WANARIADHA 400 WATIMUA VUMBI HAYDOM MARATHON

NA MWANDISHI DIRAMAKINI, Manyara

Wanariadha 400 wametimua vumbi kwenye mashindano ya riadha ya Haydom Marathon wilayani Mbulu mkoani Manyara, lengo likiwa ni kujenga wodi ya watoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tiba wa Hospitali ya Rufaa ya Haydom, Dkt.Paschal Mdoe amesema, watu mbalimbali wamejitokeza kushiriki mbio hizo.

Dkt. Mdoe amesema ujenzi wa wodi hiyo ya watoto unatarajia kuanza rasmi wakati wowote mwaka huu.

Mgeni rasmi wa michuano hiyo, Naibu Waziri wa Tamisemi, David Silinde amesema anatoa shilingi milioni 2 kwenye ujenzi wa wodi hiyo ya watoto.
“Pamoja na hayo mtanipatia karatasi ya orodha ya kuchangia ili niende nayo Bungeni tukasaidiwe kuchangia na kiasi cha pesa kitakachopatikana kitawasilishwa,” amesema Silinde.

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Dkt. Chelestino Mofuga amesema, anaunga mkono ujenzi huo kwa kujitolea shilingi milioni moja.

Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Maasay amesema amejitolea shilingi 1.5 milioni kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa wodi hiyo.
Katika mashindano ya kilomita 21 mwanariadha wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Joseph Panga alishika nafasi ya kwanza kwa wanaume na kujipatia sh.500,000 na medali ya dhahabu.

Panga alifuatiwa na Josephat Gisemo wa Polisi aliyepata sh.400,000 na medali ya fedha na watatu ni Shingade Giniki wa Katesh wilayani Hanang’ aliyepata sh.300,000 na medali ya shaba.
Kwa upande wa wanawake, kilomita 21 Failuna Matanga wa Arusha alishika nafasi ya kwanza na kujipatia sh.500,000 na medali ya dhahabu.

Grace Jackson wa JKT, alishika nafasi ya pili na kujipatia sh.400,000 na medali ya fedha na watatu ni Angela John wa Arusha aliyepata sh.300,000 na medali ya shaba.

Post a Comment

0 Comments