Mbunge Mtenga aomba wakulima wa Mtwara Mjini wakumbukwe

Na Diramakini (diramakini@gmail.com)

Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga amerejea ombi lake kwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kutuma wataalamu wake jimboni humo hususani katika eneo la Kitele ambalo linatoa maji ya uhakika ili kuwapa wakulima wa mpunga mbinu za kulima kibiashara zaidi tofauti na sasa ambapo wanalima kwa ajili ya chakula.

Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga (Picha diramakini@gmail.com).

Lengo ni kuwezesha uzalishaji mkubwa wa mpunga ambao utasaidia upatikanaji wa chakula cha kutosha kwa wakulima hao pamoja na kuuza maeneo mengine ili kuendelea kuimarisha uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Wito huo unakuja baada ya hivi karibuni wakati wa kujadili Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa kwa miaka mitano bungeni jijini Dodoma kugusia kuhusu umuhimu wa eneo hilo ambapo pia Mtenga alitoa mapendekezo ya kuboresha mpango wa elimu bure na namna ya kuvifanya viwanda hapa nchini kuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa muda mrefu.

Akizungumza mjini hapa amesema kuwa, ana imani kubwa na viongozi wa Wizara ya Kilimo wakiongozwa na Waziri Prof. Adolf Mkenda na Naibu Waziri, Hussein Bashe kwa kuwa, licha ya usikivu wao ni watu ambao wanafuatilia jambo kwa karibu ili kuhakikisha linatoa matokeo ya haraka kwa wakulima.

Mbunge Mtenga amesema kuwa, eneo la Kitele ni miongoni mwa maeneo machache ambayo yana utajiri mkubwa wa rutuba na maji ya kutosha ambalo anaamini linaweza kubadili uchumi wa wananchi hao.

Amesema, hilo ni eneo ambalo amelishuhudia tangu akiwa mtoto hadi sasa anaelekea uzeeni ambalo limekuwa linamwaga maji ambalo ni chemchem ya kutosha na linaweza kutumika ipasavyo kwa ajili ya kilimo biashara.

Mbunge Mtenga amesema, wananchi wamekuwa wakilima mpunga ambao hauna tija kubwa, hivyo anaiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kufika hapo ili kuona namna ya kuwasaidia wakulima waweze kuzalisha kwa faida zaidi.

"Ninaamini wataalamu wa kilimo wakifika kujionea, watashauri na kutupa njia ya kujikita zaidi katika kilimo biashara. Kilimo ambacho ni mkombozi kwa wakulima wengi kwa sasa, pale hakuna skimu za umwagiliaji, wakati ule mpunga ni mzuri sana,"amesema Mtenga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news