Rais Samia ateua wakuu wa mikoa, watendaji wakuu wa taasisi

Na Mwandishi Diramakini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa na watendaji wakuu wa Taasisi, taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo kutokea Zanzibar imesema, Rais Samia amefanya uteuzi huo kama ifuatavyo;

Amemteua aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Simiyu Anthony John Mtaka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, huku aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Rajab Telack kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kuchukua nafasi iliyoachwa na Godfrey Zambi ambaye amestaafu.

Aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Geita Robert Gabriel Luhumbi ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, huku Rais akimteua aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Zuberi Homera kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Tanga Martin Reuben Shigella kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuchukua nafasi ya Loata Erasto Ole Sanare ambaye amemaliza muda wake.

Pia Rais anemteua aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kagera Mej. Jen. Marco Elisha Gaguti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na anachukua nafasi ya Gelasius Gasper Byakanwa ambaye Taarifa imesema atapangiwa majukumu mengine, huku aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya Albert Chalamila akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Taarifa ya Ikulu imesema aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Aboubakar Mussa Kunenge ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani kuchukua nafasi ya Mhandisi Evarist Welle Ndikilo ambaye amestaafu.

Naye aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Manyara Joseph Joseph Mkirikiti ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kuchukua nafasi ya Joachim Leonard Wangabo ambaye amestaafu, huku aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Satano Mahenge akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida kuchukua nafasi ya Dk. Rehema Nchimbi ambaye amestaafu.

Pia Rais amemteua aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Tabora Dk. Philemon Rugumiliza Sengati kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga huku aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mwanza John Vianney Mongella akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Naye Ally Salim Hapi ambaye alikuwa mkuu wa mkoa wa Iringa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora huku aliyekuwa mkuu wa mkoa wa wa Mara Adam Kigoma Malima akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Taarifa ya Ikulu imesema Rais amemteua David Zacharia Kafulila kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuchukua nafasi ya Idd Hassan Kimanta ambaye amestaafu. (Kafulia ameshika wadhifa huo kwa mara ya kwanza).

Pia Rais amemteua Amos Gabriel Makalla kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kuchukua nafasi ya Aboubakar Mussa Kunenge ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, huku Rosemary Staki Senyamule akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kuchukua nafasi ya Robert Gabriel Luhumbi ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Taarifa ya Ikulu imesema Rais amemteua Queen Cuthbert Sendiga kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuchukua nafasi ya Ali Salim Hapi ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa Tabora huku Brig. Jen. Charles Mbuge akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuchukua nafasi ya Mej. Jen. Marco Elisha Gaguti ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

Rais pia amemteua Mwanamvua Mrindoko kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi kuchukua nafasi ya Juma Zubeir Homera ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, huku aliyekuwa Katibu wa Bunge Stephen Kagaigai akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na anachukua nafasi Anna Elisha Mghwira ambaye amestaafu.

Jen. Wilbert Augustine Ibuge yeye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuchukua nafasi ya Christine Mndeme ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku Omary Tebweta Mgumba akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe kuchukua nafasi ya Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ambaye amestaafu.

Taarifa ya Ikulu imesema Rais amemteua Makongoro Nyerere kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara anachukua nafasi ya Mkirikiti ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, huku Rais akimteua Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Emir Andengenye kuendelea na wadhifa huo katika Mkoa huo huo wa Kigoma.

Pia Rais amemteua Mkuu wa mkoa wa Njombe Marwa Mwita Rubirya kuendelea na wadhifa huo huo katika Mkoa huo huo wa Njombe.

Kuhusu uteuzi wa Watendaji Taarifa ya Ikulu imesema Rais Samia amefanya uteuzi wa watendaji wakuu wa taasisi zifuatazo;

Amemteua Balozi Joseph Edward Sokoine kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuchukua nafasi ya Brig. Jen. Ibuge ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Pia Rais amemteua Nenelwa Mwihambi kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchukua nafasi ya Stephen Kagaigai ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Dk. Edwin Paul Mhede kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) kuchukua nafasi ya John Nguya ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Taarifa imese Sylvester Antony Mwakitalu ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuchukua nafasi iliyoachwa na Biswalo Mganga ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, huku Joseph Pande akiteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka (DDPP) kuchukua nafasi ya Edson Athanas Makallo ambaye Rais amesema atapangiwa majukumu mengine.

Pia Rais amemteua Kamishna Msaidizi wa polisi (ACP) Salum Rashid Hamduni kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchukua nafasi ya Brig. Jen. John Mbungo ambaye Rais amesema atapangiwa majukumu mengine pia Rais Samia amempandisha cheo ACP Hamduni kuwa Kamishna wa Polisi (CP).

Taarifa hiyo ya Ikulu imesema Rais amemteua pia Neema Mpembe Mwakalyelye kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na kukamilisha Taarifa hiyo kwamba Uteuzi wa viongozi hao unaanza leo tarehe 15 Mei, 2021 na wataapishwa tarehe 18 Mei, 2021 kuanzia saa 9:00 alasiri, Ikulu Jijini Dar es Salaam.




Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news