kwa kutoa maoni yao mtandao na mengine mengi yaaina hiyo au yanayofanana na hayo.Mfano halisi ni tukio la Aprili 21, mwaka huu, ambapo Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Jesse Mikofu alipigwa na kuharibiwa simu yake aliyoitumia kupicha picha askari wa JKU Zanzibar, waliokuwa wanahamisha wafanyabiashara ndogo ndogo kutoka eneo la Darajani kwenda Kibandamaiti, Visiwani Zanzibar.

Tunaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua ilizochukua ikiwamo kufanya Mkutano na Waandishi wa Habari kupinga udhalimu huu, kwenda ofisi za Mwananchi Zanzibar kumpa pole na kumwomba radhi mwandishi aliyepigwa na kuwachukulia hatua askari husika.

Tunasema asante sana SMZ.Pamoja na tukio hilo la Zanzibar, katika Manispaa ya Temeke -Dar es Salaam aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Lusubilo J. 5Mwakabibi, mara kadhaa amekamata waandishi na kuwaweka ndani. Tukio la karibuni liliwahusisha waandishi wa Habari wa ITV/Radio One na Island TV ambao aliwakamata na kuwaweka ndanikwa saa kadhaa.

Tunaishukuru Serikali imemsimamisha kazi kupisha uchunguzi wa matumizi mabaya ya madaraka.Pia yapo matukio mengine kama lile la Mwandishi wa Gazeti la Nipashe mkoani Kilimanjaro, Mary Moshakutishwa na wapambe wa Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Rahib, kutokana na habari aliyoandikwa chanzo chake kikiwa ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani humo. Mwandishi mwingine ni Janeth Joseph wa Mwananchi, ambaye mwaka 2020 alipigwa kwa kitako cha bunduki na askari wakati akiwa kazini.

Mwingine ni mwandishi wa The Guardian, James Lanka, ambaye mwaka huu aliwekwa maabusu ya polisi kwa siku tatu na kunyimwa haki ya kutoa taarifa kwa ndugu ili apate dhamana.

Lanka alikamatwa alipokuwa alifuatilia habari ya maofisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kukusanya ushuru siku ya Jumalipi kwa kutumia na pasipokutoa stakabadhi.Kadhalika mwandishi Elia Peter wa Global TValitoa taarifa za pokea vitisho mara kwa mara kutoka kwa mmoja wa vigogo wa wilaya mojawapo ya mkoa wa Kilimanjaro, jambo ambalo limekuwa likimwogofya katika kutekeleza majukumu yake.

Yapo pia matukio ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana –Mwanza kumtishia mwandishi wa ITVna lile la mkoani Katavi ambako wananchi walichukua sheria mkoani dhidi ya Waandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten waliokuwa wamekwenda kuandika Habari za uchaguzi wa Imamu wa Msikiti. Wale ambao hawakukubalimatokeo waliamua kushambulia waandishi hao wa Habari na kuharibu vifaa vyao vya kazi.

Hili halikubaliki.Pamoja na kupongeza hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia kwa Waziri mwenye dhamana ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Tabia Maulid Mwita, na zile za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 6kupigia kwa Waziri mwenye dhamana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI, Maka Ummy Mwalimu, sisi Wanahabari tunasikitishwa na kuhuzunishwa na wimbi lililoibuka la kushambulia waandishi wa habari, kuharibu vifaa vya kazi au kuwakamata na kuwaweka ndani kwa ubabe bila kufuata misingi ya sheria.Imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya askari ndani ya vyombo vya dola, baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na wakuu wa wilaya wachache, wameanzisha vita dhidi ya waandishi wa habari wanaowakamata, kuwatesa, kuwaweka ndani na kuharibu vifaa vyao vya kazi.

Hili halikubaliki.Wanahabari nchini Tanzania, tunaona mwelekeo huu unatutisha hasa tunapoona watendaji serikalini na baadhi ya askari wakiwa wamebuni mbinu ya kukamata, kupiga, kunyanyasa na kuharibu vitendea kazi vya waandishi wa Habari. Hali hii inawatisha na kuwaogofya waandishi wa Habari waache kufatilia matukio na watendaji hawa au askari wapate fursa ya kunyanyasa wananchi watakavyo.

Mwandishi wa habari ni jicho la jamii hivyo anapaswa kuwapo katika matukio karibu yote kuhakikisha wananchi wanafahamu kinachoendelea. Iwapo mtu anatenda jambo jema, hana sababu ya kuhofia uwepo wa waandishi wa habari.

Hali halikubaliki kamwe na inachangia kuzorota kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini.Kimsingi matukio tuliyoyataja hayanaafya kwa taifa letu huko tuendako.

Tunayo mifano ya nchi nyingi duniani zikiwamo zile ambazo ni majirani zetu, ambazo ziliingia katika gharama kubwa ya watu wake, kwa kudharau matukio madogo madogo kama ambayo yanatokea nchini mwetu hivi sasa.Sisi waandishi wa habari, tukiwa wataalamu wa habari, tunaowatangulia wenzetu kuona kinachotokea kwa jicho la kiuchambuzi, narejea wito wa kuwapo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa uhuru wa habari nchini, ambao hatima yake ni amani na maridhiano ya kitaifa kabla hayajatukuta makubwa yaliyowakuta 7wenzetu.

Tujifunze kwa wenzetu kwamba vyombo vya dola vinaweza kufanyakazi yake vizuri vikiwa vinaungwa mkono na raia wa taifa husika na bila kuviburuza vyombo vya habari.Tunaomba serikali ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan ifuatilie kwa karibu matukio haya na kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika, ikiwa sehemu ya kupeleka ujumbe kuwa nchi hii inatawaliwa kwa mujibu wa sheria na si matakwa ya mtu binafsi.

Ni aibu kuona nchi yetu bado ina watu wanaotamani kupiga waandishi wa habari au kuharibu vitendea kazi vyao.

UTAWALA WA SHERIA

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, sualala utawala wa sheria limeingia doa katika miaka michache iliyopita, tofauti na utamaduni wa muda mrefu wa kuheshimu utawala wa sheria.

Tulizoea serikali yetu sikivu, kutekeleza mara moja uamuzi wa mahakama pale ilipotoa hukumu na serikali kushindwa katikakesi na/au mashauri husika.

Lakini kwa masikitiko makubwa tumeshuhudia tangu mwaka 2018 magazeti ya MAWIO na MWANAHALISIyaliposhinda kesi mahakamani, bado Idara ya Habari (MAELEZO)imekataa kuyapatia leseni ili yarudi mtaani na kuendelea kuchapishwa.

PONGEZI KWA KAULI YA MHE. RAIS SAMIA

Tunampongeza wazi Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye katika Hotuba yake ya Aprili 6, 2021 aliagiza Serikali kufungulia vyombo vya habari vilivyogungiwa.

Rais Samia, alisema:"Nasikia kuna vyombo vya habari huko mlivifungia fungia, sijui vijiTV vya mikononi vile, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, tusiwape mdomo wa kusema tunaminya Uhuru wa vyombo vya habari"Tunasikitika muda mfupi baadaye, agizo hili pana lilipewa tafsiri finyu na baadhi ya watendaji serikalini.

Wakasema Rais aliagiza kufunguliwa kwa TV za mtandaoni pekee.

Tunafahamu kwamba Mheshimiwa Waziri ulitoa fursa ya mazungumzo kwa magazeti ambayo yamefungiwa, nasi tunasubiri kwa shauku kuona matokeo ya mazungumzo hayo tukitaraji kwamba yataruhisiwa kuanza kuchapishwa tena. Lakini ni wazi kwamba mwenendo wa Serikali kupuuza hukumu ya mahakama ni uvunjaji wa sheria ambao unatoa picha kwamba mihimili haiheshimiani.

SHERIA ZA HABARI

Mhe. Waziri, Mahakamaya Afrika Mashariki ilitoa hukumu ikielekeza Serikali ifute vifungu tisa katika Sheria ya Huduma za Habari (MSA, 2016) kwa kuwa vinakinzana na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Rais Samia, ameiagiza Serikali kufanya marekebisho ya sheria kandamizi ziwe katika mukutadha unaoeleweka na kutamka bayana aina ya adhabu kwa kila kosa.Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Habari Dk. Harisson Mwakyembe alipokutana na Uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na ujumbe wa International Press Institute (IPI) Aprili 2, 2019 alisema Serikali iko tayari kukutana na wadau kurekebisha upungufu kwenye sheria hii.

Kadhalika Katibu Mkuu wa Wizara yako, Dk. Hassan Abbas alipozungumza katika moja ya matukio ya utangulizi wa maadhimhso haya, pale jijini Dar es Salaam, amesema milango iko wazi kwa mapendekezo ya kurekebisha sheria za kihabari. Ombi letu ni kwamba utekelezaji huu uwe wa haraka na usibakie kuwa ahadi tu.

Mhe. Mgeni ramsi, kati ya sheria kandamizi zinazolalamikiwa ni pamoja na Media Services Act 2016, Cyber Crimes Act 2015, Statistics Act 2015 (kama ilivyorekebishwa 2018), Right to Information (RTI) 2016, Online Content Regulation 2017, na nyingine nyingi ambazo kwa njia moja au nyingine zinaminya uhuru wa habari au watu kutoa mawazo.

Tunaomba hizi zirekebishwe na kuondoa masharti yanayokandamizia uhuru wa Habari nchini, ikiwamo hili gumu la kutoa leseni kwa magazeti inayotumika kama fimbo vya kufumba midomo ya baadhi ya wachapishaji.

HITIMISHO

Mwisho, Mheshimiwa mgeni ramsi, si kwaumuhimu, natambua na kupongeza juhudi za serikali za kusimamia misingi ya uwajibikaji, vita dhidi ya rushwa na ufisadi, usimamizi wa mapato ya serikali, matumizi endelevu ya rasilimali za umma, ujenzi wa miundombinu kama vile reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler’s Gorge, uimarishaji wa shirika la ndege (ATCL), kuhamia makao makuu Dodoma, usimamizi wa Sera ya Viwanda, kuidhibiti TRA isiue biashara za wawekezaji na wazawa kutokana na kodi kandamizi, na mengine kadha wa kadha, ambayo ni vyanzo vya habari tunazozichapisha.

Hata hivyo, tunasisitiza kuwa maendeleo haya yatakuwa na maana zaidi kwa kuwa na taifa ambalo wananchi wake wanaishi kwa amani halisi, kwa kuamininiana na kutumia uhuru wao wa kutoa mawazo bila woga.

Shughuli hii imeandaliwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), MISA-Tanzania, Jukwaa la WahaririTanzania (TEF), Friedrich Ebert Stiftung, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Tanzania Media Foundation (TMF), United Nations Tanzania, Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Nukta Afrika, Jamii Media, Elimika, Twaweza, East Africa Radio,Sikika, Jamii Forumsna Legal Services Facility -LSF

Asanteni kwa kunisikiliza....


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news