Vigogo wa CHADEMA wakiongozwa na Mbowe wazidi kuchanja mbuga

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amewataka wanachama wa chama hicho kuendelea kushirikiana hasa katika masuala ya kujenga chama ikiwemo ujenzi wa ofisi hali itakayowaondolea usumbufu wa kwenda kupanga nyumba binafsi.
Kauli hiyo ameitoa mkoani Shinyanga, mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa ofisi za chama hicho katika Jimbo hilo.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Mbowe amesema wanawake 19 waliofukuzwa uanachama baada ya kuapishwa kuwa wabunge bila idhini ya chama hicho ni wapambaji baada ya kujengewa msingi mzuri.

Mheshimiwa Mbowe amesema licha ya kukisaliti chama hicho, bado kina wanachama wengi wanawake wanaoweza kufanya kazi nzuri ya kuijenga Chadema na kuleta mabadiliko makubwa.

Wanawake hao 19, akiwemo Halima Mdee walivuliwa uanachama Novemba, 2020 baada ya kuapishwa kuwa wabunge bila ridhaa ya chama hicho. Hata hivyo licha ya kufukuzwa uanachama, walikata rufaa katika baraza kuu la chama hicho.

Amesema hayo katika kikao cha ndani cha Chadema mkoani Shinyanga huku akigusia katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia 2015 wanachama wa chama hicho walivyopitia wakati mgumu.

Amewataka wanachama kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutetea haki zao ili kupiga hatua zaidi kwani kazi imeanza na inaendelea hadi mwaka 2025.

Mbowe pamoja na viongozi wengine anaendelea na ziara katika mikoa mbalimbali ikiwa ni harakati za kuendelea kukiimarisha chama hicho.

Mwishoni mwa 2020

Waliovuliwa uanachama ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Mwishoni mwa mwaka jana, kabla ya kutangaza uamuzi huo, Mheshimiwa Mbowe alitaja hatua nyingine tatu ambazo kamati kuu ilizichukua ikiwa ni pamoja na kuwavua nyadhifa miongoni mwao waliokuwa viongozi wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) na lile la wanawake (Bawacha) na kuagiza mchakato wa kujaza nafasi zao uanze mara moja.

“Tumeagiza kurugenzi yetu ya kisheria itafute taratibu mbalimbali za kisheria kupinga mchakato wa kuwapata wabunge 19 wa Chadema kwa sababu mchakato huo ni batili kuanzia hatua ya mwanzo maana wameghushi majina na waliopelekewa majina nao wameyapokea,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema, licha ya kuwaita kuhojiwa hawakutokea huku wakitoa sababu zinazofanana kwamba waongezewe siku saba wajitafakari kwa madai wanahofia usalama wao kwa madai kuwa kuna wanachama walijipanga kuwafanyia vurugu.

Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema walikuwa wana nafasi ya kuomba radhi ili kurejeshewa uanachama wao na kama hawakuridhika na uamuzi huo wana haki ya kukata rufaa.

“Kikao cha kamati kuu hakikufanyika makao makuu ya chama tulikifanya katika hoteli ya Ledger Plaza (zamani Bahari Beach) Ili kuhakikisha wanakuwa huru zaidi ila wao hawakuja wote na pia tuliwapigia simu kusisitiza waje, hawa dada zetu wamekumbwa na nini,” alisema Mbowe wakati huo, ingawa bado kina Halima wanaendelea kuhudumu nafasi ya Ubunge.

Post a Comment

0 Comments