MPANGO WA KITAIFA WA RASILIMALIWATU WAANDALIWA NCHINI

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael amesema, Serikali kupitia Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu imeandaa rasimu ya Mwongozo wa Kitaifa wa Mpango wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma utakaowezesha kuainisha mahitaji sahihi ya kitaifa ikiwa ni pamoja na kuwezesha usimamizi na matumizi mazuri ya rasilimaliwatu, anaripoti James K.Mwanamyoto (OR-Utumishi).
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael akifungua kikao cha kujadili rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika leo jijini Dodoma.

Dkt. Michael amesema hayo leo jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI wakati akifungua kikao cha kujadili rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.

Dkt. Michael amesema, bila kuwa na mpango wa rasilimaliwatu, Serikali inaweza kupata changamoto ya upungufu wa watumishi au kuwa na watumishi wengi wanaotosheleza kwa idadi lakini hawana ujuzi wa kutekeleza majukumu yao kikamilifu, hivyo ndio maana Serikali imeona umuhimu wa kuhuisha Mpango wa Rasilimaliwatu wa Kitaifa.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Bw. Elisante Mbwilo akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael kufungua kikao cha kujadili rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika leo jijini Dodoma.

Amefafanua kuwa, ili kufikia uchumi wa kati wa juu kupitia Sera ya Maendeleo ya Viwanda ni dhahiri kuwa Utumishi wa Umma unapaswa kuwa na watumishi wa kutosha na wenye sifa stahiki hivyo amewataka washiriki kutumia uzoefu wao kujadili kwa kina rasimu ya mpango huo kwa lengo la kuiwezesha Serikali kupata mwongozo mzuri wa kuandaa Mpango wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu utakaokuwa na tija kwa maendeleo ya taifa.

“Tumieni uzoefu wenu na elimu mliyonayo pamoja na ubunifu ili kuiwezesha Serikali kupata Mpango Mzuri wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu.” Dkt. Michael amesisitiza.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Dkt. Edith Rwiza akiwasilisha mada kuhusu Mpango wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu kwa Washiriki wa kikao cha kujadili rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.

Kwa upande wa washiriki, Mkurugenzi Msaidizi Utawala wa Wizara ya Maji Bi. Wanyenda Kuta amesema, Mpango huo wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu utawezesha Utumishi wa Umma nchini kuwa na rasilimaliwatu yenye sifa na kukidhi utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi Rasilimaliwatu TAMISEMI, Bw. Marko Masaya amesema kuwa, Mpango wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu utaziwezesha Taasisi za Umma kuandaa mipango ya kati, muda mfupi na mrefu itakayosaidia kuwa na watumishi wenye sifa stahiki na malengo yanayopimika na kuongeza kuwa utawezesha kujua aina ya watumishi wanaohitajika na sehemu watakayopatikana aidha ndani au nje ya Utumishi wa Umma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao cha kujadili rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma baada ya kufungua kikao hicho kilichofanyika leo jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi Rasilimaliwatu TAMISEMI Bw. Marko Masaya akizungumzia umuhimu wa Mpango wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu unaojadiliwa na unaojadiliwa jijini Dodoma na wadau kutoka katika Taasisi mbalimbali za Umma.

Sanjari na hilo, Bw. Masaya ameongeza kuwa, mpango huo utaiwezesha Serikali kujua katika kipindi cha miaka miwili au mitatu ijayo itahitaji kuwa na watumishi wa aina gani, wenye weledi upi na kiwango kipi cha elimu.

Kikao cha kujadili rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kimejumuisha wasimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka katika Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news