MWELEKEO WA HALI YA HEWA KWA TANZANIA KIPINDI CHA JUNI – AGOSTI (JJA), 2021


Dondoo muhimu za hali ya hewa kipindi cha Juni-Agosti (JJA), 2021kutoka TMA.


Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na hali ya hewa inayotarajiwa katika msimu wa kipupwe kwa miezi ya Juni hadi Agosti (JJA), 2021; Ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao. Kwa kawaida, kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti (JJA), huwa ni kipindi cha baridi na kipupwe kwa maeneo mengi ya nchi. Kwa muhtasari, mwelekeo huo na athari zake unaonesha kuwa:

a) Viwango vya joto

• Kwa ujumla katika kipindi cha JJA, 2021 hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa ya kawaida katika maeneo mengi ya nchi.

• Hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa ya juu kidogo ya kiwango cha kawaida katika maeneo ya ukanda wa pwani, nyanda za juu kaskazini mashariki, ukanda wa Ziwa Victoria na magharibi mwa nchi. Aidha katika maeneo ya kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi na mkoa wa Ruvuma hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa chini kidogo ya joto la kawaida kama ilivyozoeleka.

• Vipindi vya baridi kali zaidi vinatarajiwa kujitokeza mwezi Julai.

• Vipindi vya baridi kali vinatarajiwa katika maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kusini magharibi hususan nyakati za usiku na asubuhi.

b) Upepo

• Katika kipindi cha miezi ya Juni na Agosti, 2021 vipindi vya upepo mkali wa Kusi vinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Zaidi ya hapo, katika msimu wa mwaka huu, vipindi vya upepo unaovuma kutoka kusini-mashariki na mashariki (Matlai) vinatarajiwa katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo ya mwambao wa pwani hususan mwezi June, 2021. Hali hii inatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na kusababisha vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na ukanda wa pwani (Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara)

c) Athari

• Hali ya ukavu, upepo na ubaridi inaweza kusababisha athari kwa binadamu, wanyama na mazao.

• Jamii inashauriwa kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi mazuri ya maji na kujikinga ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa inayotarajiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news