Serikali yawaomba wadau kuboresha taasisi za watu wenye ulemavu

Na Mwandishi Diramakini (Dar es Salaam)

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, ametoa wito kwa wadau mbali mbali wa maendeleo kusaidia kuboresha miundo mbinu katika vyuo vya ufundi vya watu wenye ulemavu ambavyo vipo katika kanda zote hapa nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akihutubia katika hafla ya kukabidhi mabweni ya Chuo cha Ufundi Stadi Yombo yaliyokarabatiwa na Shirika la Nyota Foundation. Wengine ni Naibu Waziri wake (Watu wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga (wa pili kulia), Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof, Jamal Katundu (kushoto) na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa (wa kwanza kulia).

Ametoa wito huo jijini Dar es Salaam alipokuwa akipokea mabweni mawili katika chuo cha Ufundi Stadi kwa watu wenye ulemavu cha Yombo ambayo yamefanyiwa ukarabati na Shirika lisilo la kiserikali la Nyota Foundation kwa gharama ya shilingi milioni themanini.

“Sisi kama serikali tumejitahidi sana kuboresha vyuo hivi lakini niwaombe wadau wengine, makampuni, taasisi mbali mbali za kitaifa na kimataifa waviangalie sana vyuo vyetu. Vyuo hivi vinakabiliwa na changamoto kubwa ya uchakavu wa miundo mbinu mbali mbali pamoja na upungufu wa miundombinu muhimu vikiwemo vyoo, madarasa, mabweni na miundombinu nyinginezo," amesema Mhagama.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, katika hafla ya kupokea mabweni ya Chuo cha Ufundi Stadi Yombo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akishiriki kukata utepe kama ishara ya kupokea mabweni ya Chuo cha Ufundi Stadi Yombo yaliyokarabatiwa na Shirika la Nyota Foundation. Alioambatana nao ni Naibu wake, Ummy Nderiananga, Naibu Katibu Mkuu, Prof. Jamal Katundu, Wawakilishi kutoka Nyota Foundation pamoja Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa.

Kwa mujibu wa Waziri Mhagama, kwa takwimu za mwaka 2019/2020, Tanzania ilikuwa na jumla ya watu 55.9 milioni; Kati ya idadi hiyo, watu milioni 2.5 ni wenye ulemavu na hivyo kuongeza mahitaji ya huduma na miundo mbinu mbali mbali kwa ajili ya kundi hilo.

Awali, akimkaribisha Waziri Mhagama katika hafla hiyo, Naibu wake anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, amempongeza Kiongozi huyo wa Wizara kwa kujitoa kwake katika kuboresha mazingira na hali za watu wenye ulemavu kupitia kuwashirikisha wadau mbali mbali wa maendeleo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akiwa ameongozana na wawakilishi wa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo wakati wa hafla ya kupokea mabweni ya chuo hicho yaliyokarabatiwa na Shirika la Nyota Foundation.

Mwakilishi wa Shirika la Nyota Foundation, Zainab Mvungi, ameishukuru serikali kwa kuruhusu ukarabati huo kufanyika pamoja na kutoa ushirikiano wakati wote walipokuwa wakifanya kazi hiyo.

Chuo cha Ufundi Stadi Yombo kinachomilikiwa na serikali kilianzishwa mwaka 1973. Chuo hicho ambacho ni kwa ajili ya Kanda ya Mashariki ni miongoni mwa vyuo sita (6) ambavyo vipo katika kanda mbali mbali hapa nchini kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu nchini. Vyuo vingine vipo Kanda ya Kusini (Mtwara), Magharibi (Tabora), Ziwa (Mwanza), Kaskazini (Tanga) na Kati (Shiyanga).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news