MUHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO, MHESHIMIWA PROF. ADOLF F. MKENDA (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KILIMO KWA MWAKA 2021/2022

Mheshimiwa Spika, natoa shukrani kwa wakulima wote kwa kazi kubwa wanazofanya kuendeleza kilimo nchini. Ni wazi kuwa mafanikio ya kilimo yanatokana na juhudi na ushirikiano mkubwa na Serikali. Kipekee nirudie kuwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Rombo kwa namna wanavyoniunga mkono na kunipa ushirikiano. Naomba wote watambue kuwa kilimo ni maisha, uchumi, biashara, viwanda na ajira.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 Bungeni Jijini Dodoma Tarehe 24 Mei 2021.
1. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, ninaomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.

2. Mheshimiwa Spika, naomba hotuba yote iliyowasilishwa mezani iingie kwenye kumbukumbu za Bunge lako Tukufu, ili mimi niokoe muda kwa kusoma tu muhtasari wa hotuba hiyo. Aidha Hotuba yote inapatikana pia kwenye tovuti ya Wizara, www.kilimo.go.tz

3. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninapenda tena kuungana na Wabunge wote kutoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa msiba mkubwa tulioupata wa kuondokewa na aliyekuwa Rais wetu, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Ninatoa pole pia kwa Mheshimiwa Janeth Magufuli, Mama Suzana Magufuli, watoto na ndugu wote wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wenzangu wote. Tutaenzi mchango mkubwa wa Rais wetu wa Awamu ya Tano katika ujenzi wa Taifa letu na tutajitahidi kuendeleza uthubutu, uchapakazi na uzalendo kama alivyotufundisha Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

4. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni pia tulimpoteza aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad.

Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa ni kiongozi maarufu sana hapa nchini na atakumbukwa kwa mengi. Tutamkumbuka sana kwa kushirikiana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuleta maridhiano na mshikamano wa Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2020. Ninatoa pole nyingi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, familia ya Hayati Seif Sharif Hamad na Watanzania wenzangu wote kwa msiba huu mkubwa wa kuondokewa na Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad.

5. Mheshimiwa Spika, kipindi hiki pia tumempoteza aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Hayati Balozi John William Herbert Kijazi. Sote tunamkumbuka Balozi Kijazi kwa uchapakazi wake na karama yake kuu ya kuwaheshimu wote aliofanya nao kazi kwa ukarimu, na uwezo wake mkubwa wa kuelewa na kuusimamia utumishi wa umma kwa uadilifu Mkubwa.

6. Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu limepata pia pigo la kuondokewa na wabunge watatu; Hayati Atashasta Justus Nditiye aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, Hayati Martha Jachi Umbulla, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Manyara na Hayati Khatibu Said Haji aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Konde. Ninaungana tena na Mheshimiwa Spika na wabunge wenzangu wote kuomboleza misiba hii mikubwa.

7. Mheshimiwa Spika, pamoja na pigo kubwa sana na huzuni kuu ya kuondokewa na aliyekuwa Rais wetu, Taifa letu limehimili vyema kwa sababu ya misingi imara ya kikatiba ya nchi yetu na utamaduni wa kisiasa ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekamata hatamu za uongozi wa nchi yetu, na ametuongoza na kutufariji katika majonzi na amefanikiwa kuleta matumaini makubwa. Ninamuombea afya njema na mafanikio makubwa katika kazi hii nzito ya kuliongoza Taifa letu.

8. Mheshimiwa Spika, kama nitakavyoeleza katika hotuba hii, mikakati yetu katika sekta ya kilimo tumeipanga kwa kuzingatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa kupitia hotuba yake hapa Bungeni ya tarehe 22 April, 2021

9. Mheshimiwa Spika, ninaomba nitoe pongezi za dhati kwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi kwa nafasi za uongozi wa juu katika Taifa letu ambazo wameaminiwa na kukabidhiwa. Ninawaombea afya njema na mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu haya makubwa.

10. Mheshimiwa Spika, ninampongeza pia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa kuendelea na wadhifa wake huo katika uongozi wa awamu ya sita, na ninamshukuru kwa kutusimamia na kutuongoza vizuri.

11. Mheshimiwa Spika, pongezi nyingi pia kwa Spika, Mheshimiwa Job Ndugai na Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kuendelea kuliongoza Bunge hili tukufu. Ninawapongeza wabunge wenzangu wote kwa kuaminiwa na vyama vyetu na kuchaguliwa kuwa wabunge. Kwa namna ya kipekee nawapongeza waheshimiwa Eliadory Felix Kavejuru na Dkt. Florence George Samizi kwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa majimbo ya Buhigwe na Muhambwe mtawalia.

12. Mheshimiwa Spika, mimi binafsi ninakishukuru sana Chama cha Mapinduzi kwa kuniteua kugombea ubunge katika Jimbo la Rombo na ninawashukuru sana wananchi wa Rombo kwa kunichagua. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Waziri wa Kilimo. Naahidi kwa Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Rais, wananchi wa Rombo na Watanzania wote kwa ujumla kwamba nitatumikia nafasi za ubunge na uwaziri kwa bidii, maarifa, weledi na uadilifu.

13. Kwa namna ya pekee namshukuru sana mke wangu, Beatrice, na familia yangu kwa ujumla kwa upendo na uvumilivu wao wakati wote.

14. Mheshimiwa Spika, ninapenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, na Makamu Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Almas Athumani Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kwa ushirikiano mzuri na ushauri makini ambao wameendelea kuutoa kwetu katika kupitia Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2020/2021 na Mpango wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2021/2022. Ushauri wao umezingatiwa na tunaahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Kamati katika kuendeleza kilimo hapa nchini.

15. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee ninawashukuru viongozi na watumishi wote wa Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano wao na bidii yao katika kazi na maandalizi ya hotuba hii. Ninamshukuru sana Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe (Mb), kwa jinsi tunavyosaidiana kwa karibu katika kutekeleza majukumu ya Wizara tuliyokabidhiwa. Ninamshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Andrew Wilson Massawe na Naibu Katibu Mkuu, Profesa Siza Donald Tumbo kwa kazi nzuri na ushirikiano mkubwa ambao wao pamoja na wakurugenzi, wakuu wa taasisi, Bodi na Wakala zilizo chini ya Wizara na watumishi wote wa Wizara kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa.

16. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipomshukuru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Musabila Kusaya ambaye kwa sasa ni Kamishna Jenerali wa Tume ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya kwa kunikaribisha na kufanya naye kazi kwa karibu kwa kipindi chote nilichokuwa naye Wizarani.
2. MCHANGO WA KILIMO KATIKA UCHUMI MWAKA 2020

17. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020, mchango wa kilimo katika Pato la Taifa (GDP) ulikuwa ni asilimia 26.9. Aidha, katika kipindi hicho, sekta ya kilimo imekua kwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na asilimia 4.4 ya mwaka 2019. Vilevile, uzalishaji wa sekta ndogo ya mazao umekua kwa asilimia 5.0 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.4 katika mwaka 2019. Pia, katika mwaka 2020, sekta ya kilimo imechangia kwa asilimia 58.1 katika kutoa ajira nchini na kuchangia zaidi ya asilimia 65 ya malighafi za viwanda nchini.
3. MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2020/2021
3.1 Makusanyo ya Maduhuli

18. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara ilikadiria kukusanya Shilingi bilioni 5.79 kutokana na vyanzo mbalimbali. Hadi Aprili 2021, Wizara imekusanya Shilingi bilioni 2.69 sawa na asilimia 46.48 ya makadirio.
3.2 Fedha Zilizoidhinishwa

19. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo kupitia Fungu 43, Fungu 05 na Fungu 24 iliidhinishiwa Shilingi bilioni 229.83. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 79.76 ni za matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 150.07 za miradi ya maendeleo.

20. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo (Fungu 43) iliidhinishiwa Shilingi bilioni 202.50 ambapo Shilingi bilioni 65.23 ni fedha za matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 137.27 ni fedha za maendeleo. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (Fungu 05) iliidhinishiwa Shilingi bilioni 17.72 ambapo Shilingi bilioni 4.92 ni za matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 12.80 ni za miradi ya maendeleo. Tume ya Maendeleo ya Ushirika (Fungu 24) ilitengewa Shilingi bilioni 9.60 kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
4.0 UTEKELEZAJI WA MALENGO MKAKATI KWA MWAKA 2020/2021

21. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2020/2021, umezingatia yafuatayo:-

i. Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2015 – 2020;

ii. Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka mitano Awamu ya Pili (2015/2016- 2020/2021); na

iii. Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II).



22. Mheshimiwa Spika, miongozo hiyo, imezingatiwa katika kuboresha mifumo ya Kitaasisi, Bodi na Sheria za Kilimo; kuunganisha wakulima wadogo na wakulima wakubwa; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji, ghala na masoko, kuimarisha upatikanaji wa pembejeo na huduma za ugani; kuimarisha maendeleo ya ushirika; Kuongeza matumizi ya teknolojia bora; kuimarisha Vituo vya Utafiti, Vyuo vya Mafunzo na Vituo vya Wakulima; na huduma za upimaji wa matabaka na ubora wa udongo.


4.1 Kuboresha Mifumo ya Kitaasisi, Bodi na Sheria za Kilimo



Mifumo ya Kielektroniki ya kutoa huduma katika Sekta ya Kilimo

23. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutumia Mfumo wa Utoaji wa Vibali kwa njia ya Kielektroniki (ATMIS), Mfumo wa Usajili wa Wadau wa Sekta ya Kilimo na Mfumo wa M-Kilimo (Mobile – Kilimo). Mifumo hiyo imerahisisha utoaji wa huduma zikiwemo vyeti vya usafi wa mazao ya mimea na vibali vya kuingiza na kuuza mazao nje ya nchi kwa wakati; huduma za ugani; usajili wa wadau wa sekta ya kilimo; na upatikanaji wa takwimu za kilimo.
4.2 Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Umwagiliaji, Masoko na uhifadhi wa Mazao ya Kilimo

24. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu ambapo skimu 13 kupitia mradi wa SSIDP na skimu tano (5) kupitia mradi wa ERPP zimekamilika. Vilevile, Tume kupitia IDF imekamilisha ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji iliyoharibiwa na mafuriko katika skimu ya Ruaha Mbuyuni (Kilolo). Aidha, ukarabati wa Skimu za Mlenge na Magozi (Iringa DC) umefikia asilimia 80.

25. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi unaotekelezwa na NFRA inaendelea kujenga vihenge vya kisasa katika maeneo ya Babati, Shinyanga, Songea, Makambako, Mbozi, Sumbawanga, Mpanda na Dodoma ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka kutoka tani 250,000 hadi tani 501,000 ambapo hadi Mei 2021, ujenzi umefikia asilimia 80.1.
4.3 Kuimarisha Uzalishaji wa Mbegu Bora za Mazao na Upatikanaji wa Pembejeo



a) Mbegu bora

26. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili, 2021 upatikanaji wa mbegu bora nchini umefikia tani 50,589.43 zisizojumuisha miche, vikonyo na vipando ambapo tani 27,330.37 zimezalishwa nchini, tani 15,758.92 zimeingizwa kutoka nje na tani 7,500.14 ni bakaa ya msimu 2019/2020.

27. Aidha, TARI kwa kushirikiana na wadau imezalisha na kusambaza miche milioni 13.56 ya mazao ya viazi vitamu, zabibu, minazi, parachichi, miwa, mkonge na pingili za muhogo milioni 40.9. Vilevile, ASA imezalisha miche 342,000 ya michikichi.

b) Upatikanaji wa Mbolea

28. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu uzalishaji na uingizwaji wa mbolea nchini ambapo hadi Aprili 2021, upatikanaji umefikia tani 678,017 sawa na asilimia 94.4 ya mahitaji ya tani 718,051 msimu wa 2020/2021. Kati ya kiasi hicho tani 426,572 zimeingizwa kutoka nje ya nchi, tani 32,239 zimezalishwa nchini na tani 219,206 ni bakaa ya msimu wa 2019/2020.

c)Upatikanaji wa Viuatilifu vya Mimea na Mazao

29. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2021, upatikanaji wa viuatilifu vya kudhibiti visumbufu vya milipuko umefikia lita 113,000 na kilo 5,000. Kati ya hizo, lita 100,000 ni kwa ajili ya kudhibiti viwavijeshi, lita 5,000 kweleakwelea na lita 7,000 nzige, lita 1,000 nzi wa matunda na kilo 5,000 za kudhibiti panya.

d) Udhibiti wa Visumbufu vya Mimea na Mazao

30. Mheshimiwa Spika, Wizara imedhibiti makundi ya nzige wa jangwani, kwelea kwelea na panya. Wizara imefanikiwa kudhibiti makundi yote ya nzige wa jangwani waliovamia nchi yetu pamoja na nzige wachanga walioanguliwa katika Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

31. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie Bunge lako Tukufu kuwashukuru Mhe. Dkt. Anna Mgwira aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Idd Kimanta aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Mhe. Joseph Mkirikiti aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, wakuu wa Wilaya za Simanjiro, Siha, Longido na Monduli, Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Wilaya husika kwa ushirikiano wao katika kupambana na nzige. Aidha, nitoe shukrani za dhati kwa Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Anga na hasa Meneja wa Kiwanja cha Ndege Arusha, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa ushirikiano wao katika zoezi la kudhibiti nzige hao.
4.4 Kuimarisha Usimamizi wa Maendeleo ya Ushirika

32. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imekagua Vyama vya Ushirika 4,494 kati ya 9,185. Aidha, kaguzi maalum zimefanyika kwa vyama 35 na hatua stahiki zimechukuliwa kwa waliojihusisha na wizi na ubadhilifu wa mali na fedha za vyama vya ushirika.

33. Mheshimiwa Spika, Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limekagua vyama vya ushirika 6,021 na Serikali imechukua hatua stahiki kwa vyama vyote ambavyo vimebainika kuwa na ubadhirifu wa fedha na mali za vyama.

34. Mheshimiwa Spika, Tume imefuatilia mali za Vyama vya Ushirika zilizochukuliwa kinyume na utaratibu ambapo mali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 68.9 zimerejeshwa. Aidha, Tume imehamasisha uanzishwaji wa Viwanda vya kuchakata mazao ambapo viwanda vimeongezeka kutoka 374 mwaka 2019 hadi 452 mwaka 2020. Pia, ajira katika Vyama vya Ushirika imeongezeka kutoka 90,090 mwaka 2019 hadi 100,100 mwaka 2020.
4.5 Kuongeza Matumizi ya Teknolojia Bora katika Uzalishaji wa Mazao



Zana za Kilimo

35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 matumizi ya trekta yameongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2019 hadi asilimia 23 mwaka 2020. Ongezeko hilo limepunguza matumizi ya jembe la mkono kutoka asilimia 53 mwaka 2019 hadi asilimia 50 mwaka 2020. Katika kipindi hicho sekta binafisi imeingiza matrekta makubwa 1,124 na matrekta madogo ya mkono 459 nchini.

Huduma za Ugani



36. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma za ugani Wizara imeandaa rasimu ya Mwongozo wa Usimamizi na Uratibu wa Huduma za Ugani utakaotumiwa na sekta ya umma na binafsi ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

37. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TARI imetoa mafunzo kuhusu teknolojia bora za kilimo kwa wakulima 51,304 na Maafisa Ugani 982 kupitia vituo 11 vya TARI na Kituo cha Usambazaji wa Teknolojia (Nyakabindi AgriTecH). Wizara pia, imeratibu maonesho ya wakulima (Nanenane) ambapo wadau 2,253 na Wakulima 1,250 walijifunza teknolojia bora za kilimo na fursa za masoko.



Uzalishaji wa Mazao



38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, uzalishaji wa mazao asilia ya biashara ya Tumbaku, Pamba, Kahawa, Chai, Pareto, Korosho, Mkonge na Sukari umefikia tani 876,510.83.



39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 uzalishaji wa mazao ya mafuta umefikia tani milioni 1.58 ikilinganishwa na tani milioni 1.23 mwaka 2018/2019.

40. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 upatikanaji wa mbegu bora za alizeti na ufuta umefikia tani 441.42 na 90.51 mtawalia. Aidha, mbegu milioni 3.82 za chikichi zimezalishwa.

41. Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao ya bustani umeongezeka kutoka tani milioni 6.59 mwaka 2018/2019 hadi tani milioni 7.56 mwaka 2019/2020.

42. Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao ya chakula yanayojumuisha mahindi, mpunga, mtama/uwele, mikunde, ngano, ndizi, muhogo na viazi kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 umefikia tani 18,196,733.

Masoko ya Mazao



43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara imeendelea kufuatilia masoko ya mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi. Wizara kupitia Bodi ya Korosho imeratibu minada 70 ya uuzaji wa korosho ambapo tani 206,718.88 za korosho ghafi zenye thamani ya Shilingi bilioni 473.17 zimeuzwa. Aidha, Wizara kupitia Bodi ya Tumbaku imekagua tani 20,381.4362 za tumbaku viwandani zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 74.85.

44. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho tani 8,517 za chai zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 11.69 zimeuzwa nje ya nchi na tani 1,795 za chai zenye thamani ya Shilingi milioni 16.19 zimeuzwa katika soko la ndani. Pia, tani 61,306 za kahawa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 123.8 na tani 1,346.7 za choroko zenye thamani ya Shilingi bilioni 2.4 zimeuzwa.

45. Mheshimiwa Spika, katika kufungua masoko mapya ya mazao, Wizara ilifanya Mkutano wa wafanyabiashara wa mazao ya nafaka ulioshirikisha Mabalozi wa Nchi za Rwanda, Misri, Burundi, DRC, Zambia, Sudan Kusini, Malawi, Kenya, Uganda na Msumbiji waweze kuunganishwa na masoko katika nchi hizo. Vilevile, Wizara imefungua masoko ya mazao mapya ya parachichi katika nchi za India, Marekani na inakamilisha taratibu za kufungua soko la zao hilo katika nchi ya China; maharage ya soya katika nchi ya China ambapo hadi Aprili, 2021 jumla ya wafanyabiashara 49 wamesajiliwa kwenye Mamlaka ya Forodha ya China kwa ajili ya kuuza soya.
4.6 Kuimarisha Huduma za Upimaji wa Matabaka na Ubora wa Udongo

46. Mheshimiwa Spika, ili kuleta ufanisi katika matumizi ya chokaa kama virutubishi vya udongo, Wizara imeandaa Mwongozo wa Matumizi ya Chokaa katika Kilimo utakaotumiwa na Maafisa Ugani kufundishia wakulima.
5. VIPAUMBELE VYA KIMKAKATI KWA MWAKA 2021/2022

47. Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti ya mwaka 2021/2022 ya Wizara umezingatia yafuatayo:-

i. Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2020-2025,

ii. Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano Awamu ya Tatu (2021/2022 – 2025/2026, na

iii. Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)



48. Mheshimiwa Spika, Miongozo yote iliyoainishwa imesisitizwa katika Hotuba ya Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alipolihutubia Bunge lako Tukufu tarehe 22 Aprili, 2021. Hotuba hiyo imeweka dira kwa kuanisha vipaumbele vikubwa na vya kimkakati. Katika kupanga mipango ya mwaka 2021/2022 tumezingatia vipaumbele hivyo kama vilivyosisitizwa kwenye maelekezo ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Daniel Chongolo, tarehe 20 Mei, 2021.

49. Mheshimiwa Spika, katika hotuba yake, Rais aliainisha tija ndogo kama tatizo kubwa linaloikabili sekta ya kilimo. Hili linaonekana wazi kwenye takwimu zinazohusu mchango wa Sekta ya Kilimo katika Pato la Taifa ambao umefikia asilimia 26.9 kwa mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 58.1 ya ajira. Hii ina maana kwamba takribani theluthi mbili ya nguvukazi hapa nchini inachangia takriban theluthi moja ya Pato la Taifa, hiki ni kielelezo tosha kwamba tija ni ndogo.

50. Mheshimiwa Spika, mpango mkubwa wa kimkakati ni kuongeza tija katika uzalishaji. Hivyo, kipaumbele cha kwanza kikubwa cha kimkakati katika kuongeza tija ni kuweka mkazo katika utafiti utakaozingatia ugunduzi wa aina za mbegu bora na mbinu bora za kilimo. Ili kufikia malengo hayo tutafanya yafuatayo:-

i. Kufanya utafiti wa mbegu bora zenye tija kubwa kwa mfano tafiti zinaonesha kuwa TARI wamefanikiwa kugundua aina za mbegu za muhogo inayozalisha wastani wa tani 22-50 kwa hekta ikilinganishwa na wastani wa tani 8 kwa hekta zinazozalishwa sasa na wakulima wengi.

Kwa upande wa pamba tija ya sasa ni kilo 250-300 kwa ekari ikilinganishwa na uwezo wa kufikia wastani wa kilo 1000-2000 kwa ekari,

ii. kuongeza bajeti ya TARI kutoka Shilingi bilioni 7.35 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11.63 mwaka 2021/2022, na

iii. kuimarisha upatikanaji wa fedha za maendeleo ya utafiti wa kilimo kwa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Utafiti kwa mujibu wa Kifungu 26(1) cha Sheria Na. 10 ya mwaka 2016 iliyoanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI Act No. 10, 2016).

51. Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha pili cha kimkakati cha kuongeza tija ni kuongeza uzalishaji wa mbegu bora. Sote tunafahamu nchi yetu bado hatujajitosheleza kwa mahitaji ya mbegu, hivyo kulazimika kuagiza kutoka nje ya nchi.

52. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza uzalishaji wa mbegu bora nchi, Wizara imepanga kuendeleza mashamba 13 ya mbegu ya ASA kwa kuweka miundombinu ya umwagiliaji kwa kutumia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji; kuongeza bajeti ya uzalishaji wa mbegu bora kutoka Shilingi bilioni 5.42 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 10.58 mwaka 2021/2022; na kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kuzalisha mbegu bora nchini.

53. Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha tatu cha kimkakati ni kuimarisha huduma za ugani. Idadi ya Maafisa Ugani wanaotoa huduma za ugani nchini katika ngazi ya Kata na Vijiji ni 6,704. Idadi hiyo, ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya 20,538. Pamoja na idadi hiyo kuwa ndogo, Maafisa ugani hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vitendea kazi pamoja na mafunzo rejea.

54. Mheshimiwa Spika, upungufu huo wa maafisa ugani pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo huchangia wakulima wengi kukosa huduma za ugani ikiwemo matumizi ya mbegu bora, matumizi sahihi ya viuatilifu, zana bora, mbinu bora za kilimo na taarifa za masoko.

55. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imeongeza bajeti ya eneo hilo kutoka Shilingi milioni 603 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11.5 mwaka 2021/2022. Fedha hizo zitatumika katika kuimarisha huduma za ugani nchini ikiwa ni pamoja na kununua pikipiki 1,500, vifaa vya kupima afya ya udongo, visanduku vya ufundi (Extension Kit), simu janja, kuwezesha uanzishwaji wa mashamba ya mfano kwa kila Afisa Ugani na kutoa mafunzo rejea. Vilevile, maafisa ugani watasimamiwa katika kuanzisha mashamba darasa kulingana na mahitaji ya wakulima kwa ajili ya kuendeleza kilimo katika eneo husika.

56. Mheshimiwa Spika, tutaianza safari yetu ya kuboresha huduma za ugani katika mikoa mitatu ya kielelezo ambayo ni Dodoma, Singida na Simiyu. Mikoa hiyo ina fursa kubwa ya kuzalisha mazao ya mafuta hususan alizeti na pamba. Katika Mikoa hiyo maafisa ugani wote watapewa pikipiki, vifaa vya kupima afya ya udongo, visanduku vya ufundi (Extension Kits), simu janja, kuwezesha uanzishwaji wa mashamba ya mfano kwa kila Afisa Ugani na kutoa mafunzo rejea yatakayozingatia mazao yote yanayolimwa katika maeneo hayo. Pia maafisa ugani hao, watawezeshwa kuanzisha mashamba darasa.

57. Mheshimiwa Spika, kwa kuwawezesha maafisa ugani hao, tunatarajia utoaji wa huduma za ugani utaimarika, wakulima wengi watafikiwa kwa wakati na tija ya uzalishaji itaongezeka. Kwa mfano matumizi ya simu janja yatawezesha wakulima kupata utatuzi wa changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo taarifa za masoko ya mazao ya kilimo wanayozalisha. Mafanikio yatakayopatikana katika mikoa hiyo ya kielelezo, yataenezwa katika mikoa mingine nchini.

58. Mheshimiwa Spika, Wizara pia itaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kuimarisha huduma za ugani kwa kutumia mbinu zilizoonesha mafanikio katika kuongeza tija. Kwa mfano, TAHA inatoa mafunzo ya kilimo bora cha mazao ya bustani na kuwaunganisha wakulima na watoa huduma za pembejeo na masoko. Vilevile, Kampuni ya kutoa huduma kwa wakulima wadogo wa chai Njombe (Njombe Outgrowers Services Company) imeajiri maafisa ugani, na inatoa huduma za uvunaji na uuzaji wa majani mabichi ya chai kwenye kiwanda cha Uniliver. Pia, Chama kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) kimeajiri maafisa ugani kwa ajili ya kutoa huduma kwenye mazao ya tumbaku na pamba.

59. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mtawanyiko wa mazao ya kilimo yanayozalishwa nchini na mahitaji ya soko, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na wadau wengine wa kilimo itasimamia utoaji wa huduma za ugani katika mikoa yote ili kuongeza tija katika mazao kulingana na viwango vya uzalishaji vinavyohitajika.

60. Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha nne cha kimkakati ni kuimarisha kilimo cha umwagiliaji. Kama tunavyofahamu, kilimo chetu nchini kinategemea mvua kwa asilimia kubwa ambazo hazitabiriki kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Kilimo cha umwagiliaji kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ubovu wa miundombinu, kutokamilika kwa baadhi ya miradi ya umwagiliaji, kukosekana kwa miundombinu ya umwagiliaji yenye fursa za umwagiliaji, mitaji ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na elimu ndogo ya matumizi ya teknolojia za umwagiliaji.

61. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchini, Wizara imepanga kuongeza eneo la umwagiliaji kwa kuhamasisha wadau kuwekeza katika ujenzi miundombinu, uvunaji wa maji na uchimbaji wa visima kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Aidha, Wizara kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji (IDF) ulioanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 52 cha Sheria ya Umwagiliaji Na. 4 ya mwaka 2013 itakamilisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo mashamba 13 ya mbegu ya ASA, kukarabati miundombinu ya umwagiliaji, kukamilisha miradi ya umwagiliaji, kujenga mabwawa na kufanya upembuzi yakinifu kwenye miradi mipya.

62. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kufanya tathmini ya skimu zote za umwagiliaji na maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji. Lengo ni kuhakiki eneo linalomwagiliwa, kubaini mahitaji halisi ya rasilimali za kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa ajili ya kuboresha Mpango Kamambe wa Uendelezaji wa Kilimo cha Umwagiliaji Nchini.



63. Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha tano cha kimkakati ni kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo. Changamoto ya masoko nchini ina sura kuu mbili; kwanza ni uzalishaji mdogo usiokidhi mahitaji ya soko na pili ni kuwepo kwa uzalishaji mkubwa ikilinganishwa na upatikanaji wa masoko. Kwa mfano, viwanda vya kukamua mafuta ya alizeti vinafanya kazi takribani miezi minne kwa mwaka kutokana na ukosefu wa malighafi. Kwa upande wa mazao ya nafaka ikiwemo mahindi na mpunga, uzalishaji wake ni mkubwa na ziada inakosa soko.

64. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha upatikanaji wa masoko ndani na nje ya nchi, Wizara itaimarisha utekelezaji wa kilimo cha mkataba katika mazao ya shayiri, ngano, alizeti, zabibu, maharage ya soya na mazao mengine kwa kutoa mwongozo wa mikataba baina ya wakulima na wenye viwanda vya kusindika mazao.

65. Aidha, Wizara itaratibu ubia wa kibiashara baina ya wafanyabiashara wa mazao hapa nchini na nchi za nje zenye fursa kubwa ya masoko ikiwemo Sudani Kusini, DRC, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Msumbiji, Kenya, Vietnam na China. Uratibu huo utahusisha safari za wafanyabiashara kwenda katika nchi hizo na kuanzisha vituo vya kuonesha bidhaa za mazao ya kilimo kutoka Tanzania.

66. Mheshimiwa Spika, Wizara itawezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika wa mazao la shayiri na hivyo kuongeza uzalishaji wa ndani; inaendelea kuratibu uwekezaji wa kampuni za bia ili kuwekeza Dola za Marekani milioni 42 katika kiwanda cha kutengeneza kimea kitakachojengwa Jijini Dodoma chenye uwezo wa kusindika shayiri tani 35,000 kwa mwaka kutoka kwa wakulima. Wizara kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imeingia mkataba na wakulima kwa lengo la kununua tani 21,600 za ngano.

67. Mheshimiwa Spika, Wizara pia, itaendelea kuratibu makubaliano kati ya wasindikaji na wakulima ambapo wasindikaji watanunua kwanza ngano inayozalishwa ndani kabla ya kuagiza kutoka nje. Aidha, katika kuimarisha kilimo cha mkataba cha zao la alizeti, Wizara itaendelea kuwaunganisha wakulima na wasindikaji na kuandaa mazingira bora ya uwekezaji katika viwanda vya kusindika alizeti.

68. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kufungua mipaka ya kuuza mazao nje ya nchi na kutoa elimu ya utumiaji wa mfumo wa utoaji vibali kwa njia ya kielektroniki (ATIMS) kwa ajili ya kusafirisha mazao nje ya nchi. Ninapenda kutoa wito kwa wafanyabiashara wa mazao kutumia mfumo huo. Aidha, ninaviomba vyombo vya usalama wa raia tushirikiane kuwezesha biashara ya mazao ya kilimo.

69. Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha sita cha kimkakati ni kuimarisha KILIMO ANGA kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya milipuko na vihamavyo kama vile nzige, kwelea kwelea na viwavijeshi vamizi. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kumekuwa na ongezeko la visumbufu vigeni vinavyoathiri uzalishaji wa mazao na kusababisha upotevu wa mazao hadi asilimia mia moja endapo havitadhibitiwa kikamilifu na kwa wakati. Aidha, baadhi ya visumbufu kama vile nzige na kwelea kwelea udhibiti wake unahitaji vifaa maalum kama vile ndege kwa ajili ya savei na unyunyuziaji wa viuatilifu.



70. Mheshimiwa Spika, Ili kutekeleza kipaumbele hicho, Wizara imeongeza bajeti ya KILIMO ANGA kutoka Shilingi milioni 150 mwaka 2020/2021 hadi bilioni tatu (3) mwaka 2021/2022. Fedha hizo, zitatumika kununua ndege moja mpya kwa ajili ya udhibiti wa visumbufu hivyo.

71. Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha saba cha kimkakati ni kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa mitaji. Upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya shughuli za kilimo umekuwa na changamoto kutokana na riba kubwa zinazotozwa, masharti ya kupata mikopo kutoka taasisi za fedha na vihatarishi katika sekta ya kilimo. Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa ni asilimia 30 tu ya wakulima wanaofikiwa na huduma za mikopo. Aidha, ni asilimia kati ya 7 na 9 ya mikopo iliyotolewa na mabenki ya biashara katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imeelekezwa kwenye sekta ya kilimo.

72. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara itafanya tathmini ya mifumo ya upatikanaji wa mitaji kwa wakulima wadogo na wawekezaji wengine kwenye sekta ya kilimo ili kuibua vizuizi na kuvitafutia majawabu kwa ajili ya kuimarisha ugharamiaji wa mazao katika mnyororo wa thamani. Aidha, Wizara imeunda jopo maalum linalohusisha watendaji wakuu wa taasisi za fedha, ambalo litaongozwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe (Mb), kwa ajili ya kupitia minyororo ya thamani ya mazao na kushauri namna bora ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya uendelezaji wa kilimo nchini.

73. Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara imeunda Timu ya Wataalam inayopitia na kuchambua mifumo ya kikodi katika sekta ya kilimo kwa lengo la kuvutia uwekezaji katika mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo. Katika hatua za awali, Timu imeanza kazi hiyo katika tasnia za mazao ya alizeti, shayiri na dhamana za mikopo. Maelezo zaidi na mambo mengine ya vipaumbele yanapatikana kwenye Hotuba nzima iliyowekwa mezani.

SHUKRANI

74. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuzishukuru Nchi na Mashirika ya Kimataifa ambayo yamesaidia Wizara katika kuendeleza kilimo. Naomba kutaja baadhi ya Nchi na Mashirika ya Kimataifa kama ifuatavyo: Serikali za Japan, Marekani, Uingereza, Ireland, Malaysia, China, Indonesia, Korea ya Kusini, India, Misri, Israel, Ubelgiji, Ujerumani, Finland, Norway, Brazil, Uholanzi, Vietnam, Canada na Poland. Ninayashukuru pia Mashirika na Taasisi za Kimataifa zifuatazo: Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, AU, IFAD, DFID, UNDP, FAO, JICA, EU, ENABEL, GIZ, UNICEF, WFP, CIMMYT, ICRISAT, ASARECA, USAID, KOICA, ICRAF, IITA, IRRI, ILRI na CABI. Nyingine ni EAC, SADC, AVRDC, AGRA, KILIMO TRUST, CIP, CIAT/PABRA, UNEP, WARDA, Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani (DLCO-EA) na HELVETAS. Wadau wengine ni Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu (IRLCO-CSA), Bill and Melinda Gates Foundation, Gatsby Trust, Rockfeller Foundation, Clinton Foundation, Aga Khan Foundation, TAHA na Asasi zisizo za kiserikali nyingi ambazo hatuwezi kuzitaja zote hapa.

75. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani kwa wakulima wote kwa kazi kubwa wanazofanya kuendeleza kilimo nchini. Ni wazi kuwa mafanikio ya kilimo yanatokana na juhudi na ushirikiano mkubwa na Serikali. Kipekee nirudie kuwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Rombo kwa namna wanavyoniunga mkono na kunipa ushirikiano. Naomba wote watambue kuwa kilimo ni maisha, uchumi, biashara, viwanda na ajira.


7. MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2021/2022
7.1 Makusanyo ya Maduhuli

76. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara inatarajia kukusanya Shilingi 34,495,000,000 kutokana na ada za ukaguzi wa mazao yanayouzwa nje ya nchi au kuingizwa nchini, uuzaji wa nyaraka za zabuni, ukodishaji wa mitambo ya Tume ya Umwagiliaji. Kati ya fedha hizo, Shilingi 4,480,000,000 zitakusanywa katika Fungu 43 na Shilingi 30,015,000,000 zitakusanywa kwenye Fungu Na.05.
7.2 Fedha kwa Mafungu yote (43, 24 na 05)

77. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara ya Kilimo inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 294,162,071,000 kupitia Fungu 43, Fungu 05 na Fungu 24 kama ifuatavyo;
7.2.1 Fedha kwa Fungu 43

78. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 228,871,243,000 kupitia Fungu 43 kwa ajili ya matumizi ya Kawaida na Maendeleo.

Kati ya fedha hizo, Shilingi 164,748,000,000 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 82,180,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 82,568,000,000 ni fedha za nje. Aidha, Shilingi 64, 123,243,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ambapo Shilingi 42,492,457,000 ni kwa ajili ya mishahara na Shilingi 21,630,786,000 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
7.2.2 Fedha kwa Fungu 05

79. Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi 51,487,450,000 zinaombwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 46,500,000,000 ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 35,000,000,000 ni fedha za Ndani na Shilingi 11,500,000,000 ni fedha za Nje. Aidha, kati ya fedha zinazoombwa, Shilingi 4,987,450,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Shilingi 3,349,266,000 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Tume na Shilingi 1,638,184,000 ni kwa ajili ya Matumizi mengineyo.
7.2.3 Fedha kwa Fungu 24

80. Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi 13,803,378,000 zinaombwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 6,549,009,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ya Tume na Shilingi 4,654,984,000 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Tume. Aidha, Shilingi 1,000,000,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya kawaida ya COASCO na Shilingi 1,599,385,000 ni kwa ajili ya mishahara ya COASCO.

81. Mheshimiwa Spika, hotuba hii pia inapatikana katika tovuti ya Wizara: www.kilimo.go.tz


8. HITIMISHO

82. Mheshimiwa Spika, NAOMBA KUTOA HOJA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news