Wakazi wa Vikindu watakiwa kusitisha shughuli zao eneo la msitu kwa hofu ya Simba

Na Diramakini (diramakini@gmail.com)

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, Filberto Sanga amewataka wananchi wanaoishi katika eneo linalozunguka msitu wa Vikindu kusitisha kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo utalii, uvuvi na uwindaji katika Msitu huo hii ni kutokana na taharuki iliyotokea kwa kudhaniwa kuwa na Simba katika eneo hilo la hifadhi.
Akizungumza katika viunga vya Msitu huo jana 18/5/2021 mara baada ya kuwasili kwa lengo la kuambatana na askari wa wanyamapori katika doria ya kuwasaka simba hao Sanga alisema tayari shughuli za kuwatafuta Simba zimeshaanza hivyo anawataka wananchi wote kusitisha shughuli zote ambazo ameziainisha.

Aidha, Sanga alisisitiza kwa kusema wakati uliopo ni wa kuwatafuta simba ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea kutokana na uwepo wa wanyama hao na hakuna mda wa kushughulikia vitu vingine katika eneo hilo hivyo shughuli zote zisimame mara moja.

Mkuu wa Wilaya alisema simba hao wameanza kutajwa katika Wilaya kuanzia jumatatu katika maeneo ya kisiju Pwani kisha kinamama walikwenda kuchita maji mtoni maeneo ya utunge kata ya mwandege na vijana wengine huko kipala mpakani waliwaona walipoenda kutafuta kamba.

Yohana Awise ni miongoni mwa wananchi waliowaona Simba hao Jike na Dume wakati walipokua wanavua samaki katika mto Mkangaza ambao upo katika msitu huo wa Vikindu. 

Yohana aliongezea kwa kusema anaiomba serikali kuharakisha kuondoa simba hao haraka ili kupunguza taharuki kwa wananchi wanaoishi karibu na eneo la msitu na hata wale wanaokuja katika eneo hilo kwa lengo la kufanya utalii na shughuli zote za kibinadamu.

Naye Bi. Zawadi Malunda Mdhibiti na Mhifadhi wa Wanyamapori, wanyama wakali na waharibifu (TAWA) alisema tayari wapo katika eneo la tukio na tayari wameshaanza juhudi za kuwasaka simba hao, ambapo ameahidi kutoondoka katika msitu huo hadi watakapofanikiwa kuwapata simba hao.

Malunda alimalizia kwa kusema anaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa kila wanapobaini mnyama yoyote wa tofauti katika maeneo yao ili kufanikisha upatikanaji wa haraka wa Simba hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news